Thursday, May 17, 2012


NI KATIKA JENGO LA WIZARA YA NISHATI   NA MADINI, WAZIRI AMWOMBA RADHI
James Magai
 BALOZI wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt jana alikwama ndani ya lifti katika Jengo la Wizara ya Nishati na Madini, Dar es Salaam kwa takriban dakika 20.

 Balozi Lenhardt akiwa  na ujumbe wake wa watu wawili,  walikumbwa na mkasa huo mchana wakati wakienda kukutana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Mbali na Balozi Lenhardt na ujumbe wake, pia kulikuwamo na watu wengine wakiwemo maofisa wa wizara hiyo na kufanya jumla ya watu saba kukwama kwenye lifti hiyo.

Saa 7:58 mchana mwandishi wetu alipofika wizarani hapo, alimkuta balozi huyo na wenzake hao wakiwa wamekwama ndani ya lifti hiyo katika ghorofa ya kwanza huku ofisa wa mapokezi wizarani hapo akihangaika kufanya mawasiliano na mafundi.

Mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo alifanikiwa kuifungua na kuacha uwazi wa kama sentimita 10 na kisha kuweka kibao ambacho kiliifanya iwe wazi lakini bila ya kuwawezesha waliokuwamo ndani kutoka.
Hatua hiyo iliwawezesha Balozi huyo na wenzake walau kupata hewa wakati wakisubiri hatua zaidi za kuwakwamua. walibaki humo hadi ilipotimu saa 8:14 mchana walipokwamuliwa baada ya mafundi waliokuwa wamefika muda mfupi kabla, kufanikiwa kuifungua.

Kutokana na tukio hilo, mkutano wa Balozi huyo na Waziri Profesa Muhongo uliokuwa umepangwa kuanza saa 8:00 ulichelewa kwa zaidi ya nusu saa kusubiri wageni hao wakwamuliwe. Ingawa hakuna ofisa wa wizara hiyo aliyekuwa tayari kuzungumzia mkasa huo wa kukwama kwa lifti hiyo, ilielezwa kwamba tatizo hilo limetokana na lifti hiyo kuwa mbovu.

Mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo ambaye hata hivyo, jina lake halikuweza kupatikana mara moja alisikika akisema kuwa lifti hiyo ina kawaida ya kukwama.

Baada ya kufanikiwa kutoka, Balozi huyo na maofisa aliokuwa ameambatana nao pamoja na maofisa wengine wa wizara waliingia katika chumba cha mkutano na kuendelea na mazungumzo.
Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, Waziri Profesa Muhongo alimtaka radhi Balozi Lenhardt na ujumbe wake kwa tukio hilo lakini akamtania kuwa bila shaka amepata uzoefu wa tatizo la nishati nchini, maelezo ambayo Balozi huyo aliyeitikia huku akicheka.

Ziara ya Balozi Lenhardt na ujumbe wake wizarani hapo ilikuwa na lengo la kumpongeza Profesa Muhongo kwa kuteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo na kuangalia jinsi ambavyo Marekani itaendelea kuisaidia Tanzania kuboresha sekta hiyo.

 Katika mazungumzo hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Manaibu Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene na Stephen Maselle na maofisa wengine wa wizara, yalijikita zaidi katika sekta ya Nishati.

Waziri Profesa Muhongo alimweleza balozi huyo umuhimu wa  nishati  katika maendeleo ya taifa na changamoto ambazo zinaikabili sekta hiyo, kiasi cha kufanya kutokuwa na uhakika wa upatikanaji wake.
Pia Profesa Muhongo alimweleza balozi huyo hatua na mikakati ambayo Serikali kupitia wizara yake imekuwa ikiichukua na inayotarajia kuichukua kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa nishati ya kutosha na ya uhakika.

“Kipaumbele cha wizara kwa sasa ni kupata umeme uhakika wa bei nafuu na unaotabirika. Ni muhimu kuongeza watumiaji wa umeme kwa kuwa kwa sasa kwa takwimu za Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania), ni asilimia 18.4 tu ya Watanzania wanaopata huduma ya umeme,” alisema.
Katika kuongeza watumiaji wa umeme, Profesa Muhongo alisisitiza kupunguza gharama za upatikanaji wa umeme majumbani, mashambani na viwandani.

Alisema lengo la kuweka msisitizo katika nishati ni kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), ili kufikia mwaka 2025 iwe ni nchi ambayo wananchi wake wanapata kipato cha kati... “Ili kufikia hilo lazima tupate umeme wa kutosha wa uhakika na wa bei rahisi.”

Akizungumzia umuhimu wa nishati katika kutengeneza ajira na kuinua uchumi, Profesa Muhongo alisema ni lazima kuinua na kuboresha sekta ya kilimo kwa kuwa ndiyo itakayoweza kuondoa tatizo hilo.“Lakini, inahitaji nishati. Sisi tunatengeneza mambo yetu sawasawa ili kusaidia sekta ya kilimo ikue na itoe ajira na chakula cha kutosha na hivyo kupunguza mfumuko wa bei. Dawa ya mfumuko wa bei ni umeme, kama haupatikani ni vigumu kuupunguza,” alisema.

Balozi Lenhardt kwa upande wake,  alisema Marekani iko tayari kushirikiana na Tanzania kutatua tatizo la nishati nchini.Alimkabidhi Profesa Muhongo mpango mkakati wa namna ya kushirikiana katika kukabiliana na tatizo hilo, ambao umeandaliwa na wataalamu wa Tanzania na Marekani.
Baada ya mazungumzo hayo, Profesa Muhongo alisema wizara kwa upande wake itakaa na kuandaa dokezo ambalo litatumika kuangalia namna ya kuanza na kutekeleza mpango huo.

0 comments:

Post a Comment