Tuesday, May 22, 2012

Habel Chidawali, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewataka wakuu wa mikoa, makatibu tawala na wakuu wa wilaya nchini kutojihusisha na siasa badala yake washirikiane na wananchi katika kuleta maendeleo.Kauli ya Pinda imekuja huku kukiwa na madai kwamba baadhi ya wawakilishi hao wa Rais katika ngazi ya mikoa na wilaya kujihusisha na siasa.

Akizungumza na wakuu hao mjini hapa jana, Pinda pia aliwataka viongozi hao kuacha umangimeza na kujitoa zaidi katika kutafuta suluhisho la matatizo yanayowakabili wananchi badala ya wao kuwa sehemu ya matatizo hayo.

Waziri Mkuu alikuwa akifungua mafunzo maalumu ya siku 10 kwa viongozi hao yaliyoanza jana.Katika hotuba aliyoisoma kwa zaidi ya saa tatu, Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa weledi na maarifa huku akionya kuwa iwapo watajihusisha na mambo ya siasa, ni wazi kuwa wanaweza kujikuta wanamezwa na wajanja.
“Ninawaonya, msitumbukie katika siasa na wala msijaribu kabisa. Huko kuna vyama vingi vitumikieni vyote ingawa kwa sehemu kubwa mtatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo simameni kidete ndugu zangu,’’ alisema Pinda.
“Katika maeneo mengi, baadhi ya viongozi wamekuwa wakijifanya miungu watu na matokeo yake wanakiuka maadili ya kazi zao na kufanya ufanisi wa kazi kushuka kwa kiasi kikubwa,” alisema.Akinukuu maneno ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Waziri Mkuu alisema: “Kiongozi anayetakiwa kwa Taifa letu, lazima awe anakerwa na matatizo ya wananchi.”

Pinda alisema viongozi hao watapaswa viongozi wa aina hiyo baada ya kumaliza mafunzo hayo.“Ninyi kama viongozi na watendaji wakuu katika maeneo yenu ni timu muhimu katika kufahamu changamoto, matatizo na kero walizonazo wananchi hasa wale wanaoishi vijijini ambao ni asilimia 80 ya Watanzania wote,” alisema.

Alikemea tabia ya baadhi ya viongozi kukaa maofisini kwa muda mrefu bila ya kuwafuata wananchi na kusikiliza kero zao jambo alilosema ni hatari kwa kiasi kikubwa na linazorotesha maendeleo.
Pinda alisema biashara ya dawa za kulevya pamoja na uhamiaji haramu ni matatizo makubwa yanayoikabili nchi kwa sasa.
Aliwataka viongozi hao kuondoa visingizio na kupambana kwa hali na mali katika kukomesha vitendo vyote viovu katika maeneo yao kwa kutumia sheria halali huku wakitahadharisha mfumo wa mazoea kuachwa mara moja.
Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyetarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo lakini, Waziri Mkuu alisema yupo nje ya nchi kikazi na alitarajiwa kuwasili jana jioni kabla ya kufika Dodoma leo jioni na kuungana na washiriki katika mkutano huo.
Alisema baada ya mafunzo hayo kila mmoja atapaswa kujiuliza kiwango cha umaskini katika eneo alilopangiwa na kuangalia pato la wastani la mwananchi katika wilaya au mkoa wake na kuainisha kama ongezeko la idadi ya watu katika mkoa au wilaya yake linaendana na ukuaji wa uchumi katika eneo husika.

“Mnapaswa pia kuzijua na kuzitambua fursa za kiuchumi zilizopo ndani ya mkoa au wilaya husika; mziainishe ni fursa zipi za kiuchumi za haraka zinazoweza kumtoa mwananchi kwenye umaskini na zaidi ya yote myaangalie ni kwa namna gani mwananchi wa kawaida atawezeshwa kutumia fursa zilizopo kuondoa umaskini unaomzunguka.”

Aliwataka kuhakikisha kuwa maeneo yao yanakuwa na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa viwango stahiki na nidhamu katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma na kujiridhisha kuwa zinatumika kwa manufaa ya wananchi.

“Ninawasihi sana mkasimamie vizuri ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri zenu kwa sababu ndiko viliko vyanzo vikuu vya mapato. Katika bajeti iliyopita, halmashauri zilipanga kukusanya Sh320 bilioni lakini, hadi kufikia Januari mwaka huu, ni Sh90 bilioni tu ambazo zilikuwa zimekusanywa.”

Aliwataka wahakikishe kuwa mikoa na wilaya zao zina akiba ya chakula cha kutosha... “Ni aibu kwa RC au DC kuomba chakula kwani si kweli kwamba hapakuwa na fursa nyingine za kuepuka hali hiyo. Fursa za kuzalisha mazao mbadala zipo, himizeni watu wenu walime mazao yanayostahimili ukame, yanayokomaa kwa muda mfupi na ikibidi muwasisitize wazalishe chakula cha ziada ili wawe na akiba ya kutosha na pia waweze kuuza na kupata fedha.”

Mada
Kwa siku hizo 10, wakuu hao wanatarajiwa kujadili mada 39 zitakazotolewa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri. Mada ya jana ambayo ni ya kwanza ilitarajiwa kutolewa na mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru na kufuatiwa na za, Waziri wa Elimu na Mafunzo, Dk Shukuru Kawambwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.
Wengine watakaotoa mada ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Othuman Rashid, Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah, Mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya maoni ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ambaye atazungumzia masuala ya Katiba pamoja na watumishi wengine wa kada mbalimbali.
Mafunzo hayo yanahudhuriwa na Wakuu wa Mikoa 24, Makatibu Tawala wa Mikoa 25 na Wakuu wa Wilaya 133.

Uteuzi wa Ma-DC
Akizungumzia uteuzi wa wakuu wa wilaya uliofanywa hivi karibuni, Pinda alisema kazi hiyo ilikuwa ngumu na iliwachukua siku 10 mfululizo huku akidokeza kuwa walilazimika kuwatema wengine katika dakika za mwisho kutokana na sababu mbalimbali.

CHANZO CHA HABARI http://www.mwananchi.co.tz/habari/49-uchaguzi-mkuu/23177-pinda-wakuu-wa-mikoa-wilaya-acheni-siasa

0 comments:

Post a Comment