Tuesday, May 22, 2012


James Magai
UPELELEZI wa kesi ya muigizaji wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu anayekabiliwa na  kesi ya mauaji bado haujakamilika.

Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Lakini jana Wakili wa Serikali, Ladislaus Komanya aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine.
Hakimu Agustina Mmbando aliahirisha kesi hiyo na hadi June 4, 2012 itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Hata hivyo jana Mahakama ya Kisutu ilibidi itumie jalada la muda kwa kuwa jalada halisi la kesi hiyo limepelekwa Mahakama Kuu na hakimu Mmbando alisema kuwa bado halijarudi.

Jalada hilo lilipelekwa Mahakama Kuu Ijumaa ya Mei 18 baada ya jopo la Mawakili wa mshtakiwa  huyo kuwasilisha maombi huko juu ya uchunguzi kuhusiana na umri halali wa msanii huyo.

Umri wa mshtakiwa huyo umezua utata kama ni mtoto au ni mtu mzima, jambo ambalo limewalazimu mawakili hao kuwasilisha maombi hayo ya uchunguzi wa umri wake Mahakama Kuu.
Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo  na Wakili Peter Kibatala Mei 15, 2012 na yamepangwa kusikilizwa  na Jaji Dk Fauz Twaib Mei 28, 2012.

Mawakili wa mshtakiwa huyo walifikia uamuzi wa kwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu baada ya kugonga mwamba Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kabla ya kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu, mawakili hao mawakili hao waliwasilisha maombi  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 7,2012  wakiiomba iamuru kesi ya msanii huyo isikilizwe katika mahakama za watoto wakidai kuwa bado ni mtoto.

Mawakili hao walidai mahakamani hapo kuwa msanii huyo ana umri wa miaka 17 na kwamba kwa maana hiyo yeye bado ni mtoto na kesi yake haipaswi kusikilizwa katika mahakama za kawaida kama mtu mzima.
Kiongozi wa jopo la mawakili wanaomtetea msanii huyo wakili Kenedy Fungamtama alidai kuwa mteja wao ana umri wa miaka 17 na si 18 kama inavyotamkwa mahakamani.

Alidai kuwa hata cheti cha kuzaliwa walichokiwasilisha mahakamani kinaonyesha mahali na tarehe aliyozaliwa mshtakiwa hivyo kuwa na umri wa miaka 17.

“Sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inatafsiri kuwa mtoto ni yule aliyekuwa na umri chini ya miaka 18 hivyo katika suala la mteja wetu alipaswa kushtakiwa katika mahakama ya watoto,” alidai Wakili Fungamtama.

Hata hivyo upande wa mashitaka kupitia kwa wakili Elizabeth Kaganda ulipinga maombi hayo na kudai kuwa bado wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo na hivyo kuomba wapewe muda zaidi.

0 comments:

Post a Comment