Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe (kulia)
akizungumza na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (kushoto) nje ya Bunge mjini
Dodoma hivi karibuni.
Filikunjombe akiwa Mbunge wa Ludewa (CCM)
mkoani Iringa, alisimama imara akiongoza mashambulizi dhidi ya mawaziri
wasiokuwa waadilifu katika utendaji kazi wao, hata kufikia hatua ya
kuichafua serikali iliyopo madarakani.
Akitumia ushahidi wa ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa kwenye Mkutano wa
Saba wa Bunge uliofikia ukomo wake hivi karibuni mjini Dodoma,
Filikunjombe aliamini na kuusimamia ukweli, kwamba baadhi ya mawaziri
hawawajibiki ipasavyo.
Mapema wiki hii, NIPASHE Jumapili ilimhoji
Filikunjombe ambapo pamoja na mambo mengine, anasema mawaziri hao na
watendaji wengine waliotajwa kwenye ripoti ya CAG, walipewa majukumu
walioshindwa kuyatekeleza.
KUINUSURU CCM
Filikunjombe anasema mkakati alioshiriki
bungeni kwa mujibu wa kanuni za chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi,
ulilenga kuinusuru CCM na serikali yake dhidi ya kupoteza mvuto na
kukubalika kwa umma.
“Chama hakina tatizo lolote, lakini sioni
kama baadhi ya mawaziri waliokabidhiwa dhamana za uongozi wanatekeleza
majukumu na wajibu wao ipasavyo,” anasema.
Filikunjombe anasema kujenga hoja dhidi ya
mawaziri wa serikali ya CCM, hakukuwa na maana ya kuibua mapinduzi,
bali kuchagiza mabadiliko yatakayosukuma mbele maendeleo ya nchi na watu
wake.
Anasema serikali ikisimamiwa vizuri na
Bunge, itayafikia matakwa ya umma na hivyo kukifanya chama hicho (CCM)
kudumu madarakani kwa muda mrefu.
“Tuhuma zinazowakabili mawaziri husika ni
moja ya maeneo yanayoiathiri jamii pana ya Tanzania hivyo hakuna sababu
ya kuweka mbele maslahi ya kisiasa, lazima tufike mahali kama hapa
tulipo sasa, tupiganie maslahi ya umma,” anasema.
MCHANGO WA WABUNGE WA CCM
Filikunjombe anasema hoja ya kuwataka
mawaziri waliotuhumiwa kwa wizi ama kutowajibika kwa mujibu wa nyadhifa
zao wajiuzulu, ilipata nguvu sana kutokana na kuzungumzwa na wabunge wa
CCM.
Anasema, “hoja hii ingesimamiwa na akina
Zitto Kabwe isingekuwa na nguvu, kwa maana watu wangesema ni kawaida ya
upinzani, lakini wabunge wa CCM tuliposimama na kuzungumza, imeleta
matokeo makubwa.”
Filikunjombe alisema hali ya ustawi wa
jamii imedumaa huku baadhi ya viongozi wa serikali wakiwemo mawaziri
wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wakijilimbikizia mali kinyume cha sheria.
Anasema hali inawawia ngumu wabunge hasa
wa CCM wanapokuwa majimboni, wakihojiwa kuhusu kutofikiwa kwa ahadi ya
maisha bora kwa kila Mtanzania, huku baadhi ya mawaziri wakizidi
kujineemesha.
“Kama kule kwangu Ludewa, wananchi
wanahoji kuhusu ukosefu wa huduma bora za afya, elimu, miundombinu na
maji safi na salama, kwa hali ilivyo sasa na hulka hii ya mawaziri
wasiokuwa waaminifu kuhujumu rasilimali za nchi, si rahisi kuyafikia
maisha bora kwa kila Mtanzania.” Anasema.
WIZI KWENYE HALMASHAURI
Filikunjombe anasema ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoashiria wizi wa fedha za
umma katika halmashauri ni matokeo ya kuwepo ombwe la uongozi hususani
katika ngazi ya serikali kuu.
“Hivi tujiulize ni kwa nini Tanzania iliyo
kwenye utajiri inakuwa masikini huku mawaziri wakibainika kuhujumu mali
za umma na kujilimbikizia,” anahoji.
Filikunjombe anasema kilichopo sasa ni
kuwepo viongozi na watumishi wa umma wanaokiuka maadili ya kazi zao na
kuwekeza zaidi katika kufikia maslahi binafsi.
“Kuna viongozi tumewapa dhamana ya kuliongoza taifa, lakini siamini kama wanatekeleza wajibu na majukumu yao ipasavyo,” anasema.
Anasema, kuwa ndani ya CCM katika wadhifa
wowote ukiwemo ubunge, haina maana kuweka kando maslahi ya umma na
kushabikia uozo kwa kigezo cha kulinda itikadi moja.
KUSAINI WARAKA WA ZITTO
Akiwa mbunge wa kwanza kujitokeza
hadharani na kusaini fomu zilizoandaliwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), Zitto Kabwe, Filikunjombe anasema miongoni mwa wabunge wa CCM
wapo waliokuwa na nidhamu ya woga.
Anasema binafsi saini aliyoiweka kwenye
fomu za Zitto haikuwa kwa niaba yake, bali iliwakilisha wananchi wa
Ludewa wanaomtaka asaini fomu hizo.
Hata hivyo anasema baada ya kusaini fomu
za Zitto akifuatiwa na wabunge wengine wakiwemo Alphaxad Lugora
(Mwibara-CCM) na Nimrod Mkono (Musoma Vijijini-CCM), walio wengi
hawakuitikia wito huo.
Anasema sababu iliyodhihirika ni kuwa na
nidhamu iliyovuka mipaka kufikia kiwango cha kuogopa, hata pale maslahi
ya umma yanapoathiriwa.
Lakini Filikunjombe anasema hilo halikuwa
tatizo kwa vile baada ya kupita kwa hoja ya Zitto, Bunge lingepiga kura
ya siri ambapo idadi kubwa ya wabunge wa CCM wangeonyesha hisia zao.
MAWAZIRI WANAOPASWA KUJIUZULU
Filikunjombe anaamini kuwa sakata hilo
halipaswi kuelekezwa katika taswira ya kumnyooshea kidole mtu binafsi,
bali wadhifa kwa kuzingatia maeneo makuu matatu.
“Waziri anaweza kujiona mwenyewe hana
kosa, mamlaka iliyomteua inaweza ikamuona anafaa, lakini sisi
anaotuongoza tukamuona hatufai, kwa hiyo lazima waondoke tu,” anasema.
Lakini Mbunge huyo anaweka wazi kwamba
wanaotajwa kutokana na ripoti iliyowasilishwa bungeni ni watu wa awali,
lakini kwenye orodha kabili wapo wengi wanaostahili kujiuzulu na
kuwajibishwa.
HISIA ZA MAPINDUZI
Filikunjombe anasema kitendo kilichofanywa
na wabunge kutaka baadhi ya mawaziri wa serikali kujiuzulu na
wachukuliwe hatua, hakimaanishi kuwepo mapinduzi, bali harakati za
kuleta mabadiliko yenye maslahi kwa CCM na umma kwa ujumla. Filikunjombe
anasema CCM bado ni chama kizuri kwa maana ya muundo, sera, ilani na
aina ya wanachama wake, lakini kimeunda serikali isiyokuwa na uwezo wa
kufikia matarajio ya umma.
“Tumepata serikali iliyo dhaifu sana kiasi
kwamba tunashindwa kutatua kero za jamii, tatizo halipo kwa chama bali
watendaji serikalini,” anasema.
Anasema kutokana na hali hiyo, ni dhana
potofu kwa wanaozusha hisia hasi kwamba yeye na wabunge walioshiriki
kushinikiza mawaziri wasiokuwa waadilifu wajiuzulu, wana mpango wa
kuhamia upinzani.
“Kwa mfano mimi ndani ya CCM nilipita bila
kupingwa jimboni kwangu, sasa kuna dalili gani za kunifanya nikihame
chama changu,” anahoji.
Hata hivyo harakati za wabunge wa CCM
zilipelekea kuwepo vikao vilivyohitimishwa na Kamati Kuu (CC) ya chama
hicho ambayo ilitangaza kuridhia kushughulikiwa na kutimuliwa kwa
mawaziri na watendaji wahusika.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment