Thursday, May 3, 2012

Kocha wa timu ya Simba, Mserbia Milovan Cirkovic
Joto la mechi ya watani wa jadi, Simba na Yaga, limezidi kuongezeka wakati siku inayosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka kote nchini ikiwa inakaribia.
Simba ambao wanapigania ubingwa wako kambini Zanzibar, wakati Yanga ambao wamevuliwa ubingwa na wamezungukwa na migogoro ya kiutawala, wamejichimbia Bagamoyo mkoani Pwani.
Licha ya mazoezi ya uwanjani, wachezaji wa Simba kwa nyakati tofauti wamekuwa wakipokea semina 'elekezi' kutoka kwa kocha wa timu hiyo Mserbia Milovan Cirkovic, ambayo lengo lake ni kuhakikisha nyota hao wanapokea mbinu za ziada za kuimaliza Yanga katika mchezo wao wa funga dimba wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambao utafanyika keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Pia wachezaji hao asubuhi kila mmoja hufanya mazoezi binafsi ya ufukweni na jioni ndio wote kwa pamoja hushiriki katika programu inayoongozwa na Cirkovic.
Kocha huyo aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Zanzibar jana mchana kuwa mbali na mazoezi ameanzisha 'darasa maalumu' kwa wachezaji wake ili kuwakumbusha mbinu za ziada za kuhakikisha ushindi unapatikana kwenye mechi hiyo na hatimaye kutwaa ubingwa wa ligi.
Cirkovic alisema kuwa anaiamini timu yake lakini ni kawaida kwa makocha kubuni njia tofauti za kuwafundisha wachezaji wake ili waweze kuimarika na kumudu mchezo kama huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani.
"Timu yangu iko vizuri na tunaendelea na programu za mazoezi kama kawaida, kila siku ushindani unaongezeka na ni ishara nzuri kwangu na kwa mashabiki wa Simba," alisema kocha huyo ambaye ameiongoza vyema timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Shirikisho yanayoendelea hapa barani Afrika.
Aliongeza kuwa matokeo ya mechi tatu zilizopita (JKT Ruvu, Moro United na Al Ahly Shandy) yameongeza morari kwa wachezaji wake ambao wameahidi kumaliza ligi kwa ushindi.
Naye daktari wa timu hiyo, Cosmas Kapinga, alisema kuwa wachezaji wote wa timu hiyo wako fiti na wanaendelea na mazoezi kama kawaida tangu walipofika Zanzibar.
"Namshukuru Mungu vijana wako poa na wanaendelea wote na mazoezi, hii ni ishara nzuri hadi kufikia sasa," aliongeza daktari huyo.
Katika kuongeza morari kwa wachezaji, juzi uongozi wa timu hiyo uliwapa wachezaji wake Sh. milioni 35 ikiwa ni motisha ya kuifunga Al Ahly Shandy magoli 3-0 katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya 16-Bora ya Kombe la Shirikisho uliofanyika Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa.
Simba ndio vinara wa Ligi ya Bara kutokana na kujikusanyia pointi 59 na wanahitaji pointi moja ili waweze kutwaa ubingwa wa msimu huu huku Azam iliyokwenye nafasi ya pili itaweza kufikisha pointi 59 endapo itashinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Chamazi.

YANGA WAJIGAMBA
Wachezaji wa Yanga ambao wako Bagamoyo mkoani Pwani wakijinoa wamesema kuwa mechi ya keshokutwa Jumamosi dhidi ya watani wao Simba itakuwa ngumu na yenye ushindani kwa kila aina kutoka pande zote mbili.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wachezaji hao walisema kuwa ukubwa wa mechi hiyo ndiyo unaosababisha upinzani licha ya kwanza wao tayari wameshapoteza nafasi ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa mwakani.
Kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima, aliliambia gazeti hili kuwa wanajiandaa kushinda na hakuna mchezaji ambaye hatarajii kushinda.
Niyonzima aliyejiunga na Yanga akitokea APR ya Rwanda, alisema kuwa mafanikio ndio kitu wanachokitegemea na kamwe hawatashuka uwanjani ili kukamilisha ratiba.
"Kwa kawaida mechi zote huwa tunapambana lakini hii tutakuwa makini zaidi, si tu kwa sababu ni mechi ngumu ila ni mechi kubwa hapa Tanzania," aliongeza kiungo huyo.
Alisema kuwa dhamira za wachezaji wa Yanga ni kuendeleza ushindi dhidi ya wapinzani hao baada ya pia kuwafunga 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza kwa goli la Mzambia Davies Mwape.
Naye beki Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema kuwa atahakikisha anaongoza vyema safu ya ulinzi ili kukwamisha mashambulizi kutoka kwa wapinzani wao.
Cannavaro alisema kuwa hana hofu na mchezo huo utakaoamua bingwa wa ligi na kuwataka wanachama na mashabiki wa timu yao kujitokeza kuwashangilia.
Alisema pia kufanya vizuri kwa kikosi chao kitasaidia kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame wanaoushikilia ambapo mashindano hayo yataanza Juni 23 hapa jijini Dar es Salaam.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment