Friday, May 4, 2012


Rais Jakaya KIkwete
JOTO la mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri yanayotarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa limezidi kupanda kutokana na Rais Rais Jakaya Kikwete kuwateua kuwa wabunge watu watatu, akiwamo Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.

Wengine walioteuliwa ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sospeter Muhongo na kada wa CCM, Janet Mbene. Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana jioni ilisema Rais Kikwete amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya Ibara ya 66(i) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Taarifa hiyo ilisema uteuzi huo unaanza mara moja.

Uteuzi huo unaongeza joto la kisiasa kwani unahusishwa na mchakato unaoendelea wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na jana baada ya wabunge hao kutangazwa kulikuwa na mjadala mkali katika mitandao ya kijamii kuhusu uwezekano wa baadhi ya wabunge wateule kuwa mawaziri.

Ibara ya 68 ya Katiba ya nchi inasema “Kila mbunge atatakiwa kuapishwa katika Bunge kiapo cha uaminifu kabla hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge”.

Pia Ibara ya 56 ya Katiba hiyo pia inasema: “Waziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge”.

Ibara ya 57 (i) inasema muda wa kushika madaraka ya waziri na naibu waziri utaanza tarehe atakapoteuliwa kushika madaraka hayo.

Kwa kuzingatia vipengele hivyo vya Katiba, mwanasheria aliyebobea katika masuala ya Katiba (jina tunalihifadhi kwa sasa) aliliambia Mwananchi kuwa mbunge wa kuteuliwa  anaweza kuteuliwa kuwa waziri bila kuapishwa kuwa mbunge.

Mwanasheria huyo alisema mamlaka ya Rais kuteua mtu kuwa mbunge kisha kumteua kuwa waziri hayaingiliani na itikadi za vyama kwani Ibara ya 55 (4) imeweka bayana kwamba,waziri atateuliwa kutoka miongoni mwa wabunge bila kutaja vyama.

Kuhusu uwezekano wa mpinzani kuwa waziri katika serikali ya chama tawala, alifafanua, "Hilo linawezekana kabisa. Ingawa sasa, sijui atafanyaje kazi maana atakuwa katika wakati mgumu. Maana hata hawezi kuingia katika vikao vya ndani vya wabunge na mawaziri wa chama tawala." 

Kiu ya wananchi

Baadhi ya wananchi walipiga simu katika chumba chetu cha habari wakisikika kuwa na shauku ya kufahamu iwapo uteuzi huo ulikuwa sehemu ya mchakato wa kutangazwa kwa Baraza la Mawaziri.

Miongoni mwa waliopiga simu kufuatilia suala hilo wamo wabunge, wanasiasa wa vyama mbalimbali, wanazuoni, wasomi na wananchi wa kawaida.

“Samahani…..nimesikia kwamba eti JK ameteua wabunge ni kweli? Ni akina nani hao? “alihoji mmoja wa waliopiga simu katika chumba chetu cha habari na baada ya kujibiwa alitaka ufahamu iwapo wabunge hao wanaweza kuwa mawaziri.

Novemba 2010 baada ya Rais Kikwete kutangazwa mshindi wa urais kwa awamu ya pili, aliteua wabunge watatu ambao ni Shamsi Vuai Nahodha, Profesa Makame Mbarawa na Zakia Meghji.

Baadaye katika Baraza lake la Mawaziri, Mbarawa aliteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Nahodha aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mbatia ni kiongozi wa tatu kutoka NCCR Mageuzi kupewa nafasi ya uongozi katika muda uziozidi mwezi mmoja na ni mwenyekiti wa kwanza wa chama cha siasa cha upinzani kuteuliwa kuwa mbunge tangu kuanza kwa siasa za vyama vingi nchini, 1992.

Aprili 6 mwaka huu, Rais Kikwete alitangaza kumteua Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa chama hicho, Dk. Sengondo Mvungi kuwa miongoni mwa wajumbe 30 wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Aprili 18 mwaka huu, Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje ya chama hicho, Nderakindo Kessy alichaguliwa kuwa mbunge wa Afrika Mashariki.

Wasifu wao
Mbatia mbali na kuwa Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, kitaaluma ni mhandisi na aliwahi kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1987 hadi 1992 alipofukuzwa kutokana na migomo iliyotikisa chuo hicho .

Baadaye mwaka 2007 hadi 2009 alikwenda nchini Uholanzi kusomea International Civil Engineering akibobea zaidi katika eneo la kukabilianana majanga (Risk management).

Mbatia pia amewahi kuwa mbunge wa Vunjo na amekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi tangu Machi 6, 2000 na uongozi wake unatarajiwa kukoma mwaka 2013.

Naye Janet Mbene ana Shahada ya Uzamili ya Uchumi kutoka Chuo cha New England Australia. Ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Kampuni binafsi ya SIA, ambayo inajenga uwezo kibiashara kwa kampuni ndogo na za kati.

Amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo Umoja wa Mataifa (UN), Shirika la kimataifa la Oxfam, Programu ya Maendeleo ya UN, Shirika la Kazi la Kimataifa na mashirika ya kimataifa yasiyokuwa ya kiserikali.

Pia ni mwanzilishi na mwenyekiti wa Shirika la Yatima Trust linaloshughulika na masuala ya wagonjwa Ukimwi na kutoa msaada kwa watoto yatima.

Kwa upande wake, Muhongo ni Profesa wa Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia ni Profesa wa heshima ya Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini.Ni mwanazuoni wa Heshima katika jumuiya kadhaa za kimataifa na kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Tume ya Ramani na Jiolojia Duniani (CGMW) na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) inayoshughulikia utoaji wa Tuzo za Kisayansi za Kwame Nkrumah kwa ajili ya wanasayansi bora iliyoundwa mwaka 2011.
Profesa Muhongo pia ni Mhariri Mkuu wa Jarida la Afrika Dunia Sayansi (Elsevier), Msaidizi wa Mhariri wa Precambrian Utafiti (Elsevier) na mwanachama wa bodi kadhaa za wahariri wa majarida ya kisayansi.
Alikuwa Rais wa Chama cha Geological ya Afrika (1995 - 2001) na Mkurugenzi mwanzilishi wa Kanda (2005 - 2010) wa Ofisi ya ICSU ya Mkoa kwa ajili ya Afrika, Pretoria, Afrika Kusini.
Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya masuala ya kisayansi wa UNESCO mwaka 2004 - 2008, na Mwenyekiti wa Programu ya Sayansi ya Kamati (SPC) ya Mwaka UN-kutangazwa Kimataifa wa Sayari ya Dunia ( IYPE) 2007 - 2010.
Kazi zingine alizowahi kufanya ni pamoja na kuwa Mwenyekiti  wa Bodi ya Wakurugenzi wa State Mining Corporation (STAMICO) na Mkuu wa Idara ya Jiolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1997-2000).
Prof Muhongo alikuwa Mwenyekiti wa wa Tume ya Serikali ya Tanzania ya Uchunguzi wa ajali ya wachimbaji madini ya Tanzanite Mererani iliyotokea mwaka 2002.

Mawaziri wapigwa 'stop'
Katika hatua nyingine mawaziri wote wamezuiwa kusafiri kikazi nje ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na kile ambacho kinaelezwa kuwa ni maandalizi ya kukabidhi ofisi kwa mawaziri wapya ambao wanatarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa.

Taarifa hizo zimekuja siku moja tu tangu Ikulu kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kusema kuwa “Watanzania wasubiri Baraza bora la Mawaziri”.

Jana, taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari serikalini vililidokeza gazeti hili kuwa mawaziri wote sasa wamezuiwa kusafiri nje ya Dar es Salaam kutokana na kusubiri mchakato huo wa kukabidhiana ofisi.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, karibu mawaziri wote na naibu mawaziri walikuwepo jijini Dar es Salaam jana isipokuwa wachache ambao haikuthibitika mara moja kama walikuwapo au la.

Vyanzo hivyo viliongeza kwamba tayari Rais amekwishamaliza mchakato wa uteuzi na baraza jipya linatarajiwa kukutana na mkuu huyo wa nchi katika semina elekezi Jumanne ya Mei 8, mwaka huu.

Kwa wiki mbili mfulululizo sasa nchi imegubikwa na mjadala kwa watu wa kada tofauti kushinikiza kufanyika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri baada ya Bunge kutaka mawaziri wanane waliotajwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh wawajibike au wawajibishwe.

Mawaziri wanaotakiwa kuwajibishwa baada ya kushindwa kuwajibika ni Mustafa Mkulo (Fedha), Omary Nundu (Uchukuzi), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Profesa Jumanne Maghembe (Kilimo, Chakula na Ushirika), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), George Mkuchika (Tamisemi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), William Ngeleja (Nishati na Madini).

Baraza Jipya

Katika kuonyesha Rais amekuwa katika mchakato wa mwisho wa uteuzi huo akisubiri kuutangazia umma, alishindwa kutokea katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani jana ambako alipaswa kuwa mgeni rasmi.

Badala yake, Rais alimtuma Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi kwa ajili ya kumwakilisha katika maadhimisho hayo ambako pia angezindua Mwongozo na Kanuni za Uongozi kwa Wamiliki na Mameneja wa vyombo vya habari Afrika. 

Katika hotuba ya uzinduzi, Dk Nchimbi alikiri kuwa Rais Kikwete amebanwa na kazi ya kupanga upya safu ya baraza lake la mawaziri akisema amemtuma yeye ili amwakilishe.
Akitumia lugha ya kimichezo, Dk Nchimbi alisema; “Nimefurahi kwa kunialika kwenye tukio hili tukufu wakati huu ambao Rais amebanwa katika kupanga wachezaji wake 11 wa kikosi cha kwanza.”

Dk Nchimbi ambaye alisoma hotuba hiyo kwa lugha ya Kiingereza alitumia usemi ambao ni maarufu katika soka kwamba Rais alikuwa akipanga “First eleven.”

Kwenye soka mwalimu hupanga “first eleven” kuwa ni kikosi chake cha wachezaji anaowategemea kwa ajili ya ushindi hasa anapopambana na timu ngumu.

Lugha hiyo ya kimichezo aliitumia Dk Nchimbi kuonyesha uzito ambao Rais Kikwete ameuweka katika kupanga upya safu ya mawaziri wake katika kipindi hiki ambacho Taifa linakabiliwa na matatizo mbalimbali kubwa likiwa ni wizi wa fedha za umma.

Hata hivyo, kwenye uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Reginald Mengi alisema kuwa anaamini kuwa Dk Nchimbi atakuwa miongoni mwa mawaziri wa baraza jipya la Rais Kikwete.

Dk Nchimbi aliielezea kauli hiyo ya Mengi kuwa imempa faraja na nguvu mpya za kiutendaji za kurudi kwenye timu hiyo ya kuongoza Serikali.

Hata hivyo, alisema pamoja na kumtia moyo huko bado ni jambo lisilotabirika wakati huu ambao haijulikani siku wala saa ambayo Rais Kikwete atalitangaza hadharani.

Habari hii imeandaliwa Leone Bahati, Boniface Meena na Patrica Kimelemeta

0 comments:

Post a Comment