Gazeti la kila wiki la Dira ya Mtanzania toleo la leo,
Jumatatu, Mei 7, mwaka huu, 2012, limechapisha habari yenye kichwa cha
habari, “Familia ya JK yachafuliwa”.
Katika habari hiyo, Gazeti hili linadai kuwa familia ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
inafanya biashara na kampuni ya Home Shopping Centre (HSC) ya Dar es
Salaam.
Aidha, Gazeti hili linadai kuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo,
Bwana Said Saad ndiye msimamizi wa biashara za familia hiyo ya
Mheshimiwa Rais.
Tunapenda kuujulisha umma habari hizo si za kweli. Ni uongo
unaolenga kuupotosha umma na kuchafua jina la Mheshimiwa Rais Kikwete na
familia yake. Na, au vinginevyo unalenga kuchafua jina la Kampuni ya
Home Shopping Centre. Kama nia ni kufanya hivyo tafadhali msilitumie
jina la familia ya Rais.
Mheshimiwa Rais Kikwete haendeshi, hajawahi kuendesha, na
wala hana mpango wa kuendesha biashara iwe ni yeye binafsi au na familia
yake. Shughuli azipendazo na ambazo anajishughulisha nazo ni kilimo na
ufugaji. Kwa ajili hiyo ana mashamba Sanzale, Kiwanga na Msoga. Hata
shughuli hizo hazijafikia kiwango cha kibiashara kwani hutumia pesa yake
ya mfukoni kugharamia shughuli hizo.
Badala ya kutoa tuhuma za jumla jumla zisizokuwa na ushahidi
wowote ni vema muwe wawazi. Ni vema gazeti likaeleza namna gani au
likamtaja ni nani ndani ya familia ya Mhe. Rais Kikwete anaendesha
biashara kwa kushirikiana na Kampuni ya Home Shopping Centre.
Kwa kufanya hivyo , Gazeti la Dira ya Mtanzania
litawathibitishia Watanzania kuhusu ukweli wa habari hizo. Aidha,
litaondoa doa baya na chafu linalotaka kuelekezwa kwa Rais na Familia
yake. Kitendo hicho hakimtendei haki Rais na Familia yake.
Ni imani yetu kuwa Gazeti hili litatoa majibu ya
masuala haya muhimu katika toleo lake lijalo, vinginevyo Familia ya
Mheshimiwa Rais itakuwa na haki ya kuchukua hatua stahiki za kisheria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
7 Mei, 2012
0 comments:
Post a Comment