Release No. 069
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 8, 2012
TWIGA STARS KUJIPIMA KWA ZIMBABWE
Timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) itacheza na Zimbabwe katika
mchezo wa kirafiki utakaofanyika Mei 12 mwaka huu kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Twiga Stars hivi iko katika ziara ya mechi za kirafiki katika mikoa
ya Dodoma na Mwanza. Leo (Mei 8 mwaka huu) itacheza na kombaini ya Mkoa
wa Dodoma ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 katika mchezo
utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma.
Kesho (Mei 9 mwaka huu) itaondoka kwenda jijini Mwanza ambapo pia
itacheza mechi moja ya kirafiki Mei 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba, na kurejea Dar es Salaam tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya
Zimbabwe.
Zimbabwe inatarajia kuwasili kesho (Mei 9 mwaka huu) jioni kwa ndege
ya South African Airways (SAA) ikiwa na msafara wa 25 na wataondoka Mei
14 mwaka huu alfajiri.
Watazamaji 41,733 walikata tiketi kushuhudia mechi ya Ligi Kuu ya
Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga
iliyochezwa jana (Mei 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
KAMATI YA MASHINDANO KUPANGA VITUO LIGI YA TAIFA
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
inatarajia kukutana leo (Mei 8 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine
itapanga vituo vya Ligi ya Taifa na tarehe ya kuanza ligi hiyo.
Mikoa nane imeomba kuwa wenyeji wa ligi hiyo itakayochezwa katika
vituo vitatu. Mikoa hiyo kupitia kwenye vyama vyao vya mpira wa miguu
ni
Mikoa iliyoomba vituo ni Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mbeya, Shinyanga na Singida.
Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni mabingwa wa mikoa. Timu hizo ni
Ashanti United ya Ilala (Dar es Salaam), Aston Villa (Singida), Bandari
FC (Kagera), CDA (Dodoma), Flamingo SC (Arusha), Forest FC ya Siha
(Kilimanjaro), JKT Kanembwa (Kigoma), Korogwe United ya Korogwe (Tanga),
Kurugenzi ya Mafinga (Iringa), Lindi SC (Lindi) na Majimaji (Tabora).
Mighty Elephant (Ruvuma), Mkamba Rangers ya Kilombero (Morogoro),
Mpanda Stars ya Mpanda (Rukwa), Mwadui FC (Shinyanga), Nangwa VTC
(Manyara), Ndanda FC (Mtwara), Pamba SC (Mwanza), Polisi Mara (Mara),
Red Coast ya Kinondoni (Dar es Salaam), Super Star ya Bagamoyo (Pwani),
Tenende SC (Mbeya) na Tessema FC ya Temeke (Dar es Salaam).
KILA LA KHERI SIMBA, PONGEZI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri
timu ya Simba kwenye mechi yake ya marudiano ya Kombe la Shirikisho
dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan itakayochezwa Jumapili (Mei 13 mwaka
huu).
Mechi hiyo itachezwa katika mji wa Shandy kuanzia saa 2 kamili usiku
kwa saa za Afrika Mashariki. Simba inaondoka kesho kwenda huko kwa ndege
ya Kenya Airways.
Msafara wa timu hiyo utaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
TFF, Hussein Mwamba, na unatarajia kurejea nyumbani Mei 15 mwaka huu.
Pia TFF inaipongeza Simba kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu
ya Vodacom (VPL) ambayo Mei 6 mwaka huu ilifunga msimu wa 2011/2012.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment