CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo kitafanya
mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es
Salaam ambapo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbord
Slaa watahutubia.
Aidha, viongozi wengine wakiwemo wabunge wake 15 ni miongoni mwa
watakaoshiriki mkutano huo, akiwemo Mbunge wa Ubungo John Mnyika ambaye
juzi, alitangazwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa mbunge
halali baada ya kushinda kesi ya kupinga ushindi wake, iliyokuwa
ikimkabili.
Joto la mkutano huo limepanda kiasi kwamba, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limetangaza kuweka ulinzi mkali.
Taarifa ya CHADEMA jana imesema kuwa, ingawa Mahakama Kuu imewapatia
ushindi wabunge wake, Tundu Lissu, John Mnyika, Gervas Mbasa na wengine
waliopingwa, leo katika mkutano huo itaeleza umuhimu wa mabadiliko ya
kimfumo katika mhimili huo, na katika utendaji kazi wa Tume ya Uchaguzi
(NEC), ambayo chama hicho kinataka iwe chombo huru katika kutekeleza
majukumu yake nyeti mbalimbali, ikiwemo kusimamia uchaguzi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
CHADEMA, John Mnyika, alidai kunahitajika mabadiliko ya kimfumo kwa
sababu kumekuwa na athari kubwa katika maendeleo ya wananchi, na pia
kikwazo cha kuweka madaraka ya uendeshaji wa nchi mikononi mwa umma kama
inavyotamkwa katika ibara ya 8 ya katiba ya sasa.
“Tunataka wananchi wajitokeze kwa wingi kusikiliza masuala mbalimbali,
zikiwemo hoja juu ya umuhimu wa kufanya mabadiliko ya kimfumo kupitia
uandikwaji wa katiba mpya, waje wajue namna ambavyo ubovu wa katiba ya
sasa umechangia kwa kiasi kikubwa matatizo makubwa yanayotukabili kama
taifa, ikiwemo umaskini, ujinga, maradhi, ufisadi na CCM yenyewe,”
alisema Mnyika.
Alidai kuwa katika mkutano huo, watazindua kampeni ya ‘kuiamsha Dar es
Salaam’, ikiwemo kaulimbiu ya ‘Vua Gamba, Vaa Gwanda’ inayotarajiwa
kuwapokea viongozi na wanachama wengi kutoka CCM.
Aliongeza kuwa, tofauti na CCM ambayo imeanza mchakato wa katiba kwa
kujifungia na kutoa misimamo ya mamlaka za chama bila hata maoni ya
wanachama wake nchi nzima, CHADEMA itatumia fursa hiyo kutoa elimu ya
uraia kwa umma juu ya sheria ya mabadiliko ya katiba, ili kuwezesha umma
kumiliki mchakato na hivyo taifa lipate katiba bora.
Mbali na Mnyika, wabunge wengine watakaoonekana leo ni pamoja na Peter
Msigwa, Ezekiah Wenje, Tundu Lissu, Grace Kiwelu, Halima Mdee, Rose
Kamili, Mhonga Said, Suzan Kiwanga, Joyce Mkya, Godbless Lema na Meya wa
Manispaa ya Musoma, Alex Malima Kasurula.
MVUTANO POLISI, CHADEMA
Hata hivyo, pamoja na Jeshi la Polisi kuruhusu kufanyika kwa mkutano
huo, kumezuka mvutano kati ya pande hizo mbili kuhusu suala la wanachama
kufanya matembezi ya hiyari kutoka kila kona ya Jiji la Dar es Salaam
kuelekea Jangwani.
Wakati CHADEMA wakitangaza ramani yatakapopita matembezi hayo, polisi
imeyapiga marufuku kwa madai kwamba hakuna sheria yoyote inayoruhusu
chama cha siasa kufanya matembezi au maandamano.
Awali, CHADEMA ilituma maombi ya maandishi kwa Jeshi la Polisi
kuruhusu matembezi hayo ya amani, kutoka sehemu mbalimbali za jiji hadi
viwanja vya Jangwani panapofanyika mkutano wa hadhara leo.
Lakini jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova alisema, wanaruhusu kufanyika kwa mkutano huo, na wamejiandaa
kikamilifu katika ulinzi, lakini si kwa matembezi.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, CHADEMA iliwasilisha barua ya kuomba
kibali cha kufanya mkutano, lakini kabla ya kujibiwa, kilipeleka barua
nyingine yenye lengo la kupewa kibali cha matembezi ya amani.
Kova alidai kuwa, mwanachama yeyote atakayekaidi amri hiyo,
atachukuliwa hatua za kisheria, na kuonya kuwa watu wasidanganyike
kufanya matembezi hayo, ila kila mtu anayo haki ya kwenda katika mkutano
kwa namna ya kawaida.
Hata hivyo, CHADEMA imepinga na kudai kuwa hayo si maandamano, bali
matembezi maalum kutoka kwenye maeneo ya jiji kwenda viwanja vya
Jangwani, ikizingatiwa kuwa hali ni ngumu na si kila mtu mwenye uwezo wa
kumudu gharama za usafiri.
Chama hicho kimedai kuwa, Watanzania wanayo haki kikatiba kufanya
maandamano na mikusanyiko ili mradi hawavunji sheria, na kimetangaza
barabara zitakazotumiwa na watu wa majimbo ya Ilala, Ukonga na Segerea,
kuwa ni Buguruni, Uhuru, Msimbazi, Morogoro hadi Jangwani.
Watakaotoka majimbo ya Kinondoni, Kawe na Ubungo, watakutanika katika
bustani ya Magomeni, kupitia barabara ya Morogoro hadi Jangwani, wakati
wale wa Kigamboni, wataanzia Kivukoni, kupitia Posta ya zamani, Makao
Makuu ya Jiji, barabara ya Morogoro hadi Jangwani.
Wale wa Temeke, wataanzia Mwembeyanga, kupitia barabara ya Mandela,
Buguruni na kukutana na wale wa majimbo ya Ilala na kuelekea Jangwani.
CHANZO CHA HABARI GAZETI LA MTANZANIA LA LEO
|
0 comments:
Post a Comment