WATU sita wamefariki dunia na wengine wawili wamejeruhiwa vibaya
baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kuanguka na
kusababisha watu wengine wawili kujeruhiwa vibaya katika eneo la Sigino
wilayani Babati mkoani Manyara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa amesema ajali hiyo
imetokea jana saa 2 asubuhi wakati gari la mizigo lililokuwa na tela
lenye namba za usajili T 536 AGH na tela lenye namba za usajili T 575
BHJ mali ya Josephat Mkalama wa mjini Babati, likitokea Iringa kuja
mkoani hapa, lilipoacha njia na kuanguka baada ya breki zake kushindwa
kufanya kazi.
Kamanda Mpwapwa amewataja waliokufa kuwa ni pamoja na dereva wa gari
hilo, Paulo Charles (38) mkazi wa Mafinga mkoani Iringa, utingo, mama
mmoja aliyetajwa kwa jina la Juliana Joseph (35) mkazi wa Sinai wilayani
Babati pamoja na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili, ambao walikuwa
wakitokea Singida. Marehemu wengine wanne majina yao hayakuweza
kufahamika mara moja.
Kamanda Mpwapwa amewataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Anjelina
Basiri (65) mkazi wa Sigino, Babati na kijana mmoja aliyejulikana kwa
jina la Lazaro (15) mkazi wa Dongobesh wilayani Mbulu, ambao walikuwa
kando ya barabara nje ya nyumba wanayoishi walipofuatwa na kukumbwa na
ajali.
Majeruhi hao wamekimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Babati (Mrara)
ambako wanapatiwa matibabu, huku hali zao zikiwa ni mbaya, na kwamba
Anjelina anapumua kwa msaada wa mashine maalumu, na kijana Lazaro akiwa
ameumia vibaya mguu wake wa kushoto akiwa hajitambui. Miili ya marehemu
imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya.
Ajali hiyo imetokea wakati juzi mkoani Mwanza, watu watano walikufa
hapo hapo na wengine watano kujeruhiwa vibaya baada ya gari la mizigo
walilokuwa wakisafiria kutoka mkoani Shinyanga kwenda Mwanza kupinduka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow aliwataja waliokufa
katika ajali hiyo kuwa ni Hawa Charles (30), Ngereja Nzeso (25), Tabu
Mwage (22) ambao ni wakazi wa Malampaka mkoani Shinyanga na wengine
wawili hawakutambuliwa.
WALIOKUFA AJALI YA MBUNGE WAFIKIA WANNE
Katika tukio jingine, idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali
ya gari iliyomhusisha Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA)
imeongezeka na kufika watu wanne baada ya mmoja kufariki wakati
akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma alisema hadi
sasa waliotajwa kufa ni pamoja na mama mzazi wa mbunge huyo, Catherine
Roman Selasini (80), mama mkwe wake, Agatha Jerome Mahoo (85) na
wanawake wawili, mmoja ikidaiwa ni shangazi yake ambao majina yao
hayajajulikana.
Majeruhi kwenye ajali hiyo ni pamoja na mke wa Selasini, Digna Kavishe
(43) ambaye amepata majeraha sehemu za kichwa na hali yake si nzuri,
pamoja na mbunge huyo ambaye amepata majeraha kwenye bega pamoja na
mkono wa kulia.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 1.00 jioni katika barabara kuu ya Moshi,
Arusha eneo la Chuo cha Ufundi Bomang’ombe wilayani Hai, baada ya gari
lenye namba za usaji T 441 BRT aina ya Toyota Land Cruiser lilikuwa
likiendeshwa na Selasini kupinduka.
chanzo cha habari: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36313
0 comments:
Post a Comment