Saturday, May 26, 2012

Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, amepata ajali baada ya gari alilokuwa akiendesha kupinduka na kumuacha akiwa majeruhi na kulazwa kwa muda katika hospitali ya wilaya ya Hai kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi.

Katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Bomang’ombe karibu na chuo cha Ufundi wilayani Hai, watu watatu, akiwamo mama yake mzazi, Gloria Shayo, walifariki dunia na wengine kujeruhiwa.

Gari hilo aina VX Toyota Land Cruiser, ambalo ni mali ya mbunge huyo, lilikuwa limepakia watu sita, akiwamo mama yake mzazi, Gloria, wakitokea Arusha kwenye msiba wa shemeji yake, Padri Fransido Malo, kwenda Moshi.

Wengine waliokuwamo kwenye gari hilo, ni mama mkwe wake, Agatha Jerome (85) na mkewe Diana Kavishe.

Watu wengine wawili waliokuwa kwenye gari hilo ambao majina yao hayajapatikana, wamefariki dunia, huku mbunge huyo akiumia mkono wa kulia na paja.

Habari zilizothibitishwa na kaka wa mbunge huyo, Francis Selasini, zinaeleza kuwa ajali hiyo ilitokea katika eneo la Chuo cha Ufundi Boma Ng’ombe, jana majira ya saa 12.45 jioni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma, alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na ajali hiyo, alisema bado hajapata taarifa kamili.

Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, vifo na majeruhi na kusema kuwa alikuwa njiani kwenda eneo la ajali.

Akizungumza katika Hospitali ya Hai ambako alikimbizwa baada ya ajali hiyo, Selasini alisema alikuwa akiendesha gari hilo kwa mwendo kasi akiwahi kuingia Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako baba yake mzazi amelazwa.

Kwa mujibu wa habari hizo, watu wawili walifariki dunia katika eneo la ajali na mmoja alifariki katika Hospitali ya Wilaya wakati akipatiwa matibabu.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Mawenzi.

Habari hizo zinasema kuwa ajali hiyo ilitokewa wakati Selasini alipokuwa anataka kumkwepa mwendesha baiskeli, akashindwa kulimudu gari, ambalo lilitoka nje ya barabara na kutumbukia kwenye mtaro.

Hii ni ajali ya pili kwa mbunge huyo baada ya kuumia tena wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka juzi katika jimbo lake kufuatia ajali iliyosababisha mkono wake uvunjike.


  CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment