Thursday, May 17, 2012



VUGUVUGU la mabadiliko (Movement for change) na oparesheni ‘Vua gamba, vaa gwanda’ jana vimeingia katika Kijiji cha Endulen, wilayani Ngorongoro baada ya mwenyekiti wa kijiji hicho, Pettei Kitaika kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema), akiwa na kundi la wanachama 415.

Mwenyekiti huyo aliyeshinda kiti hicho kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na mabalozi 10 na wenyeviti wawili wa vitongoji walijiunga Chadema baada ya kujiengua kutoka CCM.

Kijiji cha Endulen ndiko anakotoka Mbunge wa  Ngorongoro, Saning’o Ole Telele (CCM).

Baada ya kupokewa na Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Mchungaji Amani Golugwa na kukabidhiwa kadi ya Chadema. Kitaika aliahidi kuibomoa CCM katika kijiji hicho na kuhakikisha Serikali yote ya kijiji inahamia upinzani.

“Naendelea na majadiliano na baadhi ya wenyeviti wa vitongoji na mabalozi wa nyumba kumi ambao wengi wameonyesha kuchoshwa na vitendo vinavyoendelea ndani ya CCM ili wote wahamie Chadema siku ambayo viongozi wa mkoa watafika kufanya mkutano wa hadhara Endulen,” alisema Kitaika.

Akizungumzia wanachama hao wapya, Mchungaji Golugwa alisema kuwa kuhamia Chadema kwa wanachama hao wa CCM ni mwendelezo wa  harakati oparesheni za kuhimiza mabadiliko katika mfumo wa uongozi kisiasa, kiuchumi na kijamii ulioanza kuenea nchi nzima baada ya kuzinduliwa mkoani Arusha mwezi Machi, mwaka huu.

Alisema katika mfululizo wa mikutano ya oparesheni vua gamba, vaa gwanda unaoendelea sehemu mbalimbali nchini, Chadema itawapokea na kuwafundisha viongozi na wanaCCM wote watakaoonyesha kujitambua na kujutia ushiriki wao kwenye matendo ya kuhujumu uchumi, masilahi na rasilimali za taifa.

Alisema mipango iko njiani kupeleka mikutano ya vuguvugu la mabadiliko katika wilaya zote za Mkoa wa Arusha katika ziara zitakazoongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema pamoja na James Ole Millya aliyejiengua CCM na kujiunga na Chadema hivi karibuni.

0 comments:

Post a Comment