Tuesday, September 10, 2013

  Waendeleza ahadi mpya mikoani

na Mwandishi wetu, Mwanza

ZIARA ya Rais Jakaya Kikwete mkoani Mwanza imewaacha vinywa wazi wananchi baada ya mawaziri wake kuendelea kutoa ahadi mpya wakati zile zilizoahidiwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita zikiwa bado hazijatekelezwa.
Hofu hiyo inakuja wakati ambapo Rais Kikwete amebakiza miaka miwili kumaliza muhula wake wa pili, huku ahadi zake nyingi zikiwa bado zinahojiwa sehemu mbalimbali nchini.
Wakizungumza na gazeti hili jijini hapa juzi baada ya Rais Kikwete kuhutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Furahisha, baadhi ya wananchi walieleza kushangazwa na hatua ya mawaziri hao walioambata na rais kutoa ahadi mpya.
Walisema kuwa Rais Kikwete wakati wa Uchaguzi Mkuu alitoa ahadi nyingi mkoani humo na kwamba katika ziara hiyo walitarajia kuona wasaidizi wake wakieleza ni kiasi gani zimetekelezwa na zitamalizika lini.
“Yaani haya ni maajabu, maana kama unafuatilia Bunge, hata wabunge wetu kila wakati wanahoji juu ya utekelezaji wa ahadi hizo lukuki za Rais Kikwete, halafu leo kama si uongo ni nini, kuona tunaongezewa ahadi nyingine?” walihoji.
Mawaziri waliopata fursa ya kuzungumza mkutanoni hapo ni pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Charles Kitwanga, ambaye aliwahakikishia wananchi kuwa Ziwa Victoria litakuwa safi ili wavuvi wavue samaki na kufanya biashara.
“Tutahakikisha Ziwa Victoria lipo safi ili muweze kufanya biashara ya uvuvi,” alisema Kitwanga na kuibua shaka kwa wananchi hao.
Akizungumzia ahadi hiyo, mkazi wa Nyamalango, Vincent Aloyce, alilalamika kuwa biashara ya uvuvi siku hizi inafanywa na wawekezaji wakubwa.
Alisema kuwa wananchi wa hali ya chini huambulia mapanki, hivyo kuona ahadi hiyo kama kejeli kwao.
Kwamba, mwaka 2010, Rais Kikwete aliahidi kuwakopesha wavuvi zana za kuvua na kilimo ili waweze kujiendeleza.
Kauli ya pili iliyowashangaza wananchi hao ni ile ya Naibu Waziri wa Elimu (Tamisemi), Kasimu Majaliwa, ambaye katika mkutano huo hakuweza kuzungumzia matatizo ya elimu mkoni Mwanza, badala yake aliwaomba wananchi kila mmoja asali kwa imani yake kuwaombea wanafunzi wa darasa la saba wanaofanya mitihani yao kesho.
Akizungumzia kauli hiyo, Mwalimu Innocencia Paul, wa shule moja jijini hapa, alisema waziri huyo amewakejeli walimu kwa kutogusia ni lini serikali italipa madai yao kama ilivyokuwa imeahidi.
Alisema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha migomo, hivyo kuchangia matokeo mabaya.
“Hapa Mwanza shule nyingi wanafunzi wanakaa chini halafu eti waziri anakuja hapa na kutuambia tuwaombee miujiza ya Mungu wafaulu mitihani bila serikali kutatua matatizo yao.
Alikumbushia ahadi ya Rais Kikwete mwaka 2010 ya serikali kusambaza walimu 16,000 katika shule za sekondari zenye upungufu mkubwa wa walimu, ailiyoitoa akiwa Kisesa wilayani Magu.
Katika mtiririko huo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, aliahidi kupanua Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ahadi ambayo hata rais pia aliizungumzia, kuwa inafaa kutekelezwa, ili ndege kubwa kama ile ya Rais Barack Obama wa Marekani iweze kutua.
“Uwanja upanuliwe lili dege kubwa kama la Obama litue Mwanza,” alisema rais akikazia ahadi ya Tizeba.
Tizeba aliongeza kuwa serikali itahakikisha kuwa kuna treni saba za kuanza safari za Dar es Salaam hadi Mwanza ili usafiri wa reli uwepo siku zote za wiki.
“Usafiri wa Mwanza hadi Dar es Salaam utakuwapo kwa njia ya reli kila siku, ingawa kwa sasa upo kila Ijumaa na Jumanne, tunakarabati vichwa vinane katika karakana ya Morogoro, tutanunua vichwa 13 vya treni na tunatarajia kuwa na mabehewa 990.
“Tuna fedha za ziada sh bilioni 56 kukamilisha kazi hiyo kufikia mwishoni mwa mwaka 2015,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali ipo katika mazungumzo na Kampuni ya Samsung ya Korea ili iweze kujenga meli kubwa tatu katika maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyika kabla ya mwaka 2015.
Mwalimu Frederick Kitaka wa Kitangiri, alisema kuwa ahadi hiyo imerudiwa kwa mara nyingine, wakati ilitolewa na rais mwaka 2010 bila kutekelezeka hadi leo.
“Meli zote zinazotumika kwenye maziwa hayo matatu ni chakavu na zinaweza kuua maelfu ya watu wakati wowote, sasa kwa naibu waziri kuja hapa na kuendeleza ahadi haitusaidii, tunataka utekelezaji,” alisema.
Ahadi iliyokuwa gumzo ni ile ya Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, kwamba wananchi wote wa Ilemela na Nyamagana hadi kufikia Krismasi watakuwa wana uhakika wa maji kwa asilimia 100.
Kwa mujibu wa waziri huyo, kiwango cha kuzoa maji taka kitaongezeka kutoka asilimia tano ya sasa hadi asilimia 35.
“Tutapanua huduma ya maji kwa watu wote hata wanaokaa vilimani, maeneo ya Kayenze, Kahama, Nyamazobe na maeneo mbalimbali ya Nyamagana, wananchi wanatapa maji asilimia mia moja,” alisema Mwaka 2010, Rais Kikwete aliahidi kuwa vijiji vyote vilivyoko kilomita 15 kutoka kwenye bomba kuu la mradi mkuu wa maji wa Ziwa Victoria -Shinyanga-Kahama vitaunganishiwa maji.
Ahadi hiyo ya upatikanaji wa maji ilionekana kuwavuruga wananchi wengi, kwani hata jana akiwa wilayani Kwimba, wabunge wa Sumve na Kwimba kupitia CCM waliitaka serikali kutekeleza ahadi hiyo kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka kesho.
Hali hiyo ilijitokeza wakati rais akisomewa taarifa ya maendeleo na Mkuu wa Wilaya hiyo, Seleman Mzee, ambayo ilieleza kuwa baadhi ya matatizo makubwa yanayowasumbua wananchi wa Kwimba ni ukame pamoja na uhaba wa maji safi na salama ya kunywa.
Jinamizi kama hilo, liliwahi kumkumba pia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipofanya ziara ya kikazi mkoani Mwanza miezi kadhaa iliyopita.
Pinda wakati huo aliagiza tatizo hilo limalizwe ndani ya muda mfupi, vinginevyo mkurugenzi na mkuu wa wilaya hiyo atawajibika.
Katika kudhihirisha kwamba ukosefu wa huduma ya maji ni adha kubwa, Mbunge wa Kwimba, Shanif Mansoor na Richard Ndassa wa Sumve, walitoa kilio kwa Rais Kikwete huku kila mmoja akiomba mradi mpya wa maji ya Ziwa Victoria upelekwe kwanza jimboni kwake.
“Mheshimiwa Rais, mradi wa maji kutoka Ihelele-Kahama- Shinyanga uliofika hadi Mhalo nakuomba sana uupatie fedha ili usambaze maji ya kunywa kwa wananchi wa Jimbo langu la Kwimba.
“Tumechoka kuahidiwa mara kwa mara fedha zikitolewa, leo hii kero ya maji inakwisha hapa Kwimba. Hii itaisaidia CCM kupata kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka kesho,” alisema Mansoor.
Alisema kuwa mradi huo upo karibu kuliko ule unaotokea Magu kwenda Sumve, ambao bado upo kwenye makaratasi.
Naye Ndassa, alisema upatikanaji wa maji ya Ziwa Victoria kutoka mradi wa Magu kupitia Sumve na Malya, jimboni Sumve, utasaidia vijiji zaidi ya 40 kupata maji, na kwamba wananchi wanasumbuka sana kupata maji.
“Kwa nini tugombee fito wakati tunajenga nyumba moja? Mheshimiwa Rais, wananchi wa Sumve na Kwimba wanataka maji. Hili ni tatizo moja…kinachotakiwa hapa ni maji tu bila kujali kwamba yanatokea wapi kwenda wapi,” alisema.
Waziri Maghembe alitakiwa na Rais Kikwete kutoa maelezo ya mipango iliyopo kutatua adha hiyo, ambapo alisema kwamba wiki mbili zilizopita wizara yake ilikuwa inafanya kazi ya kutekeleza mradi wa maji kutoka Ihelele kwenda Kwimba.
“Mheshimiwa Rais, serikali imeweka mipango ya kusambaza maji ya Ziwa Victoria katika maeneo ya Kwimba, Magu, Lamadi, Bariadi, Maswa, Nzega, Mwanhuzi. Mpango huu tumelenga kutatua tatizo hili kubwa,” alisema Waziri Maghembe.
    Chanzo : Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment