RAIS Jakaya Kikwete jana alipata wakati mgumu, baada ya kukutana
na nguvu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Mwanza
katika ziara yake, huku Waziri wake wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, naye
akijikuta akizomewa mbele yake.
Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje, alivunja mwiko baada ya kujiunga
katika msafara huo wa raia akiwa na gari lenye alama za Movement for
Change (M4C) lililokuwa limefungwa bendera mbili za CHADEMA.
Hata hivyo maofisa usalama walipata wakati mgumu kulizuia gari hilo
lisiwepo katika msafara huo, jambo lililozua tafrani kidogo katika
uwanja wa Furahisha ambapo Kikwete alikuwa akihutubia mkutano wa
hadhara.
Awali wakati wa uzinduzi wa wodi ya wazazi iliyoko eneo la Butimba,
Rais alilazimika kumpa Wenje nafasi ya kuwasalimia wananchi baada ya
Mkuu wa Mkoa, Evarist Ndikilo, kutaka kufanya hila ya kumnyima haki hiyo
kama mbunge wa jimbo husika.
Baada ya viongozi wote kutambulishwa bila Wenje kutajwa, wananchi walianza kupaza sauti wakitaka mbunge wao naye atambulishwe.
Wenje baada ya kusimama alimshukuru Rais Kikwete kwa kumpa nafasi hiyo
lakini akamwomba amvumilie kidogo atoe salamu maalumu ya wana Mwanza.
Kama kawaida ya CHADEMA kwenye salamu yao, Wenje aliwaomba wananchi
wakunje ngumi kisha akawasalimu kwa kibwagizo cha peoples… nao
wakamwitikia power!
Akiwa katika viwanja vya Furahisha ambapo Rais Kikwete alichelewa
kuanza mkutano wake, Wenje alifika hapo na kushangiliwa kwa nguvu na
wananchi huku polisi wakiwazuia bila mafanikio.
Ilipofika saa 12 jioni kabla Rais hajaingia uwanjani, wananchi hao
walimtaka Wenje awahutubie huku wakidai bendera ya taifa ishushwe kwani
muda wake ulikuwa umefika.
Kikwete aliingia uwanjani hapo saa 12:10 akiongozana na viongozi
mbalimbali wa chama na serikali lakini wananchi hawakuonyesha
kumshangilia badala yake walikuwa wakimwonyesha alama ya vidole viwili
inayotumiwa na CHADEMA wakiimba ‘peoples…power’.
Katika hatua ya kushangaza wananchi hao walimshangilia kwa nguvu
mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, aliyekuwa ameongozana na Rais huku
wakiwazomea Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, ambaye hakufika
kabisa mkutanoni hapo.
Matata alionekana mapema wakati Rais Kikwete akisomewa taarifa ya
maendeleo makao makuu ya wilaya hiyo lakini hakufika uwanjani kabisa
katika viti vya mbele alionekana naibu wake, Swila Dede.
Baadhi ya wananchi hao walisikika wakisema chini kwa chini kuwa Matata
ni mwizi hawataki kumsikia lakini shangwe na nderemo zikajiri pale
walipotambulishwa Wenje na Kiwia.
Rais Kikwete akiwa wilaya ya Ilemela, wananchi wengi waliokuwa
wamesimama njiani walimwonyesha vidole viwili ikiwa ni alama CHADEMA.
Hata hivyo, hali hiyo ilionekana kumkera kiongozi huyo wa nchi pamoja
na maofisa wa usalama, ambapo wana usalama wakiwemo polisi walionekana
wakiwatisha na kuwazuia wananchi kunyoosha vidole viwili.
Magufuli azomewa
Waziri wa Ujenzi, Dk. Magufuli, alikumbana na jinamizi la kuzomewa
mbele ya Rais baada ya kusimama jukwaani na kutaja jina la Matata,
ambapo wananchi wengi walimzomea kwa miluzi huku wakimnyooshea vidole
viwili.
Adha Magufuli alizomewa pia aliposema wabunge wa Ilemela na Nyamagana
jijini hapa ni wana CHADEMA lakini ndani ya roho zao ni wana CCM.
Pia aliendelea kuzomewa aliposema kuwa iwapo Rais angehitaji kupokea kadi za CHADEMA zilizorudishwa angepokea nyingi.
“Mheshimiwa Rais, nampongeza Meya Matata (akazomewa), lakini pia
wabunge wa Ilemela na Nyamagana wanachapa kazi vizuri, nje CHADEMA
lakini ndani wao CCM (akazomewa).”
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Kikwete alimpongeza mbunge wa
Nyamagana kwa uchapakazi mzuri hasa kusimamia sekta ya elimu na kwamba
wabunge wa namna hiyo wanastahili kuigwa.
Hata hivyo, alisema serikali yake imejipanga vizuri kuhakikisha
usafiri wa reli, ndege, majini na barabara za lami vinaboreshwa maradufu
kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Serikali yangu imeweka nguvu kubwa katika kuboresha sekta ya
uchukuzi, ujenzi na nyinginezo. Hii ni kutaka kuwaletea wananchi wetu
maendeleo ya kisekta,” alisema.
Baadhi ya mawaziri walioongozana na Rais mbali na Magufuli ni Naibu
Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga, Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa Maji, Prof. Jumanne
Maghembe, Naibu Waziri wa Ujenzi na Dk. Charles Tizeba.
|
0 comments:
Post a Comment