Thursday, July 18, 2013


Katibu Mwenezi wa CCM Nape Nnauye akihutubia maelfu ya mashabiki wa CCM

Hawa watu wapo na bila ya shaka wana sababu. Wapo ambao wanaipigia kura CCM na bila ya shaka wana sababu yao kama zao. Ni Watanzania – bila ya shaka – na ni mamilioni – kwa uhakika – na hawa wanajitokeza siku ya kupiga kura na kuchagua wagombea wa CCM na wanaichagua CCM. Swali ambalo labda linahitaji utafiti wa kutosha ni kuwa hawa wapiga kura wanaoichagua CCM au wanachagua mgombea wa CCM ni kina nani na wanafanya hivyo kwanini?

Unaweza kudhani CDM imeshawishi kila mtu Tanzania


Ukifuatia na kusikiliza siasa za Tanzania unaweza kabisa kuamini kuwa CCM inakaribia kufa na kama ingekuwa mgonjwa hospitali basi unaweza kudhania yuko kwenye koma. Ni kama mgonjwa ambaye anajaribu kufufuliwa na mashine huku roho ikiwa imeshikilia uzi tu! Jinsi ambavyo chama kikuu cha upinzani nchini kinaonekana kuenea kila mahali, kikuvutia watu wa kila hali, na kikijionesha ndicho pekee cha kweli ni rahisi kuamini kabisa kuwa waliobakia CCM ni wabunge, madiwani, mabalozi na viongozi wa waandamizi wa CCM. Lakini ukiangalia namba ni wazi lipo kundi kubwa – na si dogo – ambalo bado linaamini, linakubali na liko tayari wakati wowote ule kuchagua wagombea wa CCM na kuichagua CCM. Fikiria: Katika uchaguzi uliopita mgombea wa Urais wa CCM alipata kura zisizopungua milioni 5 huku karibu asilimia 80 vya viti vya Ubunge vikienda CCM!

Sasa ni rahisi kusema kuwa kwenye Urais CCM walichakachua kura lakini vipi kwenye Ubunge? Na hili tumeliona hata kwenye chaguzi ndogo mbalimbali bado hata vijijini wapo wengi ambao ni mashabiki wa CCM na ambao hawajashawishika na ujumbe wa CDM. Fikiria kule Arumeru Mashariki ambapo Joshua Nassari na Sioi Sumari walikuwa wanapambana Nassari alipata kura 32,972 wakati Sioi alipata 26,757; wote walipata kwenye makumi elfu! Hawa watu ni kina nani na kwanini? Mfano mwingine wa karibuni zaidi ni kuwa kwenye uchaguzi wa kata 22 uliofanyika mwezi Juni CCM iliambulia viti 16 –japo ilipoteza kadhaa lakini kwamba bado kuna watu walichagua madiwani wa CCM inabidi ipatiwe majibu.

Wanachagua Watu siyo Chama?

Inawezekana mtu akasema hawa hawachagui chama wanachagua watu; jibu hili linavutia lakini ni nani ambaye hajui kuwa watu wanawakilisha chama? Hakuna mtu anayegombea kujiwakilisha yeye mwenyewe na kwa mfumo wetu ambao ni lazima mgombea awe na chama ni wazi kuwa kuchagua mtu ni kuchagua chama vile vile. Hivyo, ni vigumu sana kutenganisha kati ya kuchagua mtu na kuchagua chama hasa kwa vile mtu aliyesimamishwa na chama anafanyiwa kampeni na chama!

Ni wazi kabisa kuwa japo wanaweza kuangalia mtu anayegombea lakini mwisho wa siku wapiga kura wanajali ni chama gani kimemsimamisha mtu huyo kwani baadhi ya watu ambao walitoka upinzani walipoenda CCM na kusimama walishinda! – wapo wengine nao walikataliwa ndani ya chama huko huko.

Hawaipendi na Kuikubali CHADEMA

Inawezekana hili likawa jibu sahihi zaidi na kuukuu na kali; lakini laweza kuwa ndilo la kweli zaidi. Kwamba, wapo mamilioni ya Watanzania ambao bado hawajaamini, kuukubali au hata kushawishiwa na ujumbe wa CDM – kama ujumbe huo upo. Siyo kwamba hawajausikia ujumbe wa CDM au hawaujui ni kuwa hawajaukubali na haujawashawishi. Maelfu ya watu hawa wameona maandamano, wameona majigambo na hotuba motomoto – Bungeni na nje ya Bunge lakini mwisho wa siku wanasema hawajakubali. Kama hili ni kweli swali hili basi ni muhimu zaidi kwa CDM kulitafutia jibu – kwanini wapo watu ambao hawajakubali ujumbe wa CDM?

Ni kwanini hawaikubali? NI kweli wameaminisjwa ilwa CDM ni chama cha kidini, cha kikabila, cha kighaidi, kinapenda fujo, au kuna kitu zaidi ya haya maneno ya propaganda; yaani hawakubaliani na sera za CDM na mwelekeo wake?


Wananufaika na Utawala Uliopo?

Hili nalo linaweza kuwa sehemu ya lile jibu sahihi. Kwamba maelfu ya watu wanaopigia kura CCM na wagombea wake wanafanya hivyo kwa sababu chini ya mfumo wa utawala wa sasa kundi hilo linanufaika. Inawezekana kuwa ni manufaa ya kiuchumi – wafanyabiashara, wafanyakazi n.k au manufaa ya kihisia (amani, umoja, na utulivu). Inawezekana pia ni watu ambao wanaamini wataweza kufanikiwa zaidi chini ya CCM kuliko chini ya chama kingine chochote kwa hiyo wao hawapigii kura matatizo yao ya sasa bali matumaini ya maisha bora ya baadaye! Je inawezekana ndio maana asilimia 80 ya wapiga kura walimchagua Kikwete aliyekuja na “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania Yanawezekana”?

Kwamba hawa hawakujali maisha yao duni, shida zao na matatizo lukuki ambayo yapo; hawakujali ufisadi na madhara yake na hawakujali mfumo wa kupendeleana sehemu mbalimbali; walichojali ni kuwa labda huko mbeleni na wao watanufaika na hivyo wanapigia kura maisha yao ya baadaye kuliko ya sasa (they are voting for their future not their present)? Kama hili ni kweli, inawezekana kuwa CDM haijawapa matumaini kundi hili juu ya maisha ya baadaye na wana hofu kuwa endapo CDM au chama kingine cha upinzani kikiingia madarakani maisha ya kundi hili yanaweza yasiwe mazuri sana au yatakuwa na mashaka?

Inawezekana watu hawa wameamaini kuwa amani, na utulivu vinawezekana tu chini ya CCM na si chini ya chama kingine? Kama hili ni kweli CDM bado ina maswali ya kujiuliza; je ifanye nini kushawishi kundi hili kuwa amani, utulivu, na umoja utaendelea kuwepo nchini?

Hawa si Wasomi ni watu wa kijijini wanahitaji elimu zaidi

Mojawapo ya majibu ambayo yanaweza kutolewa na baadhi ya watu kuwa hawa wanaoichagua CCM hivi wengi ni watu wakijijini na labda si wasomi. Kwa makosa watu wanaojenga hili wanataka tuamini kuwa wasomi ndio wanataka mabadiliko zaidi! Hata hivyo ukiangalia utaona kuwa wasomi ndio wananufaika zaidi na mfumo wa sasa chini ya CCM na wasomi wengi wamekimbilia huko! Na ukiangalia mgawanyiko wa upigaji kura hasa kwa baadhi ya maeneo utaona kuwa mabadiliko yamekubaliwa zaidi vijijini kuliko mijini. Kama hoja ya usomi na kujua ingekuwa ina nguvu jiji la Dar-es-Salaam lingekuwa na halmashauri zinazoogozwa na upinzani; hakuna! Lakini ndio mahali penye vyuo vingi, shule nyingi, wasomi wengi na kwa uhakika kabisa lenye fedha nyingi zaidi nchini na watu wake wanavyanzo vingi zaidi vya habari lakini ndio wamekuwa wagumu zaidi kukubali upinzani!

Hata kwenye miji utaona ni miji michache bado ambayo imekubali upinzani Arusha Mjini, Mwanza Mjini, Moshi Mjini, Mbeya Mjini, Iringa Mjini, na Musoma Mjini. Sasa kwenye hii miji mingine kuna nini? Songea, Morogoro, Dodoma, Tanga, Tabora, Shinyanga, n.k kunaninini? Lakini ukiangalia vijijini upinzani unazama zaidi na zaidi; CDM inawabunge wengi wa nje ya miji mikubwa kuliko wa mijini! Kwanini hasa? Tungetarajia kuwa vijijini CDM isingeambulia hata mbunge au diwani mmoja lakini tunaona imepata wabunge na madiwani hadi sehemu ambazo haikufanya kampeni sana; fikiria Ukerewe na Maswa Mashariki! Kwanini siyo Temeke, au Ilala; au Morogoro Mjini?

Maswali haya yanahitaji majibu; je ni kwa sababu CCM inafanya vizuri sana kuliko CDM au kwa sababu kuna mbinu nyingi chafu zinazofanya CDM kujipenyeza mijini kuwa ni ngumu zaidi kuliko vijijini. Katika kutafuta majibu ya maswali haya ndio ufunguo wa nani atashinda 2015 umejificha. CDM haipaswi kutegemea kura za chuki dhidi ya CCM kuwa ni kura za mapenzi kwa CDM; hatari yake ni kuwa CCM ikifanya vizuri watu ambao walikuwa hawajafanya uamuzi bado ni rahisi kusema tujaribu nao tena. Kwa mfano Dar patakuwa pagumu sana kwenda 2015 baada ya kukamilika kwa mradi wa DART, kukamilika kwa Daraja la Kigamboni na kuboresheka kwa usafiri wa treni! Na tunavyojua jinsi CCM inavyojua kutumia miradi ya miundombinu kama kete kuelekea 2015 kutakuwa na shambulio la ukarimu hadi kwenye majimbo ya wapinzani; na wapo watakaoshawishika.

Wapo Wenye Mapenzi ya Dhati na CCM?

Jibu jingine ambalo linaweza pia kuwa ni la kweli zaidi ni kuwa wapo maelfu kama siyo mamilioni ya Watanzania ambao kwa sababu zao wenyewe wana mapenzi ya dhati kabisa kwa Chama cha Mapinduzi na hakuna lolote au chochote ambacho CCM inaweza kufanya kikaondoa mapenzi hayo. Hawa inawezekana kabisa wanatambua matatizo ya CCM na utawala wake lakini kama vile mapenzi ya mtoto kwa mzazi ndivyo nao walivyo; wanaipenda CCM kwa sababu hawawezi kupenda kwingine!

Wao wanaamini wakati huu ambapo CCM inapitia wakati mgumu zaidi ndio wakati wa kuonesha mapenzi zaidi kwa CCM kwani wanaamini mambo yakitulia basi na wao watanufaika na nchi itanufaika. Kama kundi hili ni kubwa ndani ya lile linalopigia kura CCM sijui; lakini kama kweli lipo na lina nguvu basi hili ni kundi litakalosumbua sana upinzani na hasa CDM; hawa hawajali CDM inasema nini, inapigania nini, inawakilisha nini, kwa nini, wapi, na kwa vipi! Wao wanachojali ni kuwa CCM iendelee kutawala na hata ikiwezekana hadi qiyama.

Lakini bado swali hili linahitaji majibu na yeyote mwenye majibu atushirikishe; nitayapost majibu mbalimbali kwenye blog hapa: Andika jibu lake – si zaidi ya kurasa moja (1) ukijibu swali hili: Hawa wanaopigia kura CCM ni kina nani hasa na kwanini?tunahitaji comments

0 comments:

Post a Comment