Saturday, August 11, 2012

Picture
Basi la kampuni ya Allys Sport Bus linalosafirisha abiria kutoka Dar es Salaam na Mwanza likiwa limeacha njia na kupinduka baada ya kutokea ajali inayodaiwa kusababishwa na basi la Shabiby lililokuwa likitokea mkoani Dodoma kwenda Dar es Salaam na kusababisha mabasi matatu kuacha njia katika eneo la Mkundi Makunganya barabaraba kuu Dodoma-Morogoro ambapo katika ajali hizo zaidi ya abiria 40 walijeruhiwa mkoani Morogoro
Picture
Kutoka Morogoro -- WATU 45 wamejeruhiwa kwenye ajali baada ya mabasi matatu waliyokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka eneo la Mkundi kwa Makunganya nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro, katika Barabara ya Morogoro - Dodoma.

Ajali hiyo ilitokea saa 2:30 asubuhi kwa kuhusisha mabasi matatu, Kampuni ya Shabiby lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam, Allys Sport na Sumry yaliyokuwa yakitokea Morogoro kwenda Mwanza.

Baadhi ya majeruhi waliokuwa wakisafiri na basi la Shabiby walisema basi hilo lilianza kuyumba na baadaye kuacha njia kisha kupinduka.

Mmoja wa abiria hao, Rashid Shaaban alisema baada ya basi hilo kupinduka, ghafla waliona basi jingine la Sumry likiacha njia na kupinduka wakati lilipojaribu kulipita gari jingine jirani na eneo hilo.

Alisema kuwa wakati kukiwa na msongamano wa magari katika eneo hilo la ajali, basi jingine la Allys Sport liliacha njia na kupinduka na hivyo kutokea ajali tatu katika muda usiozidi dakika 10.

Shaaban alisema baada ya ajali hizo walitokea watu waliokuwa wakijifanya kutaka kutoa msaada, lakini lengo lao lilikuwa ni kuiba mali za majeruhi. Hata hivyo, alisema lengo lao hilo halikufanikiwa kwani muda mfupi baada ya kutokea, askari walifika na kuimarisha ulinzi.

Katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, madaktari na wauguzi walionekana kuzidiwa na wagonjwa kutokana na idadi kubwa ya majeruhi waliokuwa wakihitaji huduma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alithibitisha kutokea kwa ajali hizo na kusema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa zimetokana na utelezi na mwendo kasi.
Picture
Mmoja wa majeruhi wa ajali ya basi la Shabiby, Deogratias Mrai akiwa katika wodi namba moja ya hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro akiuguza majeraha aliyopata kufuatia basi hilo walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka katika eneo la Mkundi-Makunganya Manispaa ya Morogoro lililokuwa likitoka Dodoma kwenda Dar es Salaam na kusababisha mabasi matatu kuacha njia katika eneo la Mkundi Makunganya barabaraba kuu Dodoma-Morogoro ambapo katika ajali hizo zaidi ya abiria 40 walijeruhiwa.
Picture
Picture
(Picha: Juma Mtanda)

0 comments:

Post a Comment