Sunday, July 15, 2012

 Mchungaji wa Kanisa la Christian   Chapel la Dar es Salaam, George Makala (kulia)akifafanua jambo kwa waandishisiku ya jana
WAKAZI 32 wa eneo la Mbezi Beach Kata ya Kilongawima wanakwenda mahakamani kupinga kitendo cha Serikali kuwabomolea nyumba zao hivi karibuni, kitendo ambacho wanadai wameonewa kwani wao wanamiliki maeneo hayo kihalali, huku baadhi yao wakiwa na nyaraka muhimu za umiliki na baraka kutoka Serikali za Mtaa husika.

Wakizungumza na vyombo vya habari leo wakazi hao wamesema wanasikitishwa na kitendo hicho cha mabavu kufanywa na Serikali tena kwa kuvizia ilhali kulikuwa na taratibu za kisheria za kufuatwa kabla ya zoezi hilo kama kulikuwa na haki ya kufanyiwa hivyo.

Akitoa tamko la wakazi wa eneo hilo leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa wakazi hao, Antony Mseke alisema madai ambayo Serikali kupitia Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeyatoa kuwa wao wamevamia eneo la mikoko na kujenga maeneo yasioruhusiwa hayana msingi wowote kwani eneo hilo lipo mbali na mikoko hiyo.

Alisema wanakwenda mahakamani kutafuta haki yao kwa kuwa kilichofanyika ni uvunjaji wa sheria na huenda kuna sababu nyingine wanazo na si kama ilivyotamkwa na waliobomoa.

Mseke alisema eneo hilo kuna mabango ya NEMC ambayo yanaainisha ni eneo gai lisiloruhusiwa kujengwa ambamo imo mikoko ya bahari, lakini katika nyumba zote zilizobomolewa zipo nje na mbali na mipaka ya taasisi hiyo ya mazingira.

“Tumeonewa kupita kawaida tunaiomba Serikali isiwe ikifanya kazi kwa hali kama hii ya mabavu…tunakwenda mahakamani kutafuta haki yetu maana tunaamini tupo hapa kihalali,” alisema kiongozi huyo na mwakilishi wa waathirika wa bomoa bomoa hiyo.

Akifafanua zaidi Mchungaji wa Kanisa la Christian Chapel la Dar es Salaam, George Makala ambaye naye ni mmoja wa wakazi waliokubwa na adha hiyo alisema baadhi yao wamekuwepo eneo hilo tangu mwaka 1992 bila matatizo yoyote huku wakitambuliwa na Serikali za mitaa kihalali.

Alisema anashangaa kuona NEMC kujitokeza na kuwabomolea majengo yao tena bila taarifa kitaratibu. Ameongeza zoezi hilo linaulakini kwani yapo majengo mengine ambayo ni ramani moja eneo hilo lakini hayakubomolewa jambo ambalo linazidi kujenga mazingira ya uonevu.

Alisema pamoja na mambo mengine alama za ‘X’ ziliwekwa Julai 8, 2012 na watu wasiojulikana na baada ya wao kuanza kufuatilia Julai 10, 2012 wavamizi walikuja na silaha kali na kufanya ubomoaji jambo ambalo limewatisha.

“Sisi hatukuwa na mgogoro na Serikali wala kugoma chochote, eneo ambalo mara zote lilikuwa na mvutano lilikuwa mbele yetu tena ni mbali nasi…siku zote tulitambua hilo hata baadhi ya viongozi wa Serikali wanalijua hilo, tunashangaa kuona leo tunabomolewa hivi,” alisema mchungaji huyo ambaye licha ya jingo lake kubomolewa na Kanisa analochunga pia limebomolewa.

Naye Mwanasheria wa Wakazi hao, Living Kimaro kutoka Kampuni ya L & K. Law Chambers ya jijini Dar es Salaam amesema zoezi hilo halikufanyika kitaratibu wala na mamlaka husika hivyo wanakwenda mahakani kudai haki yao.

*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)

0 comments:

Post a Comment