TAARIFA KWA UMMA
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinahimiza wanachama wake na
wananchi kwa ujumla kujitokeza kutoa maoni kwa tume ya mabadiliko ya
katiba ili taifa lipate katiba mpya.
Aidha,
CHADEMA kinatoa mwito kwa wananchi kuondokana na mtizamo kwamba
haiwezekani kutoa maoni ya katiba mpya bila kwanza kuifahamu kwa kina
katiba iliyopo bali waelewe kwamba mchakato huu unahusu kuandika katiba
mpya hivyo jambo la msingi ni wananchi kujitokeza kwa wingi mbele ya
tume ya mabadiliko ya katiba mpya na kutoa maoni kwa kueleza maudhui ya
Tanzania wanayoitaka.
Pamoja
na kutoa maoni kuhusu maudhui ya masuala ya kuzingatiwa katika katiba
mpya, CHADEMA kinatoa mwito kwa wanachama na wananchi kutoa pia maoni
kuhusu mchakato wa katiba mpya ili kuiwezesha tume kuishauri serikali
kuendelea kuiboresha sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ikidhi
mahitaji ya kujenga kuaminiana na muafaka wa kitaifa kwa mawasiliano na
mashauriano na wadau mbalimbali.
Pia,
CHADEMA kinatahadharisha kuwa uamuzi wa tume kutoa elimu wakati huo huo
ikikusanya maoni utaathiri mchakato wa katiba; hivyo pamoja na kutoa
mwito kwa umma kwenda kutoa maoni kwa tume, CHADEMA kinaendelea na
mpango wake wa kutoa elimu kwa wanachama na umma kuhusu mabadiliko ya
katiba.
Wanachama
na wananchi kwa ujumla wazingatie ratiba ya kukusanya maoni kwenye
mikoa minane kuanzia tarehe 2 Julai 2012 hadi tarehe 30 Julai 2012
iliyotangazwa na tume ya mabadiliko ya katiba katika vyombo vya habari
na katika tovuti ya www.katiba.go.tz
Mikoa
hiyo ni Tanga, Kagera, Dodoma, Pwani, Shinyanga, Manyara, Kusini Unguja
na Pemba; na kwa namna ya pekee CHADEMA kinawakumbusha wananchi wa
wilaya za Lushoto, Biharamulo, Bahi, Mafia, Kahama, Mbulu na Kusini
ambapo tume ya mabadiliko ya katiba itaanzia tarehe 2 Julai 2012
kujitokeza kutoa maoni kuwezesha nchi kupata katiba mpya.
Izingatiwe
kwamba wajibu wa kisheria wa tume ya mabadiliko ya katiba ni kuyapokea
maoni na maudhui hayo na kuandika ripoti na hatimaye kuyaweka katika
muundo wa kikatiba wakati wa kuandaa rasimu ya katiba.
“Wananchi
waelewe kwamba mchakato wa katiba mpya unahusu hatma ya nchi na maisha
ya wananchi, kwa mfano kwa muda mrefu pamekuwepo migogoro katika jamii
mingine kuhusu ardhi na rasilimali nyingine. Kupitia mchakato wa katiba
mpya wananchi watoe maoni juu ya misingi ya kikatiba ya kushughulikia
hali hiyo na kulinda haki za msingi za binadamu”.
“Aidha,
taifa lipo katika hali tete hivi sasa kutokana na tishio la migomo ya
madaktari, walimu na watumishi wengine wa umma; chanzo kikiwa mgawo usio
sawa wa rasilimali za nchi unaofanyika wakati wa bajeti, huku mamlaka
makubwa ya kikatiba ya ugawaji na usimamizi wa fedha za umma yakiwa kwa
Rais na serikali badala ya bunge ambacho ndicho chombo kikuu cha
kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi. Hivyo, wananchi wajisikie
huru kwenda kueleza maudhui ambayo wamekuwa wakiyasema mara kwa mara ya
kutaka madaraka ya Rais kupunguzwa na pia kuweka misingi muhimu ya
kudhibiti ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa maoni kwenye
tume ya mabadiliko ya katiba.”
Ifahamike
kwamba miaka mitano iliyopita CHADEMA kilisambaza kwa ngazi zake zake
za chini za chama waraka na. 4 wa 2007 kuhusu madai ya katiba mpya ambao
ulitoa elimu kwa umma baadhi ya masuala ya kuzingatiwa juu ya katiba.
Katika waraka huo CHADEMA kilielekeza viongozi na wanachama wake kwamba
hoja ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi iwe ya kudumu katika vikao vya
kikatiba vya chama pamoja na mikutano na wananchi mpaka pale taifa letu
litakapokuwa na katiba mpya.
Kwa upande mwingine, ikumbukwe kuwa CHADEMA kilishawatahadharisha watanzania kuzingatia kwamba marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya katiba yaliyofanyika mwezi Februari 2012 yalikuwa ni
ya hatua ya kwanza ya kuwezesha kuundwa kwa tume shirikishi ya katiba
kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa ripoti na rasimu ya
katiba mpya.
Hivyo,
ili kuwa na uhakika na mustakabali wa maoni yanayotolewa, wananchi
watoe pia maoni kwa tume kuhusu mchakato wa katiba na pia kuitaka
serikali itoe ratiba ya kufanyika kwa marekebisho mengine muhimu ya
awamu nyingine kuhusu bunge maalum la katiba na hatua ya kutunga katiba
mpya na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya
maamuzi kwa uhuru na kwa haki kabla ya mchakato kufikia katika hatua
husika.
Wakati huo huo;
CHADEMA kinatoa tahadhari kuhusu uamuzi wa tume ya mabadiliko ya katiba
kutangaza moja kwa moja ratiba ya kukusanya maoni ya wananchi bila
kwanza kuwa na ratiba ya kutoa elimu kwa umma kuhusu mchakato wa katiba,
katiba, ukatiba na masuala ya katiba.
Uamuzi
wa tume kutoa elimu wakati huo huo ikikusanya maoni unaweza kuathiri
mchakato wa katiba; hivyo pamoja na kutoa mwito kwa umma kwenda kutoa
maoni kwa tume, CHADEMA kinaendelea na mpango wake wa kutoa elimu kwa
wanachama na umma kuhusu mabadiliko ya katiba na inazitaka ngazi zote za
chama kuzingatia waraka na. 3 wa mwaka 2011 kuhusu sheria ya mabadiliko
ya katiba na kutoa elimu kwa wananchi kuwezesha nchi kupata katiba mpya
na bora.
Imetolewa tarehe 1 Julai 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
0 comments:
Post a Comment