Wednesday, July 11, 2012

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Ilvin Mugeta anatarajia kuketi kwenye kiti cha enzi na kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi Na.1/2007 inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na aliyekuwa Meneja Utawala na Fedha wa ubalozi huo, Grace Martin.

Hukumu hiyo ambayo inasubuliwa kwa shauku kubwa na watu wa kada mbalimbali wakiwemo wasomi wa sheria, wahadhiri wa vyuo vikuu, na wanadiplomasia mbalimbali, inatokana na amri iliyotolewa na Hakimu Mugeta Juni 16 mwaka huu, ambapo alizitaka pande mbili katika kesi hiyo Juni 11 mwaka huu, kuwasilisha kwa maandishi maombi yao kuwana washitakiwa wana hatia au la na pande zote zilitekeleza amri hiyo na akaipanga tarehe ya leo kuwa ndiyo siku atakayotoa hukumu ya kesi hiyo ambayo imedumu mahakamani hapo kwa miaka saba sasa.

Kesi hiyo ilifunguliwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Januari 22 mwaka 2007.

Awali, Mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Lincoln, Ponsia Lukosi na Vicent Haule walidai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa sita ambayo ni kosa la kula njama, wizi wa fedha Euro milioni mbili, kugushi vocha za manunuzi ya jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, kutumia risiti za manunuzi ya jengo hilo kuidanganya Serikali na kuisababishia Serikali hasara ya Euro milioni mbili.

Ili kuithibisha kesi yao, upande wa Jamhuri ilileta jumla ya mashahidi saba ambao ni aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya awamu ya tatu, Martin Lumbanga, Stewart Migwano, Marco Papi, Kaptaini Abubakari Ibrahim, Mkongoti, Kyando toka TAKUKURU na nyaraka mbalimbali.

Upande wa utetezi nao ulileta mashahidi wa tatu ambao ni Balozi Prof. Mahalu, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Grace Martin ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando, Alex Mgongolwa, Beatus Malima na Cuthbet Tenga na kuwasilisha nyaraka mbalimbali za Serikali.

Tarehe 8 Mei mwaka huu, upande wa utetezi ulifunga ushahidi wake baada ya Grace kumaliza kujitetea. Mei 7 mwaka huu, Mahalu ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu kipya cha Bagamoyo alimaliza kujitetea na siku hiyo ndiyo Rais Mkapa aliandika historia mpya nchini kwa upande wa Marais, ambapo alifika mahakamani hapo na kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo.

Julai 16 mwaka 2009, Jaji Sivangilwa Mwangesi ambaye ndiye alikuwa akiisilikiza kesi hiyo tangu ilipofunguliwa mwaka 2007 alitoa uamuzi wake ambapo aliwaona washitakiwa hao wana kesi ya kujibu.

Machi 25 mwaka 2011, washitakiwa hao kupitiwa wakili wao Mabere Marando waliwasilisha ombi la kumwomba Jaji Mwangesi ajitoe kusikiliza kesi hiyo kwa sababu hawana imani naye kwa kuwa amekuwa akikiuka wazi wazi sheria kwa malengo anayoyajua yeye.

Machi 28 mwaka 2011, Jaji Mwangesi alitangaza kujitoa kusikiliza kesi hiyo na saa chache baadaye ya siku iyo hiyo, Hakimu Mugeta aliingia mahakamani hapo akiwa na jalada la kesi hiyo na kusema yeye ndiyo atakayeendelea kusikiliza kesi hiyo.

Fuatilia habari hii Leo kwenye gazeti la Tanzania Daima.

Source: wavuti

0 comments:

Post a Comment