NA Ayoub Mangi
Ndugu Wananchi,
Ndugu Wananchi,
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru
Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu
ya kwanza ya mwaka 2012 salama. Kwa
kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda
kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa
binadamu nchini na la pili ni la mgomo wa madaktari.
Usafirishaji
Haramu wa Binadamu Nchini
Ndugu
Wananchi;
Bila ya shaka
mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43 za watu wasiojulikana,
zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa
wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja
na maiti hao, walipatikana watu 84
wakiwa hai lakini wote wakiwa wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa kuwasafirisha
watu hao hadi Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa Hospitali Kuu
ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika Kituo cha Kati
cha Polisi, Dodoma. Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21
zilipelekwa Morogoro kuhifadhiwa.
Taarifa
zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu hao ni raia
wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye Afrika ya Kusini
ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi Marekani na Ulaya. Kwa mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza
miezi mitano iliyopita. Mwezi mmoja waliutumia
Ethiopia na miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako
walipakiwa kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia
Chitego. Lori walilopanda lilikuwa
limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo kwa kukosa hewa.
Tukio la Chitego,
Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si la kwanza
kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika
kipindi cha takriban miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji
haramu kuingia nchini. Kwa mfano, kati
ya mwaka 2005 na hivi sasa jumla ya wahamiaji haramu 19,683 wamekamatwa. Karibu
wote wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500 tu magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa
makwao. Wengi wa watu hao wanatoka
Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na Bangladesh.
Wahamiaji haramu
wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo rasmi. Wapo wanaotumia nchi kavu hasa kupitia mikoa
ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
Na, wapo wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za Pemba, Unguja na za
mikoa ya ukanda wa Pwani ya Tanzania Bara yaani Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa kauli
zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji nchini kuhamia bali wao ni wapita
njia tu. Wanaelekea Afrika ya Kusini
ambako wameahidiwa kuwa watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na
Ulaya. Watu hao pia wamethibitisha
kuwepo kwa watu maalum wanaojihusisha na usafiri wao tangu nchi watokako na
zote wanazopitia mpaka kule waendako.
Aidha, wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao ili wawasafirishe na hakika
si kiwango kidogo. Kwa jumla ni kwamba
hili si suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya kusafirisha
binadamu.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia vyombo vyetu
vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa ndipo wasafirishaji walipobuni
njia za kuwasafirisha kama mizigo.
Makontena, malori yaliyofunikwa nyuma na matenki ya mafuta na ya maji
yamekuwa yanatumika kwa ajili hiyo.
Usafiri wa aina hiyo ndiyo uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe
26 Juni, 2012 na vya watu 21 vilivyotokea
mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile vya watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa wa Mbeya, mwezi
Mei, 2012.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 27 Juni, 2012
nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuzungumzia tukio la
Chitego na suala zima la biashara hii haramu na hasa mbinu mpya inayotumiwa na
wasafarishaji. Nilitoa pongezi kwa
vyombo vya dola kwa kazi nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli za biashara hii haramu
hapa nchini. Tulielewana kuwa waendelee kuimarisha
udhibiti huo kwa lengo la kukomesha kabisa biashara hii.
Niliagiza pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda
mwaka 2006 kushughulikia ujambazi sasa kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili
tatizo hili. Aidha, kwa pamoja tulikubaliana kuwa nchi yetu ishirikiane na
wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika ya Kusini kutambua
mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria.
Tayari nimeshaanza kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo
kuhusu ushirikiano huo. Nashukuru wote
wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa pamoja kuvunja mtandao huu mchafu na kutokomeza
biashara hii haramu na inayodhalilisha utu wa mwanadamu.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua
nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya Chitego na Mkoka kwa kazi
nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa
kutoa taarifa mapema juu ya jambo lenyewe, lakini pia wameonesha utu kwa
kuwajali wageni waliokumbwa na janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa
Dodoma na Morogoro ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kulishughulikia tatizo hilo
kwa umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana
na ushirikiano ulioonyeshwa na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika
kushughulikia suala hili.
Mgomo
wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa
Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa.
Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond
Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa unaendelea
wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la mgomo na hatua iliyokuwa imefikiwa,
nilielezea mazungumzo yangu na viongozi wa Chama cha Madakari wakiwemo pia
viongozi wa Jumuiya ya Madaktari. Nilitoa
taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na watarudi kwenye meza ya
majadiliano na Serikali. Siku ile pia nilielezea
matumaini yangu kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi yetu. Bahati mbaya matumaini yangu hayo hayakuwa na
hivi sasa tunashuhudia tena wagonjwa wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa
sababu ya kukosa huduma wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma tena.
Ndugu Wananchi;
Kama
walivyoniahidi,
madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi kwenye
mazungumzo na Serikali. Kama
ilivyoagizwa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa
mujibu
wa Sheria ya Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004. Chama cha
Madaktari na Serikali walifika katika
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for Mediation and Arbitration)
kwa
ajili ya majadiliano. Kwa pamoja na kwa
ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya
kuzungumza
wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili makubaliano yao.
Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe
8 Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja
na
kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi;
Kati
ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya
majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari. Katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya
madaktari yalizungumzwa. Mambo hayo ni haya
yafuatayo:
1.
Posho ya kuitwa kazini (on call
allowance) iwe asilimia 10 ya
mshahara.
2.
Posho ya kufanya kazi katika mazingira
hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia
30 ya mshahara.
3.
Madaktari wapatiwe nyumba grade A au
posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30
ya mshahara.
4.
Posho ya kufanya kazi katika mazingira
magumu iwe asilimia 40 ya mshahara.
5.
Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe
magari.
6.
Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara
wa shilingi 3,500,00/= kwa mwezi.
7.
Madaktari wapatiwe Green Card za Bima
ya afya.
8.
Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi
ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
9.
Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa
rufaa nje.
10.
Madaktari waliofukuzwa warudishwe
kazini.
11.
Huduma za afya ziboreshwe nchini.
12.
Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa
mambo saba. La kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini. Serikali ilieleza kuwa upo utaratibu kwa
mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 wa kuwakopesha
wafanyakazi wa Serikali fedha za kununulia magari au pikipiki, samani na
matengenezo ya magari. Ilikubaliwa kuwa
madaktari waitumie fursa hiyo.
Jambo
la pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya. Jambo hili lilikubaliwa na Serikali na Wizara
ya Afya imekwishachukua hatua za utekelezaji wake.
Jambo
la tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu
wa Wizara ya Afya. Kwa pamoja
walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya mamlaka ya Kamati yao ya pamoja,
waziachie mamlaka husika za uteuzi.
Uongozi wa juu wa Wizara umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la kustaajanisha hata Waziri
mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona. Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile
wameyazungumza na Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya mafanikio
Jambo
la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya
kutibiwa nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza,
kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie
maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au
asiwe kiongozi. Pili, walikubaliana
kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa nchini. Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya
Serikali. Nililieleza hili mwezi Desemba
30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge baada ya kuchaguliwa kwa mara ya
kwanza kuongoza nchi yetu.
Tumeiongeza
sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi
bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni
1.2 mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya miundombinu na elimu. Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa
tiba na wataalamu wa afya. Kazi
inaendelea katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali ya Muhimbili. Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa
miaka sita nyuma. Na kazi inaendelea
hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa nje. Matunda yake yanaanza kuonekana kwa upande wa
figo, moyo, kinywa na mipango inaendelea kwa upande wa ubongo na mishipa ya
fahamu. Tunaendelea kuimarisha mafunzo
ya madaktari na madaktari bingwa, yote
kwa nia hiyo hiyo. Hivi sasa Chuo Kikuu
cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua wanafunzi wengi zaidi ya ilivyokuwa
siku za nyuma na makazi mapya ya chuo yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua
wanafunzi wengi zaid. Mwaka 2005 tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka huu tunao 520.
Ndugu Wananchi;
Jambo
la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari
waliofukuzwa. Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa Wizarani
kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na
Lugalo. Hili ni jambo ambalo lilikuwa
limemalizika kitambo na wote walikuwa wamerudi Muhimbili.
Jambo
la sita ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu
kuboresha huduma ya afya. Mapendekezo
hayo yalihusu kutathmini sera na mpango wa afya ya msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya bajeti ya Serikali, kuwepo
na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na kuboresha viwango vya ubora wa
madaktari na kadhalika. Serikali
imeyaafiki mapendekezo hayo na yatafanyiwa kazi.
Jambo
la saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya
uchunguzi wa maiti. Hili ni jambo jipya
halikuwepo mwazoni. Hata hivyo, Serikali
imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi kufikia shilingi 100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi;
Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na kutoafikiana
kwa baadhi ya mambo. La kwanza ni suala la kufanya kazi
katika mazingira hatarishi. Serikali
imekubali hoja ya kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika
mazingira hatarishi. Serikali iliwaeleza
kuwa watumishi wa kada zote za afya watapatiwa chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika
bajeti ya 2012/13.
Aidha,
Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa
watumishi wa umma wanaostahili.
Utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha
mazingira hatarishi ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa
wahusike. Madaktari wamekataa hili la
kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara
moja.
Jambo la pili ambalo wamekubaliana
nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi.
Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za
kuishi. Aidha, imeeleza mpango ulioanza
wa kujenga nyumba 700 za madaktari
kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi wa nyumba
90 unaendelea, 50 katika mkoa wa
Mtwara na 40 katika mkoa wa Rukwa.
Kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya
pango Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu
zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba. Jambo hilo limekataliwa na Madakari na kutaka
lazima walipwe asilimia 30 ya
mshahara kama posho ya nyumba. Serikali
kwa upande wake imeona vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa
wafanyakazi wengine wote wa umma.
Jambo
lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya
kufanya kazi katika mazingira magumu.
Pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya maeneo nchini yanayo
mazingira magumu kwa watumishi wa umma
hivyo hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali
wajibu wa kuweka utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika maeneo
hayo. Kwa ajili hiyo, Serikali itatoa
mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu namna ya kuwasaidia watumishi hao
kupunguza makali ya maisha katika kila eneo badala ya kutegemea posho peke
yake.
Kuhusu posho, Serikali imeeleza kuafiki
kuwepo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha
mazingira husika, kutambua watumishi waliopo na gharama zake.
Madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la
uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa. Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali ni
rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango
vya posho kulingana na mazingira halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo.
Ndugu Wananchi;
Mambo mawili hayakuwa na muafaka
kabisa kati ya pande zetu mbili. Jambo
la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance). Kwanza sina budi kueleza kuwa Serikali
imekubali kuongeza posho hiyo. Tangu
Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi
10,000/= hadi shilingi 25,000/=
kwa daktari bingwa (Specialist), shilingi
20,000/= kwa dakari mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na shilingi 15,000/= kwa madaktari
waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns). Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi
sasa.
Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi
huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia
10 ya mshahara. Ugumu wa kukubali
pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana
kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee
kulipwa. Hili haliwezi kuwa sahihi
kufanya. Linaweza kuwafanya baadhi ya
madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa mwezi malipo
yako pale pale.
Ndugu Wananchi;
Jambo
la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu
mshahara wa kuanzia kazi wa daktari.
Madaktari wanataka uwe shilingi
3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi. Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza
mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka
20 kama ambavyo itafanya kwa
watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari
ataanzia kati ya shilingi 1,100,000/=
na 1,200,000/= kutegemea kiwango
kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa
katakata na wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu Wananchi;
Huo
ndiyo
mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na matokeo ya
mazungumzo yenyewe. Katika kikao cha
sita kilichofanyika tarehe 30 Mei, 2012, upande wa Chama cha Madaktari
ulisema
kuwa kwa vile hoja ya nyongeza ya mshahara haina mabadiliko hawakuona
haja ya
kuendelea na majadiliano mpaka watakapowasiliana na wenzao. Waliahidi
kutoa taarifa ndani ya wiki mbili. Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT
aliandika
barua kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye kiongozi wa majadiliano kwa
upande
wa Serikali, kuwa Madaktari wameikataa taarifa na ufafanuzi waliopewa
kutoka
Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu Wananchi;
Baada ya majibu yale ya madaktari, tarehe 19
Juni, 2012, Serikali na Madaktari walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa
kuwa mgogoro umekosa usuluhishi kama sheria inavyotaka. Kwa pamoja pande zote mbili zilikubaliana
suala hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi. Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu
kufikishwa ngazi hiyo ya juu, upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo
kuanzia saa sita ya usiku tarehe 23 Juni, 2012.
Hatua hiyo haikustahili kwani suala lenyewe halijafika mwisho wa
kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za Mahusiano ya Kazi nchini.
Ndugu Wananchi;
Tarehe
22 Juni, 2012, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu Kitengo cha
Kazi kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la muda kufanywa. Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza
kuwa mgomo usitishwe. Juhudi za
kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na viongozi wengine wa MAT hazikufanikiwa,
Ofisi ya MAT ilikuwa imefungwa na simu zote za viongozi wa MAT zilikuwa
zimezimwa. Hatimaye tarehe 25 Juni,
2012, alipatikana na kupewa amri hiyo ya Mahakama. Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika
Mahakamani ambapo alikana kuwa yeye hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini
hakumtaja aliyehusika. Pamoja na rai hiyo,
Jaji alimuamuru Rais wa MAT akawatangazie wanachama wake kusitisha mgomo. Dkt.
Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi leo na mgomo umekuwa unaendelea kinyume cha
Sheria.
Ndugu Wananchi;
Wagonjwa
wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali kisheria
ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari. Viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika
mgogoro na Mahakama na waajiri wao isivyostahili. Ni vyema viongozi wa Madaktari na madaktari
wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao
mkuu amekana Mahakamani kuwa hahusiki nao.
Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka hatarini. Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na
mwajiri kwa kushiriki mgomo unaokubalika kisheria. Huu siyo.
Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia, hawana cha kiwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha
yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali. Lazima watafakari sana kwa hayo
wafanyayo.
Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia maneno niliyoyasema
tarehe 12 Machi, 2012, kuwa kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni
Sera ya Serikali yetu kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Tawala (CCM). Tumeitekeleza kwa vitendo sera hiyo, hata
hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa nia yangu njema tu pekee haitoshi, lazima uwezo
wa kufanya hivyo uwepo. Kwa kulingana na
uwezo uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi hatua
kwa hatua tangu tuingie madarakani.
Tumefanya hivyo kwa jumla kwa wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za
watumishi wa umma.
Miongoni
mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za Serikali ni madaktari na
watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya.
Tena nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo mkubwa kuliko
watumishi wengine wa umma. Upendeleo upo
kwenye mafunzo ambapo wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa
asilimia mia moja wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka
2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi 178,700/=, mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=. Tuliendelea kuupandisha mwaka
hadi mwaka mpaka kufikia shilingi 957,700/=
wanazolipwa sasa. Kiasi hicho ni mara
mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma nyingine wenye shahada ya kwanza
wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata shilingi 446,100/=.
Tunafanya
hivyo kwa kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii na
ukweli kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari
nchini. Lakini inaonekana juhudi zetu
zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu Wananchi;
Sina
budi kusisitiza kwamba tunapofanya hivyo
tunaongozwa na uwezo tulio nao wa kulipa.
Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa kuwalipa mshahara wa
kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na
posho zote zile. Tukifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa
shilingi 7,700,000/=. Kwa hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema
kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana
na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini
bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na kwenda kwa muajiri
anayeweza kumlipa kiasi hicho. Nasi
tutamtakia kila la heri. Hana sababu ya
kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa mshahara
huo. Isitoshe, hana sababu ya kuendelea
kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka. Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa
kukuandikia barua ya kujieleza au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo
na kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka
kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24.
Jiepushe na yote hayo kwa kujiondoa mwenyewe. Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana jinsi
bali kukuondoa kazini maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na maadili ya kazi
ya udaktari.
Mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo
na wataendelea kufanya hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma. Najua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna
manun’guniko ya kuonewa. Hivyo, mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya
hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na
huyo ajae awe na mahali pa kuishi. Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae
daktari ambae hayupo kazini na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi ya watumishi wa
umma wakiwemo madaktari iko wazi. Tumekuwa tunafanya hivyo, na tutaendelea
kufanya hivyo kulingana na uwezo wa kibajeti.
Ni vyema watumishi wa umma wakatambua kuwa hatuwezi kutumia fedha zote
au kiasi kikubwa mno cha pesa za umma kulipana mishahara. Tukifanya hivyo, Serikali itashindwa kutoa
huduma muhimu kwa wananchi ambao ndiyo wengi na wanastahili kuhudumiwa. Hata hizo huduma za afya tunazosema ni duni
tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu kubwa ya pesa za
Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi.
Hivi
sasa matumizi ya mishahara ni asilimia
48 ya bajeti ya Serikali. Kiwango
hicho ni kikubwa mno. Uwiano mzuri ni
kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi asilimia
35 ya bajeti na asilimia 65
zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na
taifa. Sisi tumezidi kwa asilimia 13. Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa
manufaa ya walio wengi.
Suala la Dkt. Steven
Ulimboka
Ndugu Wananchi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote kuelezea
masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha kinyama
alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni, 2012. Kitendo hicho
ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo.
Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili
ukweli ujulikane. Nimesema kuwa
ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana
shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.
Natambua
kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani
siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo.
Dkt. Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya
Serikali na Madkatari. Ni kweli kwamba
yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano
haya. Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo,
lakini nilisema wamuache maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea
vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kama
nilivyoeleza, mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa
yamepatikana. Yapo maeneo machache na
hasa eneo la mshahara ambalo hatukuweza kukubaliana. Hapo tulipofikia si pabaya na tulikubaliana
sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa.
Kwa nini Serikali imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu
imekwishatoa amri ya kusitisha mgomo.
Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola ambao
wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo.
Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven Ulimboka
kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa
kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kwa niaba yangu na
kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt. Steven Ulimboka na kumuombea
apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa
taifa. Kwa namna ya pekee namshukuru na
kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na upendo na kwa hatua
alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba kumaliza kwa
kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini. Watanzania wenzenu wanateseka na kupoteza
maisha. Muwe na moyo wa huruma na upendo
na msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu kinavyowataka.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment