Mgomo wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi
sasa. Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond
Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa
unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la mgomo na hatua
iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na viongozi wa Chama
cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya Madaktari. Nilitoa
taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na watarudi kwenye meza
ya majadiliano na Serikali. Siku ile pia nilielezea matumaini yangu kuwa
mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi yetu. Bahati mbaya matumaini
yangu hayo hayakuwa na hivi sasa tunashuhudia tena wagonjwa wakiteseka,
kuhangaika na wengine kufa kwa sababu ya kukosa huduma wanazostahili kwa
vile madaktari wao wamegoma tena.
Ndugu Wananchi;
Kama
walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi
kwenye mazungumzo na Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu,
Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano
Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004. Chama cha Madaktari na Serikali walifika
katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for Mediation and
Arbitration) kwa ajili ya majadiliano. Kwa pamoja na kwa ridhaa yao
wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya kuzungumza wao
wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili makubaliano yao.
Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe 8
Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja
na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika
vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari.
Katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa.
Mambo hayo ni haya yafuatayo:
1.Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya mshahara.
2.Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.
3.Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30 ya mshahara.
4.Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara.
5.Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari.
6.Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa mwezi.
7.Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
8.Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
9.Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
10.Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
11.Huduma za afya ziboreshwe nchini.
12.Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana
wa pamoja kwa mambo saba. La kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na
kurudi kazini. Serikali ilieleza kuwa upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka
wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 wa kuwakopesha wafanyakazi
wa Serikali fedha za kununulia magari au pikipiki, samani na matengenezo
ya magari. Ilikubaliwa kuwa madaktari waitumie fursa hiyo.
Jambo la pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya.
Jambo hili lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya Afya imekwishachukua
hatua za utekelezaji wake.
Jambo la tatu, ni kuhusu hatua za
kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya. Kwa
pamoja walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya mamlaka ya Kamati yao
ya pamoja, waziachie mamlaka husika za uteuzi. Uongozi wa juu wa Wizara
umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la kustaajanisha
hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa
kumuona. Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na
Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya mafanikio
Jambo la nne
walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa
nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza, kwamba maelekezo ya Waziri
Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie maadili ya kazi zao
na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au asiwe
kiongozi. Pili, walikubaliana kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili
viongozi watibiwe hapa nchini. Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera
ya Serikali. Nililieleza hili mwezi Desemba 30, 2005 katika hotuba
yangu ya kuzindua Bunge baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza
nchi yetu.
Tumeiongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutoka
shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2 mwaka 2011/12
na imekuwa ya tatu baada ya miundombinu na elimu. Tumeziimarisha
hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na wataalamu wa afya. Kazi inaendelea
katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali ya Muhimbili.
Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka sita nyuma. Na kazi
inaendelea hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa nje. Matunda
yake yanaanza kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa na mipango
inaendelea kwa upande wa ubongo na mishipa ya fahamu. Tunaendelea
kuimarisha mafunzo ya madaktari na madaktari bingwa, yote kwa nia hiyo
hiyo. Hivi sasa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua
wanafunzi wengi zaidi ya ilivyokuwa siku za nyuma na makazi mapya ya
chuo yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua wanafunzi wengi zaid. Mwaka
2005 tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka huu tunao 520.
Ndugu Wananchi;
Jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari
waliofukuzwa. Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa Wizarani
kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala
na Lugalo. Hili ni jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote
walikuwa wamerudi Muhimbili.
Jambo la sita ni kuhusu
mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu kuboresha huduma
ya afya. Mapendekezo hayo yalihusu kutathmini sera na mpango wa afya ya
msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya bajeti ya Serikali, kuwepo
na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na kuboresha viwango vya ubora
wa madaktari na kadhalika. Serikali imeyaafiki mapendekezo hayo na
yatafanyiwa kazi.
Jambo la saba, ambalo pande zote
walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti. Hili ni
jambo jipya halikuwepo mwazoni. Hata hivyo, Serikali imelikubali na
posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi kufikia shilingi
100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi;
Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na
kutoafikiana kwa baadhi ya mambo. La kwanza ni suala la kufanya kazi
katika mazingira hatarishi. Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua ya
kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi.
Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada zote za afya watapatiwa
chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika
bajeti ya 2012/13.
Aidha, Serikali imeeleza dhamira ya
kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa watumishi wa umma
wanaostahili. Utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa
kubainisha mazingira hatarishi ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na
nani hasa wahusike. Madaktari wamekataa hili la kufanya uchambuzi,
wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya
mshahara na kianze mara moja.
Jambo la pili ambalo wamekubaliana
nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi. Serikali imekiri wajibu wake wa
kuwapatia madakari nyumba za kuishi. Aidha, imeeleza mpango ulioanza wa
kujenga nyumba 700 za madaktari kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi
wa nyumba 90 unaendelea, 50 katika mkoa wa Mtwara na 40 katika mkoa wa
Rukwa.
Kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango
Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa
taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba.
Jambo hilo limekataliwa na Madakari na kutaka lazima walipwe asilimia 30
ya mshahara kama posho ya nyumba. Serikali kwa upande wake imeona
vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa wafanyakazi
wengine wote wa umma.
Jambo lingine ambalo lilikuwa na
makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya kazi katika
mazingira magumu. Pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya
maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma hivyo hatua
zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali wajibu wa
kuweka utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika maeneo hayo.
Kwa ajili hiyo, Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu
namna ya kuwasaidia watumishi hao kupunguza makali ya maisha katika kila
eneo badala ya kutegemea posho peke yake.
Kuhusu posho,
Serikali imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa
baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika, kutambua
watumishi waliopo na gharama zake.
Madaktari hawajakubali kusubiri
zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa.
Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali ni rai ya Serikali ya kubaini
maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho kulingana
na mazingira halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo.
Ndugu Wananchi;
Mambo mawili hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili. Jambo
la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance). Kwanza sina
budi kueleza kuwa Serikali imekubali kuongeza posho hiyo. Tangu
Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi shilingi
25,000/= kwa daktari bingwa (Specialist), shilingi 20,000/= kwa dakari
mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na shilingi 15,000/= kwa madaktari
waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns).
Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa.
Madaktari kwa
upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe
asilimia 10 ya mshahara. Ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa
sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha
mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa
na hakutokea aendelee kulipwa. Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya.
Linaweza kuwafanya baadhi ya madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile
wana hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale pale.
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari
ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari. Madaktari wanataka uwe
shilingi 3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi.
Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia
15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika
mwaka huu wa fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari
ataanzia kati ya shilingi 1,100,000/= na 1,200,000/= kutegemea kiwango
kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na
wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu Wananchi;
Huo
ndiyo mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na matokeo
ya mazungumzo yenyewe. Katika kikao cha sita kilichofanyika tarehe 30
Mei, 2012, upande wa Chama cha Madaktari ulisema kuwa kwa vile hoja ya
nyongeza ya mshahara haina mabadiliko hawakuona haja ya kuendelea na
majadiliano mpaka watakapowasiliana na wenzao. Waliahidi kutoa taarifa
ndani ya wiki mbili. Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT aliandika barua
kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye kiongozi wa majadiliano kwa upande
wa Serikali, kuwa Madaktari wameikataa taarifa na ufafanuzi waliopewa
kutoka Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu Wananchi;
Baada ya
majibu yale ya madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na Madaktari
walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro umekosa
usuluhishi kama sheria inavyotaka. Kwa pamoja pande zote mbili
zilikubaliana suala hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi.
Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu kufikishwa ngazi hiyo ya juu,
upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia saa sita ya
usiku tarehe 23 Juni, 2012. Hatua hiyo haikustahili kwani suala lenyewe
halijafika mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za Mahusiano ya
Kazi nchini.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 22 Juni, 2012,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi
kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la muda kufanywa.
Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa mgomo usitishwe. Juhudi
za kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na viongozi wengine wa MAT
hazikufanikiwa, Ofisi ya MAT ilikuwa imefungwa na simu zote za viongozi
wa MAT zilikuwa zimezimwa. Hatimaye tarehe 25 Juni, 2012, alipatikana na
kupewa amri hiyo ya Mahakama. Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika
Mahakamani ambapo alikana kuwa yeye hahusiki na kuitisha huo mgomo
lakini hakumtaja aliyehusika. Pamoja na rai hiyo, Jaji alimuamuru Rais
wa MAT akawatangazie wanachama wake kusitisha mgomo. Dkt. Namala Mkopi
hajafanya hivyo hadi leo na mgomo umekuwa unaendelea kinyume cha Sheria.
Ndugu Wananchi;
Wagonjwa wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa
halali kisheria ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili
ya udaktari. Viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika
mgogoro na Mahakama na waajiri wao isivyostahili. Ni vyema viongozi wa
Madaktari na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa
halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana Mahakamani kuwa hahusiki
nao. Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka hatarini.
Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki mgomo
unaokubalika kisheria. Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana pa
kukimbilia, hawana cha kiwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha
maisha yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa
halali. Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo.
Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa
kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu
kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Tawala (CCM). Tumeitekeleza kwa vitendo
sera hiyo, hata hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa nia yangu njema tu pekee
haitoshi, lazima uwezo wa kufanya hivyo uwepo. Kwa kulingana na uwezo
uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi hatua
kwa hatua tangu tuingie madarakani. Tumefanya hivyo kwa jumla kwa
wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za watumishi wa umma.
Miongoni mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za Serikali
ni madaktari na watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya. Tena
nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo mkubwa kuliko watumishi
wengine wa umma. Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo wanafunzi wa
udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa asilimia mia moja wakati
wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi
178,700/=, mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=.
Tuliendelea kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi
957,700/= wanazolipwa sasa. Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya
watumishi wa taaluma nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi
ambao kwa wastani hupata shilingi 446,100/=.
Tunafanya hivyo kwa
kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii na ukweli
kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari nchini.
Lakini inaonekana juhudi zetu zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu Wananchi;
Sina budi kusisitiza kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo
tulio nao wa kulipa. Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa
kuwalipa mshahara wa kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na posho zote zile.
Tukifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi
7,700,000/=. Kwa hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi
hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya
kazi Serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na
kwenda kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho. Nasi tutamtakia kila
la heri. Hana sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo.
Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo. Isitoshe, hana sababu ya kuendelea
kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka.
Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya kujieleza
au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na
kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa
kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote
hayo kwa kujiondoa mwenyewe. Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana
jinsi bali kukuondoa kazini maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na
maadili ya kazi ya udaktari.
Mamlaka za ajira zimeanza
kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya hivyo kwa wote wanaoendelea
kugoma. Najua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna manun’guniko ya
kuonewa. Hivyo, mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili
ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo
ajae awe na mahali pa kuishi. Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae
daktari ambae hayupo kazini na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi
ya watumishi wa umma wakiwemo madaktari iko wazi. Tumekuwa tunafanya
hivyo, na tutaendelea kufanya hivyo kulingana na uwezo wa kibajeti. Ni
vyema watumishi wa umma wakatambua kuwa hatuwezi kutumia fedha zote au
kiasi kikubwa mno cha pesa za umma kulipana mishahara. Tukifanya hivyo,
Serikali itashindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi ambao ndiyo wengi
na wanastahili kuhudumiwa. Hata hizo huduma za afya tunazosema ni duni
tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu kubwa ya pesa
za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi.
Hivi sasa matumizi
ya mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya Serikali. Kiwango hicho ni
kikubwa mno. Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi
asilimia 35 ya bajeti na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na
shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa. Sisi tumezidi kwa
asilimia 13. Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio
wengi.
0 comments:
Post a Comment