na Charles Misango, Dodoma
SIKU moja baada ya Mbunge wa Musoma Vijini, Nimrod Mkono (CCM),
kuibu ufisadi mpya katika mgodi wa makaa ya mawe Kiwira, Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amezima hoja hiyo akidai
mbunge huyo ana maslahi ya kibiashara.
Profesa Muhongo, alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu hoja za wabunge
katika kuhitimisha mjadala wa taarifa ya hali ya uchumi na mpango wa
maendeleo kwa miaka mitano, iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Akizungumza kwa kujiamini, waziri huyo bila kumtaja Mkono kwa jina,
alisema kuwa hawezi kujibu hoja zake kuhusu ufisadi wa Kiwira kwa vile
mbunge huyo ni mwakilishi wa kampuni moja ya Dubai ya madini, na hivyo
asingeweza kuzungumzia taarifa za watu walio katika ushindani wa
kibiashara.
Hata hivyo, hoja hiyo ilionekana kumkera Mkono, ambaye aliomba kutoa
taarifa na kumtaka waziri huyo kufuta kauli yake kwa vile katika mchango
wake wa kimaandishi, aliweka bayana kuwa ana mgongano wa kimaslahi kama
kanuni zinavyotaka.
“Mheshimiwa Spika, jana wakati nachangia niliweka wazi mgongano wa
kimaslahi, ingawa nilifanya hivyo kimaandishi kutokana na muda mdogo wa
kuchangia kwa maneno. Hivyo namwomba waziri kufuta kauli hiyo,” alisema
Mkono.
Ombi lake nalo liligonga mwamba baada ya Spika Anne Makinda, kudai
kuwa, hata waziri hakuwa amemtaja jina hivyo si lazima kulalamikia jambo
hilo.
Mkono ambaye alilazimika kutii amri ya kiti, alionekana kuzungumza
chini chini, kabla ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) kusimama
na kuomba mwongozo, akitaka waziri ajibu hoja za tuhuma za Kiwira hata
kama hakutaka kujadili suala la uhusiano wa maslahi wa mbunge Mkono, kwa
vile ni nzito na zinahitaji majibu yakinifu.
Hoja ya Mnyika nayo ilipigwa chini na Spika kwa kudai kuwa, suala hilo litamalizwa kwa kufuata utaratibu.
Juzi, wakati akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya serikali kwa
mwaka 2012/2013, Mkono alidai kuwa uuzaji wa mgodi huo ni kinyume na
makubaliano yaliyofikiwa na Bunge mwaka 2007 ambapo liliagiza kwamba
mgodi huo uliokuwa umeuzwa kwa Kampuni ya Tan Power urudishwe serikalini
baada ya kuwa umeuzwa kwa dola laki saba tu.
Mkono alisema kuwa katika hali ya kushangaza, Kampuni ya Tan Power
ambayo ilikuwa imeingia ubia na serikali iliuzwa kwa Waustralia kiasi
cha mabilioni ya dola.
Aliliomba Bunge kuunda kamati maalumu kuchunguza uuzaji wa Kampuni ya
Tan Power kwa bei ya kutupwa kwa kampuni moja ya Australia.
“Mheshimiwa Spika, Kiwira kulikoni? Lini Bunge litaunda kamati ya
kwenda kuangalia Kiwira?” aliuliza mbunge Mkono ambaye pia ni
mwanasheria maarufu nchini.
Alisema pamoja na yote hayo, sasa serikali imetenga sh bilioni 40 kwa
ajili ya mradi wa Kiwira na kuhoji nani aliteketeza fedha za awali
zilizotolewa kwa ajili hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Muhongo alitangaza kiama kwa wafanyakazi
wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) na kuagiza kuwa kuanzia
sasa atawawajibisha mara moja watendaji watakaofanya kazi kwa uzembe.
Aliagiza shirika hilo kuhakikisha limewawekea umeme wateja wote walioomba na kulipia kufikia Juni 31.
“Natoa amri kuwa wale wote waliokuwa wamelipia kabla ya 31 Mei,
wanapaswa kuunganishiwa umeme mwisho wa mwezi huu na ikiwa bado watoe
taarifa wizarani ama kwangu mwenyewe.
“Mambo sasa ni kwa vitendo, na TANESCO wajue kuwa hakuna mjadala
katika utendaji wa kazi. Ama wanatekeleza au hawawezi,” alisema.
Kuhusu gesi, alisema rasimu ya sera ya gesi itapitiwa na wataalamu
wote Julai, na kisha wataitisha maoni ya Watanzania nchi nzima ili
waichambue, na watakwenda katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuwashirikisha
wananchi wa huko kabla ya kuleta muswada bungeni Oktoba mwaka huu.
Kwa upande wa madini, alisema kuwa leo atakutana na wachimba madini
kote nchini ili kuweka mikakati ya namna ya kuboresha uchimbaji na
ukusanyaji kodi na umiliki wa leseni.
0 comments:
Post a Comment