MBUNGE wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka (CCM) ametaka kujua
mpango wa dharura wa serikali katika kumaliza tatizo la msongamano wa
barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani ambayo inadidimiza
uchumi wa nchi.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, mbunge huyo alisema tatizo la
msongamano katika barabra hiyo ni kubwa na linadidimiza uchumi wa nchi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Gerson Lwenge
alisema serikali itazingatia hilo na itahakikisha kunakuwepo na barabara
za watembea kwa miguu na zile za magari.
“Watu wanatakiwa kufuata sheria na kuacha kupitisha magari kwenye
barabara za watembea kwa miguu, kwani ndicho kitu ambacho kimekuwa
kikifanyika, kwa watu wengi wanapoona msongamano umezidi wamekuwa
wakikiuka sheria na kupita kwa watembea kwa miguu hiyo sio haki,”
alisema Lwenge.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango
gani kabambe wa kupanua barabara ya kutoka Dar es Salaam hadi Kibaha
kuwa njia nne au sita, ili kuondoa tatizo hilo la msongamano.
Akijibu swali hilo, Lwenge alisema serikali ina mpango wa kujenga
“Express way” kuanzia Dar es Salaam hadi Chalinze kwa kilomita 100 ya
njia sita kwa njia tatu kila upande.
0 comments:
Post a Comment