KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, ameiponda hotuba ya bajeti iliyosomwa bungeni juzi,
akisema inaonyesha wazi kuwa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM),
imefikia mwisho wa kufikiri.
Alisema kuwa kitendo cha serikali kushindwa kutafuta vyanzo vipya vya
mapato na badala yake kuendelea kutegemea vinywaji laini na vileo na
kuruhusu wananchi waweke majina yao kwenye pleti za magari badala ya
namba za magari ni hatua kuwa hawana ubunifu wa kukuza uchumi.
Akizungumza na Tanzania Daima jana jioni kwa njia ya simu kuhusu
bajeti hiyo, Dk. Slaa ambaye alikuwa mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu
mfululizo, alisema licha ya kwamba ni mapema kutoa maoni lakini bajeti
imejaa matamko ya kisiasa.
“Hayo aliyosoma Waziri William Mgimwa ni matamko ya kisiasa si hotuba
ya bajeti, kwani tunaoelewa bajeti ni vitabu vinne wanavyopewa wabunge,
nami navingojea nimeomba nipatiwe ila kama ndiyo hivyo alivyosoma tuko
kwenye hali mbaya,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kuwa kinachoshangaza ni kuongezeka kwa deni la taifa halafu
fedha zinazokopwa na serikali imezielekeza kwenye matumizi ya kawaida
badala ya maendeleo.
“Taifa linakopa ili iweje, kulipana mishahara na posho ama? Hii ni
hatari kwa vizazi vijavyo miaka 30 hadi 40 ijayo. Zamani hata serikali
zilizotangulia zilikopa lakini mikopo hiyo ilitumika kujenga viwanda,
shule, barabara na huduma nyingine, leo tunafanya hivyo?” alhoji.
Alisema inashangaza kuona serikali inakopa kutoka vyombo vya biashara
halafu inapelekea fedha hizo kwenye uendeshaji jambo lililozifanya hata
taasisi za fedha za kimataifa kuwanyima mikopo na hivyo wamekimbilia
kwenye mabenki.
Alifafanua kuwa ni katika makosa kama hayo imenyimwa mkpo wa sh
bilioni 480 kwa ajili ya Shirika la
Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO).
Kuhusu vyanzo vya mapato, Dk. Slaa alisema anashangaa kuona kila mwaka
serikali akili yake inalalia kuongeza kodi kwenye vileo na kuacha sekta
nyeti kama madini.
“Tumerudia vyanzo vile vile ukiacha hicho cha watu kuruhusiwa kutumia
magari yenye majina yao badala ya namba za usajili, sasa labda walevi
watakapogoma kunywa ndipo serikali itapata ubunifu wa kuangalia vyanzo
vingine,” alisema.
Hata hivyo, Dk. Slaa aliponda chanzo kipya cha mapato cha kuwaruhusu
watu kuweka majina badala ya namba, akidai kuwa hatua hiyo mbali na
kuleta matabaka kisaikolojia kwa wenye fedha kujiona wameiweka serikali
mfukoni lakini pia ina madhara kuichumi.
“Mafisadi hawaoni uchungu hata kidogo kutumia fedha ila jambo la
msingi ni kwamba wamezipataje, sasa kwa hali kama hii watafurahi kwa
vile wanaona serikali imewahalalisha bila kujali kama fedha zao ni
haramu,” alidai.
Aliongeza kuwa hata, vipaumbele ambavyo serikali imeelekeza kwenye
bajeti yake, utekelezaji wake utakuwa mgumu kwani fedha zilizotengwa ni
ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.habari na http://www.freemedia.co.tz/daima
0 comments:
Post a Comment