WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa, anadaiwa kusoma
hotuba ya bajeti iliyojaa kasoro nyingi, ikiwa ni pamoja na kukosekana
kwa vipengele muhimu vilivyokubaliwa na Kamati ya Uchumi na Fedha.
Kwa kufanya hivyo, waziri huyo sasa anashutumiwa kwa kuidharau na
kukiuka kwa makusudi maagizo ya kamati hiyo yaliyokuwa na lengo la
kuiboresha bajeti ili ilete manufaa kwa wananchi.
Tuhuma hizo nzito zilitolewa jana na mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina
(CCM), mbele ya waandishi wa habari, na kutangaza rasmi kuipinga bajeti
hiyo kwa madai kuwa haina tija kwa wananchi wanyonge.
Aidha alisema kuwa bajeti iliyosomwa bungeni ilikataliwa na kamati
hiyo bungeni kutokana na kubaini kuwa ni mbovu na haikidhi vigezo na
malengo ya kumkomboa Mtanzania maskini.
Mpina ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, alisema kuwa walimtaka Waziri
Mgimwa kwenda kuifumua upya na kufanya marekebisho, lakini serikali
imekataa ikitoa sababu na visingizo vingi.
Kwa kujiamini, Mpina alisema kitendo cha waziri Mgimwa kutojali
mapendekezo yao, kimeifanya bajeti hiyo kuonyesha kuwa serikali haina
nia njema ya kuboresha maisha ya Watanzania ambao kila siku wanapiga
kelele juu ya kuwepo kwa umaskini uliokithiri.
Mpina alisema kuwa anajua msimamo wake huo, unaweza kumletea matata
ndani ya CCM, lakini akadai kuwa yuko tayari kwa lolote hata ikiwa ni
kufukuzwa ndani ya chama hicho.
Mpina alisema bajeti hiyo imejaa upungufu mwingi, ikiwemo kuelekeza
fedha nyingi katika matumizi makubwa ambayo siyo ya msingi na kuyaacha
mambo ya maendeleo.
Alifichua kuwa bajeti hiyo, pia imekiuka makubaliano ya wabunge ya
utekelezaji wa mpango wa miaka mitano wa maendeleo ambao unalenga
kuboresha maisha ya Watanzania ambao wamekata tamaa kutokana na umaskini
walionao.
Mpina alibainisha kasoro nyingine kubwa kuwa ni ukiukwaji wa maagizo
ya wabunge ambao waliitaka serikali kuhakikisha kila mwaka wa fedha
inatenga sh tirilioni 2.7 kutoka katika fedha za ndani kugharamia miradi
ya maendeleo na kutenga asilimia nyingine 35 ya bajeti kwa ajili hiyo.
Mbunge huyo alisema pia katika makubaliano ya wabunge na serikali
yaliyokiukwa katika bajeti hiyo ni kuhakikisha kuwa fedha za umma
zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo hazitumiki kwa ajili ya
mambo mengine.
Mpina alizidi kufichua kuwa wakati wa kujadili mpango wa maendeleo wa
miaka mitano, aliyekuwa Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo, aliwahakikishia
wabunge kuwa mambo hayo yangezingatiwa kikamilifu na fedha hizo
zingetengwa kila mwaka, ikianza na bajeti ya mwaka huu.
“Lakini ukisoma bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi
inaonesha kuwa matumizi ya kawaida yametengewa trilioni 10.5, sawa na
asilimia 70, na matumizi ya maendeleo yametengewa trilioni 4.5, sawa na
asilimia 30, wakati fedha za ndani zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya
maendeleo ni trilioni 2.2 tu, badala ya 2.7,” alisema.
Alisema kitendo cha serikali kutenga trilioni 2.2 badala ya trilioni
2.7 ambayo inaleta tofauti ya sh bilioni 500, iliyoainishwa awali katika
mpango wa maendeleo, kimeifanya miradi mingi kutengewa fedha kidogo
huku mingine mingi ikikosa fedha kabisa.
“Kibaya zaidi katika bajeti hii, mapato ya ndani kwa sasa yameongezeka
kwa trilioni 1.5, huku matumizi ya kawaida yakipanda kwa trilioni 1.9
wakati fedha za maendeleo zikipungua kwa bilioni 397.8 ikilinganishwa na
mwaka wa fedha 2011/12.
“Hapa inadhihirisha dhahiri kuwa serikali haina nia ya dhati ya kupunguza matumizi ya kawaida,” alisema Mpina.
Mbunge huyo alizidi kusisitiza kuwa wakati serikali ikiendeleza
matumizi makubwa yasiyokuwa na tija, Watanzania wengi wanakufa kwa
kukosa matibabu kutokana na kukosekana kwa zahanati, dawa na waganga na
wengine wakikabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama, elimu bora
kutokana na upungufu mkubwa wa madarasa na nyumba za walimu.
Mpina aliongeza kuwa kwa kipindi kirefu serikali imekuwa ikitoa ahadi
za kupunguza matumizi ya kawaida ili kuongeza kasi ya utoaji huduma na
uwekezaji katika sekta zinazokuza uchumi na kupunguza umaskini.
Alitoa mfano wa wizara mbili za Nishati na Madini na Fedha na Uchumi
ambazo zimejipangia kiasi kikubwa cha fedha kwa matumizi aliyoyaita kuwa
si ya lazima.
Kwa Wizara ya Nishati na Madini, Mpina alibainisha kuwa imejitengea sh
milioni 142 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya mafunzo ya nje, wakati
mwaka jana ilitenga sh milioni 34, hivyo kuwa na ongezeko la milioni
108.
Wizara hiyo itatumia sh milioni 567 kwa ajili ya mawasiliano, badala
ya milioni 71.76 ilizotumia katika mwaka wa fedha 2011/12, wakati katika
kile kilichoitwa Kitengo cha Utawala na Mawasiliano kitatumia sh
bilioni 2.003 badala ya sh milioni 53.87 za mwaka jana.
Nayo Wizara ya Fedha na Uchumi imejitengea sh milioni 582.3 kwa safari
za wakubwa za ndani, katika Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, wakati
mwaka jana ilitumia sh milioni 283, na safari za nje itatumia sh
milioni 874,wakati mwaka jana ilitumia sh milioni 532.Habari na http://www.freemedia.co.tz/daim
0 comments:
Post a Comment