Ibrahim Yamola
CHAMA Cha Madaktari
Tanzania (MAT) kimetangaza mgogoro na Serikali na kuipa wiki mbili
kuyapatia ufumbuzi matatizo yao la sivyo watafanya mgomo wa nchi nzima.
Wametoa msimamo huo walipokutana jana jijini Dar es Salaam ikiwa ni
siku chache baada ya ujumbe wao uliokuwa kwenye mazungumzo na Serikali
kugoma kusaini makubaliano kwa kile walichoeleza mpaka wapate ruksa ya
wanachama. Jana ilikuwa ni siku ya ujumbe huo kuwasilisha taarifa ya
makubaliano ambayo Serikali ilitaka waisaini na hivyo wanachama hao
hawakuyaridhia hivyo kuamua kutangaza mgogoro.
Habari
zilizoifikia Mwananchi Jumapili kutoka ndani ya kikao hicho cha ndani
zilieleza kuwa madai ambayo
Serikali imeshindwa kuyatekeleza ni nyongeza
ya mishahara, mazingira mazuri ya kazi, marupurupu, nyongeza ya posho
ya wito wa dharura, posho za nyumba na chanjo.
Mkutano huo
ambao uliwashirikisha madaktari pamoja na viongozi wa chama hicho
walikubaliana kutangaza mgogoro wa wiki mbili na baada ya hapo wataingia
katika mgomo ili kuishinikiza Serikali kuyapatia ufumbuzi madai yao.
Walidai
kuwa kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ilishindwa
kuyatatua matatizo yao kwa kigezo kwamba Serikali haina uwezo wa
kifedha.
“Hata kama Serikali ingekuwa na fedha isingeweza
kuongeza mishahara kama ambavyo tunataka kutokana na madai kwamba
itasababisha migogoro na watumishi wengine,” kilisema chanzo chetu
kutoka ndani ya mkutano huo wa madaktari.
Madaktari hao
walilalamika kwamba ahadi iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwenye
mkutano wao ya kuhakikisha madai yao yanashughulikiwa kikamilifu wakati
akiwataka warejee kazini baada ya mgomo waliofanya Januari mwaka huu,
haikutekelezwa.
“Haiwezekani Serikali imeshindwa kutatua
madai yetu hata moja na sisi tuendelee kukaa kazini hii ni dharau na
kitakachofanyika ni kurudi kama tulivyofanya awali na itakuwa zaidi ya
mgomo tulioufanya,” alisikika akilalamika mmoja wa wajumbe kwenye
mkutano huo.
Walielezea kushangazwa kwa tabia ya Serikali
kutotekeleza ahadi zake hadi pale watu wanapochukua hatua mbadala, kama
vile kuandamana na kugoma.
Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka
kutajwa jina lake alisema wamekubaliana waendelee kufanya migomo
kushinikiza kukubaliwa matatizo yao.
Walidai kuwa Serikali
imekuwa ikifanya kazi kwa mazoea na wakati mwingine ikiingiza siasa
katika masuala ya msingi kitu ambacho ni hatari kwa jamii na taifa kwa
ujumla.
Wanasema serikali imeshindiwa hata kuwapatia chanjo ya kuwakinga na maambukizo ya magonjwa mbalimbali wakiwa kazini.
“Serikali
kweli imeshindwa hata kutufanyia chanjo na kusema itafanya hivyo kwa
awamu huu ni uuaji kwani tunafanya kazi katika mazingira magumu, lakini
inashindwa kututhamini,” alilalamika daktari huyo. Walionya kuwa
Serikali isipokuwa sikivu kwa safari hii watafanya mgomo ambao utakuwa
mbaya kuliko ule uliofanyika awali na kusababisha taharuki kubwa kwenye
hospitali nchini hususan Muhimbili.
Hata hivyo, baadaye
Mjumbe wa MAT, Dk Godbless Charles aliwaambia waandishi wa habari kuwa
walichoamua wanachama katika mkutao wasio ni mrejesho wa tathmini ya
taarifa ambayo ilitolewa na Serikali baada ya kikao kilichofanyika Machi
31 mwaka huu.
“Sisi tumewapelekea na wao wakataka irudi
mezani na kupitiwa upya madai kabla ya wiki mbili na yawe yamepatiwa
ufumbuzi,” alisema Dk Charles.
Akielezea juu ya mazungumzo
yao alisema: “Tangu kamati hiyo ilipoundwa na Waziri Mkuu ili
kushughulikia madai yetu, tumekutana mara sita na mara zote tulishindwa
kufikia mwafaka. “Baada ya kurejesha taarifa ambazo hazikuwa na majibu
ndio maana tukaamua kuitisha kikao cha ndani ili wanachama waamue
wenyewe wasije kutuona tunawasaliti,” alisema.
Rais wa MAT,
Dk Namala Mkopi alikiri kwamba wanachama wamekubaliana kutangaza
mgogoro wa wiki mbili na serikali na baada ya hapo watapanga hatua za
kuchukua.”
Mgomo uliofanyika Januari mwaka huu ulisababisha
vifo kwa wananchi kwa kukosa huduma ambapo Waziri Mkuu Pinda
aliwasimamisha kazi mara moja Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni
na
Mganga Mkuu Dk Deo Mtasiwa. Madai mengine ya madaktari hao ilikuwa
ni kuwang’oa mawaziri jambo ambalo Rais Kikwete alilitekeleza kwa
kutowarejesha kwenye Baraza alilolisuka upya kwa kuteua wengine.
0 comments:
Post a Comment