Sunday, June 10, 2012

TIMU ya soka ya Tanzania, Kili Taifa Stars leo inawakaribisha Gambia katika mechi ya kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Dunia, wakitaka kushinda kupoza machungu ya kufungwa na Ivory Coast, Jumapili iliyopita.
Katika mechi hiyo iliyopigwa mjini Abidjan, Stars ilifungwa mabao 2-0, hivyo leo watakuwa na kibarua cha kusawazisha makosa kwa kushinda mechi hiyo ya pili katika kundi la C.

Hata hivyo, Stars inapaswa kucheza kwa tahadhari kubwa, kwani wakati ikitaka kushinda, Gambia nao watakuwa wakipigana kushinda kufikisha pointi nne.
Wakicheza kwenye uwanja wa nyumbani, Gambia walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Morocco.
Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen alisema jana kuwa, kikosi chake kipo fiti tayari kwa mechi ya leo, lakini akisikitishwa kukosa kanda (DVD) za wapinzani wao.
Poulsen alisema kitendo cha kukosa mikanda ya mechi za Gambia, kimesababisha kuwakabili wapinzani wao bila kuwafahamu vizuri kiuchezaji.

Alisema cha kusikitisha zaidi, ndivyo ilivyokuwa hata wakati wa kujiandaa na mechi iliyopita dhidi ya Ivory Coast, lakini akisema vijana wake watajitahidi kushinda mechi ya leo.
“Pamoja na kuzikosa DVD, nimekiandaa kikosi changu kuikabili Gambia, naamini vijana wangu watatumia vizuri uwanja wa nyumbani kushinda mabao mengi,” alisema.

Poulsen alisema, vijana wake wapo fiti kiufundi na kisaikolojia, isipokuwa Nurdin Bakari huku Haruna Moshi ‘Boban’ aliyekuwa majeruhi, hali yake ikiimarika na huenda akapangwa.
Naye Kocha wa Gambia, Luciano Machini, akizunngumza kwenye mazoezi ya timu yake juzi katika Uwanja wa Karume, alisema mechi itakuwa ngumu.
Stars iliyo nafasi ya 139 kwa ubora wa soka duniani, inakutana na Gambia iliyo nafasi ya 113, katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.

Mechi hiyo itakayochezeshwa na Ruzive Ruzive akisaidiwa na Salani Ncube na Edger Rumeck kutoka Zimbabwe, ni ya tatu kwa Stars chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Viingilio leo ni sh 3,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani; sh 5,000 (rangi ya chungwa); VIP C sh 10,000; VIP B sh 20,000 na VIP A ni sh 30,000.
Baada ya mechi ya leo, Stars itashuka dimbani kwa mara ya tatu katika kampeni hiyo Machi 21, mwakani kwa kuwakaribisha Morocco.

0 comments:

Post a Comment