Tuesday, June 19, 2012

Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa Riadha Tanzania (RT) na wadau wengine wa mchezo huo wawe wabunifu na kufanya jitihada za kufufua mchezo huo wakati serikali ikiendelea kutekeleza jukumu lake la kuwasaidia.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati alipokutana na viongozi wa RT na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

“Kama kuna kitu mnataka serikali isaidie, itawasaidia… lakini mchezo wa riadha kama michezo mingine, inahitaji juhudi za vilabu vya michezo yenyewe, na serikali inachangia tu lakini jukumu kubwa ni lenu,” alisema.

Aliwataka viongozi wa riadha waanze kwa kuelekeza juhudi zao katika ngazi za chini ambapo ndipo wanapoweza kuvitambua vipaji vya watoto, kuvikuza na hatimaye kuviendeleza.

Aliongeza kuwa ahadi yake ya kusaidia michezo iko palepale, ambapo yuko tayari kugharamia wakufunzi au walimu wa michezo mbalimbali nchini kwa ajili ya kukuza michezo.

Mbali na BMT na RT, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenela Mukangara na katibu mkuu wa wizara hiyo, Sethi Kamuhanda.

 

0 comments:

Post a Comment