Friday, June 8, 2012


Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa,
Wakati serikali inajiandaa kuwasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2012/13 bungeni wiki ijayo, wananchi na makundi mbalimbali nchini wametoa maoni kuhusiana na mambo wanayotaka yawemo katika bajeti hiyo.

Katika bajeti hiyo ambayo ni ya kwanza kusomwa na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, aliyechukua mikoba kutoka kwa Mustafa Mkulo tangu Mei 4, mwaka huu, serikali inapendekeza kutumia zaidi ya Sh. trilioni 15 kutoka Sh. trilioni 13.5 za bajeti ya mwaka huu unaomalizaka Juni 30.

TUCTA: KIMA CHA CHINI 200,000/-

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limesema matarajio yao katika bajeti hiyo ni mshahara wa kima cha chini kwa wafanyakazi wote wa serikali kupanda kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 200,000.

Naibu  Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Hezron Kaaya, alisema kuwa kiwango hicho cha mshahara ni kidogo na hakitatosheleza mahitaji ya wafanyakazi, lakini wameamua kuweka kiwango hicho kutokana na uwezo mdogo wa serikali.

“Msimamo wetu bado upo kwenye Sh. 315,000, lakini serikali ilituomba tupunguze kwa sababu haina uwezo wa kutupa kiwango hicho, tulikubaliana nao na tumepunguza hadi Sh. 200,000 japo bado ni ndogo sana kutosheleza mahitaji,” alisema Kaaya.

Kaaya alisema wanatarajia kodi ya mapato haitazidi asilimia kumi ili kupanua wigo wa walipa kodi na kupunguza mzigo wa wafanyakazi katika kulipa kodi kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Aidha, alisema wanatarajia kuwa misamaha ya kodi itapunguzwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu hawaoni haja ya misamaha kuwa katika kiwango kikubwa kama ilivyo sasa, huku akiitaka serikali kuja na mipango madhubuti na halisi ya kudhibiti mfumuko wa bei ili kuondoa hali ngumu ya maisha kwa wananchi.

“Hatutarajii kuongezeka kwa bei za bidhaa muhimu zinazogusa maisha ya kila siku ya Mtanzania hususani nishati kwa sababu zikipanda zinasababisha maisha magumu kwa wananchi na wafanyakazi wakiwemo,” alisema Kaaya.

Kaaya alisema wafanyakazi wa kawaida wapo katika hali ngumu ya maisha inayosababishwa na tabaka lililopo kati yao na wakubwa wachache na kwamba hawapo tayari kuvumilia tabaka hilo, hivyo iwapo bajeti hiyo haitakidhi matarajio yao watachukua hatua.

CWT: MUONGEZA ASILIMIA 100

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch, aliitaka serikali kuwa sikivu kwa kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 100 ili wayamudu maisha.
Alisema ili mwalimu ambaye ana watoto wanne amudu kula milo mitatu, anatakiwa kuwa na mshahara wa Sh 650,000 kwa mwezi.

“Hivi sasa mwalimu mshahara anaoupata unatosha kula milo mitatu kwa wiki moja tu, jambo hili halimuwezeshi mwalimu kufanya kazi yake kwa ufanisi kwa kuwa anakuwa anafikiria jinsi ya kufidia pengo, tunataka bajeti hii kuangalia suala la nyongeza ya mishahara kwa walimu,” alisema Oluoch.

Alisema hali hiyo pamoja na walimu kukosa posho ya kufundishia pamoja na ile ya mazingira magumu imewafanya walimu kukata tamaa.

MAFUTA TAA KODI CHINI

“Bajeti ijayo inatakiwa kuweka kipaumbele katika upunguzaji wa bei za pembejeo na kuangalia miundombinu ya usafishaji ili kusaidia kukuza uzalishaji wa vyakula katika maeneo mbalimbali,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, (Udom), Paul Loisulie.

Alisema kuwa pia kodi iliyoongezwa katika mafuta ya taa inatakiwa kuangaliwa upya kwa sababu imeyafanya mafuta hayo ambayo ni tegemeo kubwa kwa wananchi walio masikini kuwa kubwa na hivyo kushindwa kumudu kuyanunua.

Alisema mafuta hayo licha ya kutumika katika kupikia, lakini yamekuwa ni chanzo kikubwa cha mwanga katika maeneo ya vijijini hivyo suala la kupandisha kodi kwa ajili ya kuepuka uchakachuaji wa mafuta ya petroli linapaswa kuangaliwa upya.

Pia alisema suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu linatakiwa kuangaliwa upya ili kuwawezesha watoto wa masikini wanaochukua masomo ya sanaa kunufaika na elimu.

PAYE IWE ASILIMIA 10

Kuhusu kodi ya mishahara, Loisulie alisema kuwa kodi inayotozwa kwa wafanyakazi hivi sasa ni kubwa mno na hivyo serikali inapaswa kupunguza kodi hiyo angalau iwe chini ya asilimia 10.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda na Kilimo (TCCA), mkoani Dodoma, Faustine Mwakalinga, alitaka bajeti iangalie katika kufuatilia kodi kwa wafanyabiashara wakubwa kama wamiliki wa migodi badala ya kuendelea kuwabana watu wa chini.

Pia alitaka kodi inayopatikana katika mafuta ya taa itumike katika kupunguza mahitaji ya wakulima kwa kuhakikisha wanapata pembejeo zote kwa bei nafuu ili wazalishe kwa kiasi kikubwa.

EAC: IONDOE MAKALI YA MAISHA

Ofisa wa Bajeti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC), Stephen Mwilolezi, alisema: “Iwe ni bajeti itakayopunguza ukali wa maisha kwa kupunguza matumizi ya anasa serikalini.

“Serikali ifute kabisa ununuzi wa magari ya anasa kama ‘mashangingi’, ipunguze safari za nje kwa viongozi wa juu na pale ambapo ni lazima ipunguze msafara wakuwa na maofisa wengi ambao hawana umuhimu.

“Wafanyakazi watumie magari yao na serikali iwape fungu la mafuta tu,” alisema.

Mwilolezi alisema kipaumbele kiwe upatikanaji wa umeme wa uhakika na ujenzi wa barabara.
Alitaka serikali itafute masoko ya mazao ya shambani ambako Watanzania wengi wameajiajiri.

Pia alitaka uchumi usimamiwe kwa umakini zaidi na siyo kuacha ujiendeshe ovyo ovyo kama inavyoonekana kwa sasa.

Aidha, alitaka bajeti hiyo ielekee zaidi katika iongezayo ajira kwa Watanzania wengi ili kuinua vipato vyao na uchumi kwa ujumla.

WATU WA CHINI

Mwalimu mstaafu na mkazi wa Majengo Juum, Sakina jijini Arusha, Samwel Samson Mollel, alitaka bajeti hiyo iangalie zaidi watu wa chini kwa kuwawezesha ili waweze kuzalisha na hivyo kuchangia kulipa kodi serikalini.

Alitaja sekta ya kilimo kuwa serikali inaweza ikajikita kuwawezesha wananchi wake kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara na akataka iimarishe soko la mazao yao.

Waziri wa Elimu wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku) kilichoko mkoani Mbeya, Milanzi Petro, alisema ili bajeti ijayo iwanufaishe wananchi, ni lazima wizara zinazoigusa jamii moja kwa moja zipewe kipaumbele ili ziwe na uwezo wa kuwahudumia wananchi.

Alisema tatizo kubwa ambalo linawakabili wananchi wengi ni mfumko wa bei na ili kukabiliana na hali hiyo, kilimo kipewe kipaumbele kwa kuiwezesha kwa fedha Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika katika bajeti ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kupunguza bei za vyakula.

Aliongeza kuwa wizara nyingine inayostahili kupewa kutengewa bajeti kubwa ni ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili vijana wengi wapewe ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri wenyewe na hivyo kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

MIKAKATI MIPYA

Mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Chuo Kikuu Huria (OUT) Tawi la Mbeya, Eddo Mwamalala, alisema bajeti inapaswa kuja na mikakati madhubuti itakavyosaidia kupunguza na kudhibiti mfumuko wa bei.

Mkazi mwingine wa Soweto Jijini Mbeya, Angelica Sullusi, aliwataka wabunge kuwa na uzalendo wa hali ya juu wakati wa kujadili bajeti ili maaamuzi watakayofikia yasiwe ya kujutiwa na wananchi.

Mwenyekiti wa TCCIA, mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi, alisema matarajio ya walio wengi kuwa kati a bajeti ya mwaka serikali haitapandisha bei ya bidhaa ambazo kila mwaka imekuwa iliongezwa kama vinywaji na sigara.

“Tunataka kuona ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato, tuna madini na maliasili nyingine ambazo hazitozwi kodi ipasavyo, tunataka kuona mrahaba ukichukuliwa kwenye madini,” alisema.
Aidha, aliitaka serikali kupunguza matumizi kama ununuzi wa magari ya kifahari ambayo bei yake ni ndogo kuliko gharama za kuyatunza.

“Pia tunatarajia serikali itapunguza kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi 15 ili kuwa sawa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema ni vyema bajeti hiyo ikawa na mpango mahususi wa kujenga nyumba za walimu kwani idadi ya walimu inaongezeka, lakini hawana mahali pa kuishi kwenye shule za kata, hivyo kuwaweka katika mazingira magumu.

YALE YALE

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kuwa bajeti ijayo haiwezi kukidhi matakwa na matarajio ya wananchi walio wengi.

Alisema bajeti ya 2011/12 ilikuwa na vipaumbele vingi na vya msingi, hivyo ingekuwa vyema bajeti hiyo ingeimarisha tu vipaumbele hivyo, kwani bajeti iliyopita ilisifiwa na watu wengi pamoja na kuwa serikali ilishindwa kuvitekeleza kama ilivyokuwa imeviainisha.

“Nafikiri bajeti hii haiwezi kukidhi matakwa ya wananchi, nilitegemea kwamba ingeimarisha vipaumbele vya mwaka jana, ambayo tuliisifia sana na ambayo ilikuwa na vipaumbele vingi,” alisema.

Dk. Bana aliishauri serikali kuongeza vyanzo vipya vya kodi pamoja na mapato na kupunguza matumizi yote yasiyo ya lazima kama vile matumizi ya magari ya anasa na kuweka utaratibu wa viongozi na wafanyakazi wa serikali kutumia magari ya kawaida.

“Ni vyema serikali ikapunguza matumizi ya magari ya anasa, utakuta kiongozi mmoja anatumia magari kadhaa, hii ni kuiongezea mzigo serikali, ambao siyo wa lazima, kwa nini wasitumie magari yao binafsi?,” alihoji Dk. Bana.

VYANZO VIPYA

Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini-Iringa, Adrian Ndunguru, alipendekeza kuwa katika bajeti ijayo ni vizuri serikali ikajielekeza kutafuta vyanzo vipya vya kodi kwa ajili ya kuendeshea matumizi ya serikali.

 “Ni vizuri bajeti ijayo ikaziba mianya ya ubovu wa bajeti zilizopita ambazo hazikuwa na tija kwa umma, serikali ije na mpango mpya wa kutafuta fedha kutoka katika vyanzo mbadala vya kuendeshea matumizi ya serikali …Tunaumia kwa sababu matokeo ya kodi hayaonekani kwenye maisha ya mtu mmoja mmoja kwa sababu fedha zinazopatikana zinatumika kuendeshea matumizi makubwa ya serikali,” alisema Ndunguru.

 Alizitaja sekta zinazopaswa kuwa kipaumbele kwa sasa kuwa ni afya, kilimo, maji, barabara na sekta ya elimu ambayo inatakiwa kutiliwa mkazo zaidi katika masomo ya sayansi ili kuliokoa taifa na aibu ya kukosa wataalamu.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Frank Mwaisumbe, alisema kuwa bajeti inapaswa kujibu matatizo ya kiuchumi yanalolikabili taifa kwa sasa, ikiwamo mfumuko wa bei.

 MATATIZO YA WANAFUNZI


Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Mauna Chuma, aliitaka serikali kuja na bajeti yenye tija kwa umma ikijibu matatizo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.

Mhitimu wa Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Aman Mwaipaja, alisema anategemea bajeti hiyo itaweza kupunguza kodi ya mafuta ili kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa.

Alisema bajeti hiyo pia inapaswa kuelekeza fedha zake katika maendeleo ya vijiji kwa kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, kilimo na elimu ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Dk. Cravery  Tungaraza, alisema anategemea bajeti hiyo itasaidia zaidi wananchi wa kipato cha chini kwa kuwaondolea mambo mbalimbali yanochangia kuongezeka kwa gharama za maisha hususani mfumuko wa bei.

KIPAUMBELE KILIMO NA ELIMU

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Waislam cha Morogoro, Ally Sarehe, alisema katika bajeti hiyo lazima serikali ihakikishe inatoa kipaumbele kwa elimu na kilimo kwa kuwa ni sekta zinazochangia katika utoaji wa ajira.

ASKOFU MUNGA: UMAKINI UTAWALE

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk. Steven Munga, alisema kuwa ni ukweli usiopingika kwamba serikali hutegemea mapato kuinua uchumi wa nchi kutokana na makusanyo yake ya kodi, lakini ni dhahiri kuwa kodi hiyo imekuwa ikichangiwa na wanyonge kuliko wafanyabiashara wakubwa.

Askofu huyo pia alilalamikia kukosekana kwa umakini wa serikali katika usimamizi mzuri wa bajeti na kutoa angalizo kuwa bila usimamizi itakuwa vigumu kufikia maendeleo.

Kuhusu misamaha ya kodi kwa mashirika na taasisi za dini, alisema kuwa msamaha huo ni nadharia tu na siyo kwa vitendo kwani wamekuwa wakilazimika kutumia gharama zao binafsi ili kuepuka usumbufu unaojitokeza.

Alisema hatua hiyo inatokana na usimamizi mbovu na mapungufu makubwa katika wa sera na sheria zilizopo bila kujali kuwa Taasisi za dini hapa nchini zimekuwa mstari wa mbele katika kuchangia shughuli za maendeleo kwenye sekta mbalimbali hapa nchini.

Dk. Munga alisema inashangaza kuona kuwa makampuni makubwa hapa nchini hususan yale ya madini yakijipangia yenyewe kiwango cha kulipa kodi, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu wa kisheria.

SHILINGI ISHUGHULIKIWE

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Eckenford (ETU) cha jijini Tanga, Jonas Kitutu, alisema ni vyema serikali sasa ikaanza kushughulikia tatizo la kuporomoka kwa Shilingi kwa lengo la kukabiliana na mtikisiko wa kiuchumi duniani.

Kitutu alisema kuwa kuongeza mishahara siyo suluhu ya kuboresha maisha ya wananchi kwani serikali inapaswa kujizatiti katika kuhakikisha nchi inakuwa na uchumi imara unaotokana na kukua kwa pato la Taifa.

IPUNGUZE VIFO


Magreth Minja, mwanafunzi wa OUT mjini Tanga, alisema bajeti ya kila mwaka haijalenga viashiria vikuu vya umaskini hususan kupunguza vifo vya akina mama na watoto, upatikanaji wa maji safi na salama, barabara nzuri hasa vijijini na kuboresha huduma  za afya na elimu.

Alisema kutokana na hali hiyo, bajeti ijayo hainabudi kujikita katika kutekeleza malengo ya Mpango wa Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa dhati.

Imeandikwa na Emmanuel Lengwa, Mbeya; Salome Kitomari, Moshi; Sharon Sauwa, Dodoma; John Ngunge, Arusha; Godfrey Mushi, Iringa; Ninael Masaki na Samson Fridolin, Dar; Lulu George, Tanga na Ashton Balaigwa, Morogoro. CHANZO GAZETI LA NIPASHE

0 comments:

Post a Comment