Vita ya Lowassa,CCM yaibuka upya
MKAMA AMJIBU,ASEMA KAULI YAKE SI SAHIHI,ASHUGHULIKIE KWANZA MATATIZO YA JIMBO LAKE
Patricia Kimelemeta na Fidelis Butahe
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM), kimemjibu Mbunge wa Monduli,Edward Lowassa kwa kumtaka azungumzie matatizo yanayolikabili jimbo lake badala ya kufanya mikutano ya hadhara kukiponda chama hicho huku akisahau kwamba yeye ni miongoni mwa mwanachama.
Kauli hiyo ya CCM imekuja siku moja baada ya mbunge huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya awamu ya nne kabla ya kujiuzulu kwa kashfa ya mkataba wa kampuni hewa ya kufua umeme ya Richmond, Februari 2008, kudai kuwa tatizo la CCM liko katika uongozi na utendaji na kwamba kitendo cha viongozi kushindwa kushughulikia kero, ndio mwanzo wa chama hicho kuparaganyika kwa kuwa watu wanatafuta mbadala wa kero zao na matatizo yao.
Akizungumza na gazeti Mwananchi kwa njia ya simu jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alisema si sahihi kwa Lowassa kutoa kauli hiyo kwenye mikutano ya hadhara wakati anajua bayana taratibu za chama hicho.
Alisema Lowassa alipaswa kuzungumzia matatizo ya jimbo lake yakiwemo migogoro ya ardhi, wawekezaji na wananchi, wakulima na wafugaji,maji na kero nyingine mbalimbali na si kukishambulia CCM.
Alisisitiza kuwa kama Lowassa amebaini matatizo ya uongozi ndani ya CCM, alipaswa kuyazungumzia ndani ya vikao vya chama kwa sababu ana mamlaka ya kukosoa au kurekebisha, lakini si kwenda kwenye mikutano hiyo na kuanza kutoa kasoro wakati bado yumo ndani ya chama na ameshika nyadhifa mbalimbali.
“Tunamshangaa Lowassa kukaa kwenye mikutano ya hadhara na kuanza kukiponda chama, amejidhalilisha mwenyewe, kwa sababu aliwahi kuwa kiongozi mkubwa ndani ya chama na serikalini, lakini ameshindwa kutatua kero mbalimbali zinazoikabili nchi na jimbo lake pia, leo anakaa na kujadili matatizo ya chama kiutendaji wakati bado ni mwanachama na kwamba ana mamlaka ya kukikosoa kwenye vikao halali,”alisema Mukama.
Aliongeza kuwa mpaka sasa jimbo lake linakabiliwa na kero mbalimbali hivyo alipaswa kuwaambia wapigakura wake, ni kwa kiasi gani amezishughulikia tangu aanze kuliongoza.
Alisema Lowassa mpaka sasa bado ni mwanachama wa CCM, na kwamba ni miongoni mwa viongozi wanaohudhuria vikao mbalimbali vya chama, hivyo alipaswa kutumia vikao hivyo na si kupanda majukwaani, kujisafisha mbele ya wananchi ili aonekane mtetezi wa rasilimali za umma.
Alisema hatua hiyo ya Lowassa ni kukurupuka kwani kama moja ya viongozi wa chama hicho, ana wajibu na jukumu la kutatua migogoro iliyopo ndani ya chama na hata kuishauri Serikali.
“Amewahi kuwa Waziri Mkuu, ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama na Serikali, na kwamba bado ni mwanachama wa CCM, hivyo na yeye ni miongoni mwa watu wanaopaswa kutatua matatizo iwe ya kichama au kuishauri Serikali iliyopo madarakani ambayo ni ya chama chake. Hawezi kukurupuka, anapaswa kuwa na hekima na kukaa na wenzake kwa ajili ya kujadili matatizo yaliyopo ili yaweze kutatuliwa, si kama alivyofanya,”alisisitiza Mukama.
Alisema mbali na hilo, alipaswa kuweka wazi matatizo ya uongozi aliyokuwa akiyazungumzia kuwa yapo katika ngazi ipi ya kata, wilaya, mkoa au taifa, badala ya kuishia kusema kuna matatizo ya kiutendaji na uongozi ndani ya chama.
Kauli ya Lowassa
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mto wa mbu Arusha wiki hii, Lowassa aliwaambia wananchi kuwa CCM inakabiliwa na matatizo ya kiutendaji na uongozi lakini kuna mambo matano yanayomfanya aendee kuwa mwanachama wa chama hicho.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni muundo mzuri wa chama, kutetea wanyonge, kudumisha umoja na mshikamano, kuwalinda raia wa kawaida katika kupata na kufaidi rasilimali za nchi dhidi ya matajiri na wawekezaji wa nje na mfumo mzuri unaowezesha watu kujisahihisha.
Lowassa alikaririwa akisema CCM itakapoacha misingi yake ya awali ikiwemo kutetea wanyonge, hatakuwa mmoja wa wanachama wake.
“Pamoja na uzuri wake, muundo wa chama chetu ni mzuri sana, imani ya chama chetu ni nzuri sana ,misingi inayoongoza chama chetu ni mizuri sana , lakini tuna tatizo la utendaji na uongozi ndani ya chama chetu” alisema Lowassa na kuongeza;
“…ama katika kufanya uamuzi ama uamuzi usio sahihi au kutochukua hatua kwa matatizo yanayowakabili wananchi kwa wakati muafaka.
Lowassa alisema matatizo hayo ndiyo yanayowafanya watu wakichukie chama hicho na kukiona kuwa ni kero na kuanza kutafuta mbadala wake.
“Tukionekana hatujali shida za wananchi wetu, watatafuta mbadala , lakini kero hizi zishughulikiwe kwenye vikao,” alisema.
Kauli hiyo ya Lowassa ilikuja saa chache baada ya kukutana na kundi la vijana makada wa CCM wilayani Monduli ambao walimshinikiza atoe msimamo wake kwa madai kwamba amekuwa akiandamwa na kuonewa ndani ya chama hicho huku wakimtaka ahamie Chadema.
Vijana hao walimhakikishia kuwa wataendelea kumuunga mkono mbunge huyo na kuwa naye sambamba kwa uamuzi wowote atakaouchukua hata kama ni kuhamia kambi ya upinzani.
Hata hivyo Lowassa aliwajibu vijana hao kuwa si sahihi kukihama CCM kwa sasa na kuwaomba wawe watulivu na kutumia vikao halali vya chama kujadili na kutafuta ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinazokikabili chama hicho.
0 comments:
Post a Comment