Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye.
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imejadili kwa kina suala la kupanda kwa
gharama za maisha nchini. NEC inakiri kwamba ni kweli lipo tatizo la
kupanda kwa gharama za maisha nchini.Tatizo hili pia limezikumba karibu nchi nyingi za Afrika Mashariki na kwakweli karibu sasa lipo dunia nzima.
Baadhi ya sababu za kupanda kwa gharama za maisha hapa nchini ni pamoja na;
1. Hali mbaya ya mavuno inayotokana na uhaba wa mvua au mvua kunyesha kipindi cha nje ya msimu katika maeneo mengi nchini.
2. Kuongezeka kwa bei ya mafuta duniani, hivyo kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa bidhaa na usafirishaji wa mazao.
3. Kuyumba kwa thamani ya dola ya Marekani.
4. Kuwepo kwa soko huria ambapo sasa mazao ya chakula yanapata soko nje ya nchi, na wakati mwingine kuuzwa nje kwa njia ya magendo na hivyo kusababisha uwepo wa ukubwa wa mahitaji na hivyo kuongezeka kwa bei ya chakula nchini.
5. kuongezeka kwa walaji wakati uzalishaji ukiwa mdogo.
6. kutofanikiwa (ikiwemo kuhujumiwa na wafanyabiashara wasio waaminifu) kwa baadhi ya mikakati ya kudhibiti mfumko wa bei.
Uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
1. Pamoja na Serikali kuendelea kuchukua hatua za muda mrefu na wa kati za kukabiliana na tatizo hili, CCM inaiagiza Serikali kuchukua hatua za haraka za muda mfupi ikiwemo kuangalia upya baadhi ya kodi katika vyakula pamoja na kodi ya ongezeko la thamani VAT katika sukari.
2. Utaratibu wa ruzuku ya mbegu na mbolea upanuliwe ili kunufaisha wakulima wengi.
3. Serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa mpango wake wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula nchini, hasa kwa kupitia Hifadhi ya Nafaka ya Taifa, ikiwa ni pamoja na kujenga maghala zaidi ya mazao ya chakula katika maeneo ya uzalishaji wa mazao, na kutenga fedha nyingi zaidi kwa ununuzi wa mazao hayo. Pamoja na hili, mipango ifanywe kuongeza uwezo wa wakulima kuhifadhi chakula chao wenyewe na kupunguza upotevu baada ya mavuno (post-harvest losses).
3. Serikali iendelee kupanua utaratibu wake wa kutumia Hifadhi ya Nafaka ya Taifa (SGR) kama nyenzo ya kudhibiti kupanda kwa bei za vyakula. Wakati wa uhaba wa vyakula katika maeneo ya mijini, kasi ya kupeleka chakula maeneo hayo iongezwe na utaratibu mzuri zaidi wa usambazaji wa chakula utumike ili walaji, na sio wasafirishaji na wasindikaji, wanufaike.
4. Serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kilimo nchini, hasa ASDP na SAGCOT, ambayo itasaidia kumaliza tatizo la chakula nchini na kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania walio wengi.
5. Serikali idhibiti malipo ya huduma ya ndani kwa kutumia fedha za kigeni, hasa dola za kimarekani. Aidha, Serikali iongeze udhibiti wa Maduka na mahoteli yanayofanya biashara ya fedha za kigeni ili kuondoa hujuma kwa uchumi wa nchi inayofanywa kutokana na uhuru uliokithiri katika biashara hii.
6. Waajiri wahimizwe kupandisha mishahara na malipo mengineyo kwa wafanyakazi wao ili waweze kumudu gharama za maisha.
7. Serikali iweke jitihada zaidi za kudhibiti ulanguzi wa bidhaa muhimu na upandishaji holela wa bei za vyakula, kodi za nyumba na usafiri.
Imetolewa na:
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
15/05/2012
0 comments:
Post a Comment