Thursday, May 31, 2012

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbroad Slaa amemtaka Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia kuacha kutisha na kuwakamata wananchi wanaomuuliza maswali katika mikutano ya hadhara akidai amekashifiwa.
Akihutubia umati wa wananchi katika Kata ya Mtimbwilimbwi na Nanyamba, Slaa alisema ni uvunjaji wa sheria na ubabe kukamata wananchi waliowapigia kura.
Slaa alisema hayo baada ya wananchi kumwelezea kuwa, wamekuwa wakikamatwa na viongozi wa serikali na CCM wanapouliza maswali, ndiyo maana wameingiwa woga.
Alisema Ghasia ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), anafanya vitendo hivyo kwa kuwa ana uhakika wa kutogombea tena ubunge katika Jimbo la Mtwara Vijijini baada ya kutambua kuwa hawezi tena kushinda.
Slaa alisema maisha ya wakazi wa Mtwara Vijijini na umasikini unaowazunguka, ni aibu kwa uongozi katika miaka 50 ya uhuru, ambapo wajawazito wanalazimika kwenda hospitali wakiwa na vifaa.
“Enzi za Mwalimu Nyerere hakukuwa na suala hilo, leo hata mtoto mdogo anajua kuwa mama yake anakaribia kujifungua kwa kuwa ni lazima atakuwa anahangaika kutafuta vifaa vya kujifungulia,” alisema Dk. Slaa.
Alibainisha kuwa, Jimbo la Karatu ambalo wananchi wake hawakuwahi kuwa na waziri kwa miaka 15 sasa, wanafikiria kuingiza maji ndani ya nyumba zao wakati Mtwara Vijijini ambayo mbunge wake ni waziri, wananchi wanatafuta maji umbali wa zaidi ya kilometa 10.Katika hatua iliyoonesha kukithiri kwa umasikini, Dk. Slaa alilishwa supu ya ngozi ya ng’ombe kama kitoweo, ambapo wananchi walidai wamefanya hivyo kwa kuwa hawana uwezo wa kununua nyama.
Walisema hata hizo ngozi ni lazima aende mtu kuzifuata Mtwara mjini na siku inapokosekana wanajihesabia kama wamekosa nyama halisi.
Kufuatia hali hiyo, Dk. Slaa aliwataka wananchi wa Mtwara mjini kujiepusha na kuuza uhuru wao kwa gharama ya shilingi elfu tano na badala yake wasimamie ukombozi wa kweli.
MBOWE KUMBANA WAZIRI MKUU
Akizungumza katika mikutano aliyoifanya katika kata za Madimba na Tangazo, Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema kuanzia sasa atakuwa msemaji wa wakazi wa Mkoa wa Mtwara kwa kuwa hawana msemaji wa shida zao hususan kuhusu zao la korosho na gesi.
Alisema akifika bungeni swali lake la kwanza kwa waziri mkuu ni kumuuliza Serikali ya CCM inatumia sera gani kuchimba gesi katika Mkoa wa Mtwara.
Mbowe alishangazwa na kitendo cha serikali kuweka nguzo za umeme katika maeneo yenye nyumba za nyasi, na kukiita kitendo hicho kama dharau, na kwamba ilipaswa kwanza kuhakikisha wananchi wake wana nyumba bora.
WENJE AMVAA MBATIA
Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA) amemshambulia Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia akidai amefungishwa ndoa ya mkeka na CCM, kwa kupewa ubunge wa viti maalum na Rais Jakaya Kikwete ili kumsaidia kutekekeza ilani isiyotekelezeka.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Majengo katikati ya mji wa Mtwara juzi, Wenje alisema kitendo cha Mbatia kukubali ubunge wa viti maalumu, kimeonesha udhaifu wake mkubwa, kwamba si mpinzani wa kweli wa kupinga ufisadi na ubadhirifu unaofanywa na Serikali ya CCM.
Hatua hiyo ya Wenje kumuita Mbatia mbunge wa viti maalumu, iliibua mvutano katika mkutano huo baada ya makundi ya watu kutofautiana, wengine wakisema hata CHADEMA kuna wabunge wa viti maalumu.
Kutokana na mabishano hayo, ilimlazimu Wenje mwisho wa mkutano kutoa ufafanuzi jinsi wabunge wa viti maalumu wa chama wanavyopatikana na wabunge wanaoteuliwa na rais kwa mujibu wa mamlaka ya ibara ya 66 (1) (a) ya katiba ya nchi.
“Ndugu zangu hakuna sababu ya kubishana hapa, wapo wabunge wa viti maalumu wa chama husika wanaotokana na idadi ya wabunge halali waliochaguliwa kwa kura za wananchi, na wapo wabunge wa kuteuliwa na rais kwa mujibu wa kifungu hicho, wote ni wabunge, lakini tofauti yao ni huyu ni wa rais na huyu ni wa wananchi.
chanzo cha habari hii ni : http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36475

0 comments:

Post a Comment