0digg
MABALOZI WAGOMA KUCHUKUA FOMU KUOMBA UONGOZI, WASOMI WAIONYANa Waandishi wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemaliza uchaguzi katika ngazi ya mashina na matawi huku kikikabiliwa na tatizo la kupata wagombea nafasi ya mabalozi wa nyumba kumi katika maeneo mbalimbali nchini.Uchunguzi wa gazeti hili katika mikoa mbalimbali, umebaini kuwa makada wengi wa CCM walikwepa kugombea nafasi hiyo jambo lililofanya walazimishane na kuleta wakati mgumu kupata warithi.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, mabalozi au wajumbe wa shina ndio ngazi ya kwanza ya uongozi ndani ya chama hicho pia ni kiungo muhimu kati ya chama na wananchi katika maeneo wanayoishi.
Mbali ya majukumu mengine, mabalozi wa nyumba kumi wamekuwa wahamasishaji wakuu wa chama katika maeneo yao, kuhakikisha wanachama wanajiandikisha kwenda kupiga kura pia kujua idadi yao kwenye eneo husika.
Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Augustino Mbogo, amekiri kuwa kazi ya kuchagua mabalozi wa nyumba kumi iliingia dosari na kufanya baadhi ya watu kususa.
Hata hivyo, aliwarushia lawama baadhi ya watendaji ndani ya chama hicho kwa ngazi ya Kata na Matawi kuwa walikuwa kikwazo cha kukwamisha mchakato huo na kuwafanya baadhi ya wanachama kususa.
Mbogo alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akielezea namna mchakato wa uchaguzi ndani ya chama unavyoendelea, ikiwemo uchaguzi wa ngazi ya mashina ambao umefikia kilele hivi karibuni.
Alisema kuwa katika wilaya yake, yako maeneo ambayo viongozi walitoa taarifa kuwa mabalozi walikuwa wakikataa kugombea na maeneo mengine waliamua kupeana nafasi hizo bila kufuata taratibu zozote.
“Ni kweli kuna baadhi ya maeneo hali haikuwa nzuri, mfano Kata za Chihanga,Hombolo na Mtumba tumepata wakati mgumu watu waligoma kugombea nafasi hizo,’’alisema Mbogo.
Kiongozi huyo alibainisha sababu za wanachama kugomea kugombea nafasi hizo ambapo alisema ni kutokana na ukiritimba mkubwa uliokuwa ukifanywa na baadhi ya makatibu wa maeneo husika.
“Unajua wale viongozi wa ngazi ya chini ni watu wa kuchaguliwa, hivyo katika maeneo mengi walikuwa wakipanga safu zao ili kujijenga na kuwa na mtaji wa wapiga kura pindi watakapoanza kugombea na wao,’’alisema.
Alitolea mfano kuwa baadhi ya maeneo fomu za kugombea nafasi hizo za mashina zilikuwa zikiuzwa kati ya Sh 5000 hadi 10,000 kinyume na utaratibu jambo lililofanya baadhi ya watu kushindwa kuzinunua.
Wakati Katibu huyo akieleza mchakato huo, uchunguzi uliofanywa katika baadhi ya maeneo umebainisha kuwa kwa baadhi ya sehemu, nafasi hizo hazikutangazwa kabisa,hivyo kufanya mabalozi waliokuwa madarakani waendelee kuongoza hata kama muda umepita.
Kata za Nzuguni, Iyumbu, Makutupora pamoja na maeneo ya Mpunguzi, Zuzu na maeneo kadhaa ya mjini Dodoma, uchaguzi huo haukufanyika na wengi hawajui kama mwaka huu ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi kwa mabalozi.
Kamati ya siasa Arusha yakutana
Uchaguzi wa Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa mashina, matawi na mabalozi katika wilaya tano za mkoa wa Arusha, umeelezwa kudorora kwa kiasi kikubwa mwaka huu, huku wilaya za Arusha mjini na Arumeru zikishindwa kabisa kufanya uchaguzi wa matawi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya chama hicho, ambazo zimethibitishwa na Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare, zimebainisha kuwa, kudorora kwa chaguzi hizo kumesababisha na sababu mbali mbali ikiwepo hali ya kisiasa mkoani Arusha.
Sababu nyingine zilizotajwa na baadhi ya viongozi wa CCM wa wilaya mkoani hapa, ni pamoja na kukosekana wagombea, na hivyo viongozi waliopo kuendelea kushikilia nafasi zao na kushindwa kusimamiwa zoezi la uchukuaji fomu, kurejeshwa na kupitisha majina kutokana na viongozi wengi kushiriki katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, uchaguzi wa matawi katika wilaya hasa za Arusha na Arumeru hadi jana ulikuwa haujafanyika, wakati uchaguzi wa mashina na mabalozi pia haujafanyika kwani wengi wa mabalozi, wameendelea na nafasi zao.
"Unajua mwaka huu, hapa Arusha tulikuwa na uchaguzi wa Arumeru kuanzia Januari hadi Aprili viongozi wengi walikuwa huko, hivyo ilishindikana uratibu wa chaguzi,"alisema kiongozi huyo.
Hata hivyo, alisema katika wilaya nyingine za Longido, Monduli, Karatu na Ngorongoro, uchaguzi wa ngazi za Mashina na matawi zimefanyika kwa wastani wa asilimia 80 tu.
Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Siasa Mkoa wa Arusha, ilitarajiwa kukutana jana kupokea taarifa za chaguzi hizo na kujua uhai wa chama katika wilaya zote.
Sanare alisema katika kikao hicho, kila wilaya itakuwa na ripoti yake ya chaguzi, hivyo kujulikana taarifa sahihi ni maeneo gani hazijafanyika na sababu zake, pia hatua ambazo zitachukuliwa.
"Naomba usubiri mara baada ya kikao cha Kamati ya Siasa tutakuwa na taarifa kamili ya chaguzi hizo na hali ya kisiasa ya mkoa wetu,"alisema Sanare.
Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa ambayo hali ya kisiasa imekuwa tete kwa CCM hasa kutokana na viongozi wake na makada kadhaa kujiengua na kujiunga na chadema.
Kinondoni
Akizungumza jana Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Aron Mwaikambo alisema chaguzi zilizo tayari ni za jumuiya pamoja na chama ngazi ya ubalozi na matawi.
Mwaikambo alisema, ubalozi wa nyumba kumi tangu Februari mwaka huu ila hapakuwa na upinzani kwa sababu sehemu nyingi ni mtu mmoja tu alijitokeza kugombea, hivyo kushinda bila upinzani.
“Tulifanya uchaguzi wa nyumba kumi kuanzia Februari 2 hadi 5 mwaka huu tukamaliza zoezi hilo na tulipenda kungekuwepo na upinzani ila watu walikua wachache na katika kila eneo la hizo nyumba kumi aliyechukua fomu ndio mshindi kwasababu hapakua na upinzani kabisa”alisema Mwaikambo.Alieleza:
Sehemu nyingi wazee wamechoka hivyo wamewaachia vijana nafasi hiyo lakini asilimia kubwa ya vijana hawakujitokeza kwani licha ya balozi kuwa anatekeleza kazi za chama, pia ana jukuma la kupatanisha migogoro inayotokea katika nyumba hizo hasa familia ambapo kwa vijana inakua ngumu.
Temeke
Wakati hayo yakiendelea Kinondoni Msemaji wa CCM Wilaya ya Temeke, Saad Kusilawe amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimepata watu wengi waliojitokeza kuchukua fomu za ubalozi wa nyumba kumi katika kata zake zote.
Akizungumza jana ofisini kwake, alisema hali ilikuwa tofauti na alivyofikiria kwani waliojitokeza ni wengi tofauti na kipindi cha nyuma kulikuwa na wanachama wapatao 5,228 na katika kipindi hiki waliokuja kuchukuwa fomu hizo wamefikia 7,800 hali ambayo inaonyesha kuwa chama hicho bado kipo imara.
Kusilawe alisema hali ya siasa ina changamoto hasa kipindi hiki ambacho vijana wengi wamejikita katika suala la siasa na kupelekea mambo kubadilika kutokana na kujitambua kwao.
“kwakweli vijana wamekuja juu sana kipindi hiki ila kinachoniogopesha ni kuhusu kuja kwao juu ni kwa kuchochewa na baadhi ya wanasiasa kufanya fujo na siyo kujenga nchi kama inavyofikiriwa”alisema kusilawe.
Aliongeza kuwa vijana wengi hivi sasa wamekaa kiushawishi na mara nyingi uacha mambo yanayowapeleka shule na kuanza kufanya siasa ambayo mara nyingi inakuwa ni hasara kwao kutokana na fujo wanazo zianzisha.
Dodoma
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Mjini, Augustino Mbogo amekiri kuwa kazi ya kuchagua mabalozi wa nyumba kumi iliingia dosari na kufanya baadhi ya watu kususa.
Hata hivyo, aliwarushia lawama baadhi ya watendaji ndani ya chama hicho kwa ngazi ya Kata na Matawi kuwa walikuwa ni kikwazo cha kukwamisha mchakato huo na kuwafanya baadhi ya watu kususia.
Mbogo alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akielezea namna mchakato wa uchaguzi ndani ya chama unavyoendelea ikiwemo uchaguzi wa ngazi ya mashina ambao umefikia kilele mwishoni mwa wiki.
Alisema kuwa katika wilaya yake yako maeneo ambayo viongozi walitoa taarifa kuwa mabalozi walikuwa wakikataa kugombea na maeneo mengine waliamua kupeana nafasi hizo bila kufuata taratibu zozote.
“Ni kweli kuna baadhi ya maeneo hali haikuwa nzuri, mfano Kata za Chihanga, Hombolo na Mtumba tumepata wakati mgumu watu waligoma kugombea nafasi hizo,’’alisema Mbogo.
Kiongozi huyo alibainisha sababu za wanachama kugomea kugombea nafasi hizo ambapo, alisema ni kutokana na ukiritimba mkubwa uliokuwa ukifanywa na baadhi ya makatibu wa maeneo husika.
“Unajua wale viongozi wa ngazi ya chini ni watu wa kuchaguliwa, hivyo katika maeneo mengi walikuwa wakipanga safu zao ili kujijenga na kuwa na mtaji wa wapiga kura pindi watakapoanza kugombea na wao,’’alisema.
Alitolea mfano kuwa baadhi ya maeneo fomu za kugombea nafasi hizo za mashina zilikuwa zikiuzwa kati ya Sh 5000 hadi 10,000 kinyume na utaratibu jambo lililofanya baadhi ya watu kushindwa kuzinunua.
Wakati Katibu huyo akieleza mchakato huo, uchunguzi uliofanywa katika baadhi ya maeneo umebainisha kuwa katika maeneo mengi nafasi hizo hazikutangazwa kabisa, hivyo kufanya mabalozi waliokuwa madarakani waendelee kuongoza hata kama muda umepita.
Hofu ya kutotangaza inatokana na ukweli kuwa baadhi ya mabalozi hawapendi kuendelea kuongoza na hivyo kama nafasi hizo zingetangazwa, ni wazi kuwa wangeweza kuziachia huku chama kikikosa mgombea katika eneo husika.
Kata za Nzuguni, Iyumbu, Makutupora pamoja na maeneo ya Mpunguzi,Zuzu na maeneo kadhaa ya mjini Dodoma, uchaguzi huo haukufanyika na wengi hawajui kama mwaka huu ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi kwa mabalozi.
Mara
Uchaguzi ngazi ya mashina na matawi ya ya CCM umeshindwa kufanyika katika maeneo mbalimbali wilayani Serengeti ,kutokana na wanachama wengi kususa kujitokeza, hali iliyosababisha watu wateuliwe kushika ubalozi kinyume na utaratibu wa kawaida wa chama wa kupigiwa kura.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili ulibaini kuwa nafasi nyingi za ubalozi wa mashina zimekimbiwa na wanachama wa CCM na sasa waliotayari wanateuliwa kujaza nafasi hizo.
“Hii ni aibu kubwa na haijawahi kutokea maana ilipofika kipindi hiki cha uchaguzi, watu walifukuzana kuwania ubalozi
,lakini leo mtu akionekana anachukua fomu ya ubalozi watu wanamzoea, hakika chama kinakwenda pabaya,”alisema Katibu mmoja wa Tawi la CCM, jina limehifadhiwa.
Katika Kata ya Manchira, mbali na uteuzi wa mabalozi na wengine kukataa uteuzi hata uchaguzi wa viongozi ngazi ya tawi uliokuwa ufanyike mwishoni mwa wiki hii ulishindikana baada ya wanachama wakiwemo waliochukua fomu, kutojitokeza.
Habari za uhakika na zilizothibitishwa na baadhi ya viongozi wa matawi na Kata wa chama hicho, zinadai katika Tawi la Rwamchanga, walijitokeza watu wasiozidi wanane, hali iliyomlazimisha Katibu wa Uchumi wa Kata hiyo, John Wambura ambaye alikuwa msimamizi, kuahirisha hadi Mei 21 mwaka huu.
Hali hiyo pia iliyakumba matawi ya Ntamyo,Miserere na Miseke
ambapo wanachama hawakujitokeza hata waliojaza fomu za kuwania nafasi mbalimbali ,huku kukiwa na uvumi kuwa wana mpango wa kujiungua Chadema na wanasubiri viongozi wa kitaifa wahame.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Patrick Chandi alikiri kuwepo kwa migogoro baadhi ya maeneo ambapo amelazimika kumwagiza Katibu wake wa wilaya kufuatilia chanzo cha matatizo.
“Kwa ujumla tunaendelea ingawa kuna mambo hayawezi kwenda sawa sawa.
Maeneo kama Rwamchanga,Tamukeri ,Kisaka na kwingineko kuna migogoro ya ndani kwa ndani,”alisema.
CCM yanusa anguko 2015
Baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM kubariki mjadala wa kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa rais, wasomi wameibuka na kudai kuwa hali hiyo imetokana na chama hicho kusoma alama za nyakati sambamba na kuanza kunusu harufu za anguko lake.
Mbali na kuridhia kuhoji mahakamani matokeo ya rais, kikao cha Nec, kilichomalizika mwanzoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, pia kilibariki majadala wa mgombea binafsi, madaraka ya rais, utaratibu wa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano pamoja na mambo yanayosababisha kuwepo kero za Muungano.
Baraka hizo za Nec zinaashiria kuwa chama hicho tawala kimesoma alama za nyakati na kutambua kuwa ipo siku kinaweza kung’oka madarakani na kuwa chama cha upinzani, hivyo kuwa na haki ya kikatiba kulalamikia matokeo ya rais au vyovyote vile.
Kwa muda mrefu, vyama vya siasa, wanaharakati na watu wa kada mbalimbali, wamekuwa wakihoji kinga hiyo ya rais inayomfanya asiweze kushitakiwa wakati akiwa madarakani na hata baada ya kumaliza muda wake.
Lakini jana, wakati wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti, wasomi hao wamesema kuwa huenda ubadhirifu wa mali za umma na matendo mengine yasiyo ya kizalendo, yakapungua kwa kuwa kama suala hilo likijadiliwa na Watanzania wakaridhia liingizwe katika katiba mpya, rais atakuwa makini zaidi katika utendaji wake wa kazi.
Vile vile, wamesema kuhoji madaraka ya rais kutaongeza uwajibikaji na uzalendo kwa rais atakayekuwa madarakani au atakayemaliza muda wake kwa kuhofia kuburuzwa mahakamani.
Hata hivyo, walionya kuwa lazima kuwe na utaratibu maalumu ili kuzuia kila mtu kumshitaki rais aliyemaliza muda wake.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo, alisema kuwa kitendo cha CCM kuridhia kuwepo mjadala huo, kinaonyesha wazi kuwa chama hicho tawala kimeshasoma alama za nyakati na kwamba kuna siku kitakuwa cha upinzani.
“Labda wamesoma alama za nyakati, jambo hili kwa muda mrefu limekuwa likilalamikiwa na wapinzani. Chama chochote cha siasa kinaweza kuwa cha upinzani hakuna mwenye hati miliki katika utawala wa nchi,” alisema Dk Mkumbo.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Gaudence Mpangala, alisema kuwa suala la rais kutoshitakiwa, liliibuka zaidi baada ya kushamiri kwa mfumo wa vyama vingi na kwamba ilikuwa hivyo ili kuepusha migogoro ya kisiasa.
Alisema kuwa katika misingi ya kidemokrasia, rais anaweza kushitakiwa kwa kuwa wengi wamekuwa wakifanya mambo kinyume na taratibu za nchi husika na kwamba kitendo cha kuwepo sheria ambayo itawafanya washitakiwe, kitasaidia kuwajibika zaidi.
“Kinga kwa rais ina uzuri wake na kama nchi inaamua kuwa na sheria hiyo basi lazima kuwe na sheria ya kulinda ushindani wa kisiasa…, hii itasaidia kwa kuwa hali ikiwa tofauti kila mtu atakwenda mahakamani,” alisema Prof. Mpangala.
Alisema kuwa mfumo wa vyama vingi umejaa vurugu za kila aina, kwamba demokrasia ya mfumo wa vyama vingi inatakiwa kuboreshwa ili kwenda sambamba suala hilo.
Prof. Tolly Mbwete wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), alisema kuwa hali hiyo itasaidia kwa kuwa itakuwa vigumu kwa rais kufanya madudu wakati wa utawala wake.
“Hii itasaidia kwa kuwa hawatafanya tena madudu…, hawatakuwa wakivurunda tena katika utawala wao kwa kuhofia kuhukumiwa na sheria hii, ni utaratibu mzuri” alisema Prof. Mbwete.
Mambo mengine ambayo Nec ilibariki yajadiliwe ni Muundo wa Bunge na Baraza la Wawakilishi, uwepo wa Baraza la pili la Kutunga Sheria, ukomo wa idadi ya wabunge, mfumo wa Mahakama na nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uongozi wa Jamhuri ya Muungano.
Yabaki yalivyo
Mambo ambayo Nec iliona yabaki au yaingie katika Katiba mpya kama yalivyo, ni pamoja na kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kubaki kwa muundo wa Serikali mbili, kuendeleza mihimili mitatu ya dola na kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Mambo mengine ni kuendeleza umoja wa kitaifa, kufanyika uchaguzi mara kwa mara katika vipindi maalumu kwa kuzingatia haki ya kupiga kura, kuendeleza haki za binadamu, dola kutokuwa na dini na Serikali kuwa mmiliki wa rasilimali kuu za nchi.
Mengine kuwa ni kusimamia maadili ya viongozi ikiwa ni pamoja na kuipa nguvu ya kikatiba Tume ya Maadili ya Viongozi, kuimarisha madaraka ya umma, kuhamasisha sera ya misingi ya kujitegemea, kusimamia usawa wa jinsia na haki za wanawake, watoto na makundi mengine, kusimamia hifadhi ya mazingira na Rais kuendelea kuwa mtendaji.
Habari hii imeandaliwa na Fidelis Butahe, Anthony Mayunga, Serengeti, Mariam Sangoda, Bakari Kiango, Habel Chidawali, Dodoma, Mussa Juma, Arusha
Najua wengine watarudi nyumbani. Ubalozi sio shingo ngumu. Hali halisi ni ngumu. Wao wanaweza kujitoa kama Chadema kweli wakawa nje. Ngoja kazi ianze na walipa kodi pia wafanyakazi na wakulima watasema lao wasomi Bwana ni kazi kuwaridhisha.
ReplyDelete