Mnyika afunika Dar
AMBWAGA TENA MGOMBEA CCM, MAHAKAMA KUU YATUPILIA MBALI MADAI YA NGH'UMBI
James Magai na Nora Damian
NDEREMO na vifijo vya wapenzi na Chadema, jana viliitikisa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam baada ya Jaji Upendo Msuya kutupilia mbali madai ya aliyekuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Ubungo kupitia CCM, Hawa Ngh’umbi kupinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa jimbo hilo, John Mnyika wa Chadema.
Huu ni ushindi wa pili wa Mnyika dhidi ya Ngh’umbi baada ya kumshinda katika matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa jimbo hilo la Ubungo, katika uchaguzi wa Oktoba 31, 2010.
Katika hukumu hiyo ya kurasa 57 aliyoisoma kwa saa 1:21 (kuanzia saa 4:10 hadi 5:31), Jaji Msuya alitupilia mbali hoja zote tano, ambazo pande zote ziliyakubali kama mambo yaliyokuwa tata, hivyo kuhitaji uamuzi wa mahakama.
Jaji Msuya alitupilia mbali madai yote ya Ngh’umbi akisema ameshindwa kuyathibitisha mahakamani pasi na shaka, huku akidai kuwa ushahidi wa shahidi wa kwanza (PW10 upande wa madai) ulikuwa ni maneno ya kusikia tu ambayo hakuyashuhudia.
Ngh’umbi alifungua kesi dhidi ya Mnyika akidai kwamba uchaguzi huo uligubikwa na ukiukwaji wa taratibu wakati wa mchakato wa kampeni na utangazaji matokeo.
Mbali na Mnyika ambaye alikuwa mdaiwa wa pili katika kesi hiyo wadaiwa wengine walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na Msimamizi wa Uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni).
Katika kesi hiyo namba 107 ya mwaka 2010, Ngh’umbi ambaye alikuwa akitetewa na Wakili Issa Maige, katika hati yake ya madai na wakati akitoa ushahidi wake mahakamani pamoja na mashahidi wake alidai kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa sheria katika uchaguzi huo.
Ngh'umbi alidai kuwa, ukiukwaji wa sheria ulifanywa katika mchakato wa ujumlishaji wa kura na utangazaji wa matokeo, hivyo uliathiri matokeo ya uchaguzi huo kwa ujumla wake.
Kutokana na madai hayo, Ngh'umbi aliiomba Mahakama pamoja na mambo mengine ibatilishe matokeo hayo na kuamuru ufanyike uchaguzi mdogo.
Hata hivyo, katika hukumu yake Mahakama ilitupilia mbali madai na maombi yote ya Ngh’umbi na kumthibitisha Mnyika kuwa mbunge halali wa jimbo hilo.
Katika hukumu hiyo, Jaji Msuya alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wachache na kwamba, mlalamikaji huyo alipaswa kuwaita mahakamani baadhi ya watu kutoka upande aliokuwa akiulalamikia kwenda kumtetea.
Chadema walipuka
Hukumu hiyo ya Jaji Msuya iliamsha shangwe kubwa, makofi na miluzi miongoni mwa wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika ndani na nje ya mahakama hiyo, wakifuatilia hukumu hiyo kupitia kwenye spika zilizowekwa nje ya ukumbi wa mahakama.
Wakati Chadema wakichekelea, upande wa mlalamikaji Ngh’umbi na Wakili wake, Maige walielezea kutoridhishwa na hukumu hiyo huku wakielezea kushangazwa na sababu alizozitoa Jaji Msuya kutupilia mbali madai yao na kumpa ushindi Mnyika.
Kwa upande wao wafuasi wa Chadema walielezea kuridhishwa na hukumu hiyo huku Mwenyekiti wake wa Taifa, Freeman Mbowe ambaye pia alihudhuria mahakamani hapo akisema kuwa Mahakama imedhihirisha kuwa inatenda haki hata kwa wapinzani.
Katika hukumu yake, Jaji Msuya alisema anatambua kuwa wingi wa mashahidi si kigezo cha kushinda kesi ila kuaminika na kukubalika kwa ushahidi wa mashahidi.
Alisema mlalamikaji alishindwa kuithibitishia mahakama madai yake kwa kushindwa kuwaita mahakamani mashahidi wengi zaidi ili kuunga mkono ushahidi wa mashahidi wake wawili.
Baadhi ya mashahidi ambao Jaji Msuya aliwataja kwamba walipaswa kuitwa mahakamani na upande wa walalamikaji ni pamoja na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Lambart Kyaro na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Rajabu Kiravu.
Kutokana na sababu hizo, Jaji Msuya alitupilia mbali madai yote ya Ngh’umbi akisema ameshindwa kuthibitisha madai yake katika hoja zote tano ambazo zilipaswa kutolewa uamuzi.
Hoja ambazo Ngh’umbi alipaswa kuzithibitisha mahakamani ni pamoja na kama mlalamikiwa wa pili (Mnyika), alitoa kauli za kashfa dhidi yake, kwa kumwita fisadi akimtuhumu kuuza jengo la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na iwapo kulikuwa na upungufu katika ujazaji wa fomu namba 21B ( fomu za matokeo ya kura za ubunge vituoni).
Hoja nyingine ni kama mlalamikiwa wa pili (Mnyika), aliingia na kompyuta (laptop) tano katika chumba cha majumuisho ya kura na kama ndizo zilizotumiwa na wasimamizi wa uchaguzi kuhesabu na kujumlishia kura pia kama Mnyika, aliingia na kundi la wafuasi wake katika chumba cha majumuisho kinyume cha sheria.
Hoja ya mwisho ambayo Ngh’umbi alipaswa kuithibitisha ni kama kulikuwa na makosa katika ujazaji wa Fomu namba 24B (fomu za matokeo ya jumla ya ubunge) hivyo kuathiri matokeo ya uchaguzi mzima.
Ushahidi
Akitoa ushahidi wake mahakamani, Ngh’umbi alidai kuwa matokeo hayo siyo sahihi kwa sababu pamoja na mambo mengine, katika fomu ya matokeo yaliyotangazwa kuna kura 14,854, zisizojulikana mahali zilikotoka huku Ngh’umbi na shahidi wake wakiziita kura hewa.
Alidai kuwa kwa mujibu wa fomu hiyo, kura halisi zilikuwa ni 119,823, kura halali zilikuwa ni 117,639 huku kura zilizokataliwa (zilizoharibika) zikiwa ni 2,184.
Lakini, wakati wakijitetea, mdaiwa Mnyika alikanusha madai hayo yote licha ya kukiri kuwepo kwa mkanganyiko wa usahihi na uwiano wa kura katika Fomu namba 24B. Hata hivyo, alidai kuwa dosari hizo zinaweza kurekebishwa na kwamba haziathiri matokeo kiasi cha kuyafanya yawe batili.
Mawakili wa utetezi, Justice Mulokozi kwa niaba ya AG na Edson Mbogoro kwa niaba ya Mnyika walidai kuwa mlalamikaji ameshindwa kuthibitisha madai yake na hivyo, kuiomba mahakama iyatupile mbali.
Hata hivyo, wakili wa Ngh’umbi, Issa Maige alitamba kuwa wameweza kuthibitisha madai yao kwa kiwango kinachohitajika kisheria na kuiomba mahakama itengue matokeo hayo yaliyompa ushindi Mnyika.
Maige alisema madai mengine yameungwa mkono na mashahidi wa utetezi hususan DW1 aliyekiri Mnyika kuingia na kompyuta katika chumba cha majumuisho ingawa, alikanusha kuzitumia kufanyia majumuisho tofauti na Mnyika aliyekana kuingiza kompyuta hizo katika chumba hicho.
Pia wakili Maige alihoji sababu ya mawakili wa serikali kutokuwaita mahakamani baadhi ya mashahidi ambao walitajwa na upande wa madai na wa wadaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine, katika mchakato wa uchaguzi huo.
Wakili Maige aliwataja mashahidi hao ambao alidai walikuwa ni muhimu kuitwa mahakamani ili kujibu madai na kutoa ufafanuzi wa masuala yaliyowagusa kuwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Nec.
Mkurugenzi huyo alidaiwa kwamba ndiye alikagua kompyuta zilizotumika kufanyia majumuisho ya kura badala ya zile zilizotoka Manispaa ya Kinondoni kutokana na mfumo wa awali ulioandaliwa na Nec kuonekana kuwa haufai.
Maige alidai kuwa kitendo cha kushindwa kumwita mkurugenzi huyo mahakamani kutoa maelezo ya ukaguzi alioufanya na mbinu alizozitumia kuithibitishia mahakama kuwa katika kompyuta hizo isingewezekana kuingizwa taarifa za kughushi ni kinyume cha sheria.
Akirejea kesi ya Stanbic Bank (T) Ltd dhidi ya Woods (T) Ltd namba 48 ya mwaka 2002, alidai Mahakama ilishatoa mwongozo kuwa ushahidi wa kitaalamu hauwezi kuthibitishwa kwa maneno matupu, pasipo mtaalamu kuitwa kuutolea ufafanuzi.
Wakili Maige alidai kuwa upande wa madai umethibitisha kuwa kompyuta zisizostahili kisheria ndizo zilizotumika kufanya majumuisho na kwamba, ndizo zilizosababisha kuwepo kwa mkanganyiko uliojitokeza katika fomu ya matokeo wa kura zaidi ya 14,000 zisizo na maelezo.
Hata hivyo, katika hukumu yake Jaji Msuya alisema jukumu la kuwaita mashahidi hao akiwemo mkurugenzi huyo na Kiravu lilikuwa ni la mlalamikaji na kwamba, kwa kushindwa kufanya hivyo ameshindwa kuthibitisha madai yake.
Kuhusu makosa katika ujazaji wa fomu namba 24, Jaji Msuya alikubaliana na hoja za utetezi ni makosa ya kibinadamu akidai kuwa kulingana na mchakato wa jukumu hilo kufanya kazi hiyo kwa muda mrefu ni jambo la kawaida kwa makosa kama hayo kutokea.
“Katika hitimisho langu nakubali kuwa hakuna hoja hata moja katika hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho kama ilivyodaiwa kuthibitishwa,” alisema Jaji Msuya na kuongeza:
“……ninatamka kuwa mdaiwa wa pili alichaguliwa kihalali kuwa mbunge wa Jimbo la Ubungo, katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010 kwa kura 16, 198. Mdai atalipa gharama za uchaguzi”.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 31, Novemba 2, 2010 Msimamizi wa Uchaguzi, Raphael Ndunguru alimtangaza Mnyika kuwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho kwa kura 66,742 dhidi ya Ngh’umbi aliyepata kura 50,544 akimzidi Ngh’umbi kura 16,168.
Hata hivyo, Ngh'umbi hakuridhika na matokeo hayo ndipo alipofungua kesi hiyo Mahakama Kuu kupitia kwa Wakili wake Issa Maige akiiomba mahakama hiyo itengue matokeo ya uchaguzi huo.
Polisi wazingira mahakama, shughuli zasimama
Waandishi Wetu
JESHI la Polisi Kanda maalumu ya Dares Salaam jana liliimarisha ulinzi kwa kuweka askari zaidi ya 30 katika mahakama kuu kanda ya Dares Salaam wakati wa hukumu ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo la Ubungo, hukumu ambayo ilimpa ushindi John Mnyika wa Chadema.
Wakati jeshi hilo likiimarisha ulinzi, baadhi ya shughuli katika eneo hilo zilisimama kwa muda. Katika viwanja vya mahakama hiyo, askari polisi zaidi ya 30 wakiwemo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walikuwa wametanda.
Wafuasi wa CCM na Chadema walifika mahakamani hapo kuanzia saa 2.00 asubuhi na wengine wakiwa wamevalia sare za vyama vyao, lakini walilazimika kusubiri nje ya geti hadi saa 3:15 waliporuhusiwa kuingia ndani ya mahakama. Chadema waliongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.
Mnamo saa 5:30 asubuhi baada ya Jaji Upendo Msuya kumaliza kusoma hukumu yake, wafuasi wa Chadema walianza kushangilia huku wafuasi wa CCM wakionekana kuwa na nyuso za huzuni na wengine waliangua kilio.
Wafuasi wa Chadema walikuwa wakishangilia huku wakiimba nyimbo mbalimbali na kunyanyua vidole viwili juu. Wafuasi hao walisikika wakisema, ‘peoples power (nguvu ya umma), mafisadi wameshindwa.’
Muda mfupi baadaye, Mnyika alitoka nje ya mahakama na kubebwa juu na wafuasi wa Chadema huku akishangiliwa. Wafuasi wa CCM walianza kuondoka taratibu katika viwanja vya mahakama hiyo na wengi wakionekana kuwa na nyuso za huzuni.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Mbowe alisema “….lingekuwa pigo sana kama tungemkosa Mnyika kwasababu tunathamini kazi yake ndani ya chama, jimbo na taifa kwa ujumla”.
Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema licha ya kuwepo kwa mahakimu na majaji wachache wasiokuwa waadilifu lakini ,bado wanaendelea kuiamini mahakama.
“Tunaishukuru mahakama imesimamia misingi ya sheria tunaiheshimu sana na tunaomba iendelee hivyo. Hii imeonyesha kuwa mahakama inaweza kutenda haki hata kwa wapinzani,”alisema Mbowe.
Alisema anakusudia kupeleka hoja bungeni kufanya marekebisho ya sheria ya uchaguzi ili mtu anayefungua kesi bila hoja za msingi mbali na kulipa gharama za uendeshaji kesi pia aweze kuilipa Serikali kwasababu inatumia pesa nyingi kuendesha kesi. Mbowe alisema kesi hiyo imegharimu zaidi ya Sh1bilioni.
Hata hivyo, akitoa mchanganuo wa gharama za kesi hizo wakati kesi hizo zilipofunguliwa Jaji Kiongozi Fakih Jundu alisema kila kesi ingegharimu takribani Sh52milion na kwamba, kwa kesi zote 43 zilizokuwa zimeshafunguliwa zingegharimu zaidi ya Sh2bilioni.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kesi hiyo ilifunguliwa kwa jazba bila kuwapo kwa ushahidi wowote na kushauri kuwa kama mtu hana ushahidi asikimbilie mahakamani.
Mwenyekiti huyo wa Chadema, alishauri pamoja na wadai kutakiwa kulipa faini pia wawe wanashtakiwa kwasababu wanaliingiza taifa katika hasara kubwa isiyokuwa ya msingi na kuchelewesha maendeleo.
Ngh’umbi kichwa chini
Saa 5:52 asubuhi baada ya hukumu hiyo, Ngh’umbi alitoka nje ya mahakama akiwa ameongozana na wafuasi wachache wa chama chake. Akizungumza na waandishi wa habari alisema atakwenda kukaa na wakili wake ili wajipange.
“Sasa hivi bado ni mapema sana kusema nitafanya nini hadi nikae na wakili wangu nijipange,”alisema Ng’umbi huku akisindikizwa na wafuasi wake kwenda kupanda gari.
Mapema Saa 3:20 Ngh’umbi akiwa amevalia suti ya kijivu, alingia ukumbi namba moja wa mahakama Kuu, na kuketi kwenye benchi la mbele nyuma ya mawakili.
Dakika sita baadaye, saa 3:26 Mnyika aliingia ukumbini na kupokewa na wafuasi wa Chadema kwa kumpigia makofi. Mnyika alikuwa amevaa sare za chama chake zenye rangi ya khaki maarufu kama kombati.
Mnyika alijibu kwa kuwapungia mikono na kwenda hadi benchi alilokuwa amekaa Ngh’umbi ambako, walisamiliana kwa kupeana mikono kisha alikaa kushoto kwake na kuanza kuzungumza wakati wakisburi Jaji Msuya kuingia mahakamani.
Wakati fulani Ngh’umbi alionekana akimgusa Mnyika kifuani mithili ya mtu aliyekuwa akimpima mapigo ya moyo.
Mbowe ndiye aliyeonekana kivutio zaidi baada ya kuingia ukumbini humo, saa 3:45 naye akiwa amevaa kombati. Kuingia kwa Mbowe kuliwafanya wafuasi wa Chadema kulipulika kwa shangwe kubwa huku wakimpigia makofi na kelele.
Mbowe alikwenda kwa Mnyika wakasalimiana kisha alikaa kwenye benchi lililokuwa nyuma ya benchi, walilokaa Mnyika na Ngh’umbi na kusubiri kusomwa kwa hukumu.
Dakika 11 baadaye baada ya Mbowe kuingia ukumbini, saa 4:08, Jaji Msuya aliingia mahakamani na kukaa kwenye kiti chake. Alianza kusoma hukumu hiyo saa 4:10 hadi saa 5:30 alipohitimisha.
Shughuli zasimama
Ushindi huo wa Mnyika ulisababisha shughuli mbalimbali katika baadhi ya mitaa ya jiji kusimama kwa muda kutokana na maandamano yalioyoanzia Barabara ya Kivukoni hadi eneo la Kimara kona, zilipo ofisi za Mbunge huyo.
Maandamano yalikuwa yakiongozwa na Mbunge huyo huku magari ya FFU yakifuatilia kwa karibu.
Awali, polisi walimshauri Mnyika apande gari ili kuzuia maandamano yasiendelee, lakini wafuasi wake walikataa na kumwambia Mbunge wao asikubali na kusisitiza: ”tunakuomba Mheshimiwa utusikilize sisi hakuna kupanda gari tutatembea na wewe mpaka kwenye ofisi zetu”.
Wakati msafara huo ulipokuwa njiani, ulizuiwa na wafanyabishara ndogondogo eneo la Manzese na eneo la Big Brother lililopo njia panda ya Mabibo waliotaka kuongea na Mnyika ili kumpongeza.
Hata hivyo, ombi hilo halikuwezena badala yake walishauri kujiunga katika msafara huo kuelekea katika ofisi za mbunge huyo.
Hali kama hiyo ilijitokeza pia katika eneo la Ubungo stendi ya mkoa ambako, vijana walijaa barabarani na kuzua msafara wakitaka aingie ndani stendi ili wampongeze hata hivyo, nao pia walishauriwa wajiunge kwenye msafara. Mbunge huyo baada ya kufika katika Ofisi za Chadema jimbo la Ubungo, alipanda juu ya gari na kuanza kuwahutubia wafuasi wake waliofurika katika ofisi hizo.
“Napenda kuwapongeza wananchi wa jimbo langu na wapenzi wa Chadema,vijana ,wanawake na wazee mliojitokeza kwa wingi kuanzia mahakamani hadi hapa tulipo kwa kujitolea muda wenu na kuacha kazi zenu na kuungana na mimi.Na hiyo haikuanza leo bali mlifanya hiyo tangu kesi ilipoanza hadi leo tumeisha, nawapongeza sana,” alissema Mnyika.
Aliongeza: “Nilikuwa katika kipindi kigumu cha kushughulikia matatizo ya jimbo langu na wakati huo, kushughulika kesi kitu ambacho kilikuwa kinaniweka katika wakati mgumu.”
“Sasa Mahakama imeishatenda haki na mimi Mbunge halali, nitaanza kushughulikia matatizo ya wananchi ….nitaanza na mpango wa kuanzisha mfuko wa elimu wa jimbo ambao utasomesha watoto ambao wazazi hawana uwezo. Katika mpango huo nategemea kufanya harambee na kukusanya kiasi cha Sh.100milioni.”
Wakati akihitimisha hotuba yake, aliwataka wafuasi kutoondoka eneo hilo bali wauungane naye katika hafla fupi ya kusherekea ushindi ambapo aliagiza ng’ombe mzima kuchinjwa huku wengi wakijitolea michango kwa ajili ya kununulia vinywaji.
Imeandaliwa na Nora Damian, James Magai na Fidelis Felix
CHANZO CHA HABARI;http://mwananchi.co.tz/component/content/article/37-tanzania-top-news-story/23269-mnyika-afunika-dar.html
0 comments:
Post a Comment