Friday, May 25, 2012

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imesema meli kubwa 14 kati ya 74 zilizokuwa zikitoa huduma katika Ziwa Victoria zimesimamishwa kufanya kazi baada ya kufanyiwa ukaguzi na kubainika kuwa na upungufu.

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Kanda ya Ziwa, Alferd Waryana aliliambia gazeti hili jana kwamba udhibiti wa vyombo vya usafiri wa majini hufanywa na Sumatra kwa kushirikiana na uongozi wa bandari, polisi, manahodha, wamiliki na watendaji wa kata na vijiji.

Akitoa takwimu za ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na Sumatra kwa meli kubwa alisema katika mwaka 2006/07 walikagua meli 40 na kati ya hizo, 29 zilisimamishwa. Mwaka 2007/08 ukaguzi ulifanyika kwa meli 45 na 29 zilisimamishwa.

Aliongeza kuwa katika mwaka 2008/09 meli 132 zilifanyiwa ukaguzi ambapo 41 zilikutwa na upungufu na kusimamishwa, 2009/10 meli 166 zilikaguliwa na 43 zilisimamishwa na mwaka 2010/11 meli 128 zilikaguliwa na 18 zilikuwa na mapungufu.

Alisema meli nyingi hukutwa na mapungufu katika mashine na kuwa na bodi zenye matatizo hivyo kutakiwa kufanyiwa matengenezo.

Mamlaka imekuwa ikipitia na kuridhia ubunifu wa meli inayotaka kujengwa kwa kuangalia kila hatua ya ujenzi na inapokamilika hukaguliwa na kuainisha vifaa vya kujiokolea, kuongozea, nyenzo za kupambana na moto na kuhakiki uwiano wa meli kabla ya kutoa cheti.

Akizungumzia boti zinazotoa huduma ya usafiri katika Ziwa Victoria, Waryana alisema kuanzia mwaka 2008 hadi sasa jumla ya boti 6,271 zilikaguliwa na kati ya hizo 4,922 zilikidhi viwango na kupewa vyeti.

Aidha kwa upande wa boti zilizoruhusiwa zinazotumia mashine, alisema abiria wote wahakikishe wanavaa maboya ya kujiokolea wakati wote wa safari
CHANZO CHA HABARI HII NI GAZETI LA HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment