NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos
Makalla amejitoa katika Kamati ya Fedha ya klabu ya Simba na kuanzia
sasa atakuwa akizisaidia timu zote hapa nchini.
Makalla alibainisha hayo juzi, katika sherehe za klabu hiyo
kujipongeza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zilizofanyika
ukumbi wa Dar Live Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Makalla, alisema, sababu ya kujitoa ni kutokana na wadhifu mkubwa alionao kwa sasa.
“Mimi nilikuwa ni mmoja wa viongozi waliokuwa katika Kamati ya Simba
na kuchangia mafanikio haya ambayo Simba imeyapata, lakini kwa sasa kwa
kuwa ni waziri, jukumu langu ni kusaidia timu zote nchini bila ya kujali
Simba wala timu yoyote,” alisema Makalla.
Aliuasa uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi, kutoridhika na mafanikio
hayo na kuwaomba kuzidi kupigana kufa na kupona ili kuendeleza hali ya
mafanikio ndani ya klabu hiyo na kujipanga ili kufanya vizuri zaidi.
Alisema ana imani kubwa klabu ya Simba ina uwezo mkubwa wa kujenga uwanja mzuri wa kisasa kutokana na ukongwe ambao inayo.
Katika sherehe hizo, Makalla akimkabidhi nahodha wa Simba, Juma
Kaseja, tuzo na medali maalumu kwa ajili ya aliyekuwa mchezaji wa timu
hiyo, marehemu Patrick Mafisango aliyefariki hivi karibuni kwa ajali ya
gari, ambapo nahodha huyo alishindwa kujizuia na kuangua kilio na
kuwafanya baadhi ya wachezaji wenzake, mashabiki na wapenzi kuanza
kumwaga machozi.
Kabla ya kutolewa kwa tuzo hiyo, ulipigwa muziki wa ‘Kazi yake Mola
Haina Makosa’ wa Msanii Madee kumkumbuka Mafisango na mara baada ya
wimbo huo kumalizika, shughuli zote ukumbini hapo zilisimama kwa dakika
moja na watu wote walisimama na kumwombea mchezaji huyo.
Naye Meneja wa Global Publishers Limited, Abdallah Mrisho, alikabidhi
sh milioni 3 kwa Kaseja, kama zawadi yao kwa wachezaji na benchi la
ufundi ikiwa ni pongezi kwa kazi nzuri waliyoifanya katika msimu
uliopita wa 2011/12 hadi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Sherehe hizo zilipambwa na wanamuziki na bendi mbalimbali hapa nchini, ikiwemo Msondo, Mshauzi Classic, Young D.
CHANZO CHA HABARI:http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=36432
0 comments:
Post a Comment