RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kuwaapisha mawaziri na manaibu waziri aliowateua na wengine kuwabadilisha wizara. Kwa mujibu wa Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi jioni, Rais wa Kikwete atawaapisha watendaji hao waandamizi wa Serikali kuanzia saa tano asubuhi. Mawaziri pamoja na manaibu waziri wapya watakaoapishwa leo ni 13 pamoja na wanne ambao walipandishwa kutoka manaibu waziri na kuwa mawaziri kamili. Rais Kikwete pia amewahamisha wizara mawaziri wanane na manaibu waziri sita. Mawaziri wapya watakaoapishwa na Wizara zao kwenye mabano ni Mbunge wa Handeni, Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Mbunge wa Kalenga, Dk William Mgimwa (Fedha) na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini). Manaibu Mawaziri wapya ni Mbunge wa Rufiji, Dk Seif Suleiman Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii), Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (Nishati na Madini- Nishati), Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Mbunge wa Buchosa, Dk Charles Tizeba (Uchukuzi) na Mbunge wa Mvomero, Amos Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo). Wengine ni Mbunge wa Makete, Dk Binilith Mahenge (Maji), Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Maselle (Nishati na Madini ), Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki (Katiba na Sheria) na wabunge wa kuteuliwa, Janet Mbene na Saada Mkuya Salum ambao wote wamekuwa Manaibu Waziri wa Fedha. Naibu Mawaziri waliopandishwa na kuwa mawaziri kamili ni Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Fenella Mukangala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) na Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii). Mawaziri wengine waliohamishwa kutoka wizara zao za awali kwenda nyingine ni, Celina Kombani kutoka Katiba na Sheria kwenda Ofisi ya Rais (Manejimenti ya Utumishi wa Umma) ambako amechukua nafasi ya Hawa Ghasia ambaye amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi). Shamsi Vuai Nahodha aliyehamia Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akitokea Mambo ya Ndani, ambako amechukua nafasi ya Dk Hussein Mwinyi ambaye amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Dk Emmanuel Nchimbi amehamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akitokea Habari, Utamaduni na Michezo wakati Waziri wa Katiba na Sheria sasa ni Mathias Chikawe ambaye alikuwa Ofisi ya Rais (Utawala Bora) na Profesa Jumanne Maghembe amehamishiwa Maji akitokea Kilimo; George Mkuchika ambaye sasa amehamishiwa Ofisi ya Rais – Utawala Bora akitokea Tamisemi na Profesa Mark Mwandosya ambaye ameteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais, asiyekuwa na Wizara Maalumu. Kabla ya hapo alikuwa Wizara ya Maji. Manaibu Waziri waliohamishwa wizara zao za zamani zikiwa kwenye mabano ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Charles Kitwanga (Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Adam Malima, Kilimo, Chakula na Ushirika (Nishati na Madini) Pereira Ame Silima, Mambo ya Ndani ya Nchi (Fedha). Wengine ni Gregory Teu, Viwanda na Biashara (Fedha) Lazaro Nyalandu Wizara ya Maliasili na Utalii (Viwanda na Biashara), Jerryson Lwenge Ujenzi (Maji). Waliobaki kwenye nafasi zao Mawaziri waliobaki kwenye nafasi zao ambao hawataapishwa leo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi. Wengine ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo. Pia wamo mawaziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka. Kwa upande wa manaibu ni Kassim Majaliwa na Aggrey Mwanry (Tamisemi), , Dk Makongoro Mahanga (Kazi na Ajira), Benedict Ole-Nangoro (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Mahadhi Juma Maalim (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Goodluck Ole-Medeye (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Ummy Mwalimu (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Philipo Mulugo (Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Dk Abdulla Juma Abdulla (Ushirikiano wa Afrika Mashariki). |
Home
»
»Unlabelled
» JK kuapisha Mawaziri leo
Monday, May 7, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment