CAG: Mawaziri wapya wakicheza watang'oka | Send to a friend |
Boniface Meena MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amewaonya mawaziri wapya na watendaji serikalini kwamba ripoti zake hivi sasa zina nguvu za kusimamia uwajibikaji hivyo, wanapaswa kusimamia vyema wizara zao kuzuia ubadhirifu wa fedha za umma. Kauli hiyo ya Utouh ni ya kwanza tangu ripoti yake ya mwaka huu kuwang’oa mawaziri sita kati ya wanane ambao wizara zao zilionekana kugubikwa na ufisadi wa fedha za umma. Akizungumza jana, Utouh alisema mawaziri wanapaswa kufahamu kwamba kuanzia sasa hadi mwaka 2015, zitatoka ripoti nyingine tatu, hivyo ni vyema wakachukua tahadhari wakiwa ndiyo wasimamizi wakuu wa shughuli za wizara. Alisema kilichotokea bungeni na hadi mawaziri kuwajibishwa, kimethibitisha kuwa sasa kutakuwa na uwajibikaji mkubwa utakaosababishwa na ripoti zake kama watendaji wasipofuata taratibu za Serikali. “Mawaziri ni wasimamizi wa wizara hata kama ni wanasiasa, wao ndiyo wanaowajibika kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri wizarani hivyo ni muhimu wakafanya hivyo,” alisema Utouh. Alisema kilichotokea ni sehemu ya uwajibikaji na kusema hatua iliyochukuliwa na Rais imetokana na ripoti ya ofisi yake kuonyesha udhaifu katika usimamizi uliofanywa na watangulizi wao hivyo kuwataka kuwa makini. Utouh alisema kwa kuwa ofisi yake inapaswa kuandaa ripoti tatu hadi kufikia mwisho wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete watendaji hao waandamizi wa Serikali wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutimiza wajibu wao. Alisema angalizo hilo haliwahusu mawaziri tu, bali hata watendaji walioko chini yao. CAG alisema hivi sasa ofisi yake inaandaa ripoti nyingine mahsusi kuhusu vitendo vya jinai, rushwa na ubadhirifu vilivyotokana na kile kilichowang’oa viongozi hao tayari kwa ajili ya kuiwasilisha kwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru). “Barua ambayo Takukuru walituandikia kuhusu wale ambao wamezungumzwa kwenye ripoti nimeiona na tunaishughulikia lakini nikwambie tu kwamba hata kama wasingetuandikia tungewapelekea kwa kuwa tumekuwa tunafanya kazi nao kwa karibu,” alisema. Ripoti hiyo ya CAG ndiyo iliyamlazimu Rais Kikwete kupangua Baraza lake la Mawaziri na kuwang'oa sita, Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omary Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Mustafa Mkulo (Fedha) na William Ngeleja (Nishati na Madini). Nafasi za mawaziri hao sasa zimejazwa na Mbunge wa Handeni, Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Mbunge wa Kalenga, Dk William Mgimwa (Fedha) na Mbunge wa Kuteuliwa Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Hussein Mwinyi (Afya na Ustawi wa Jamii) na Balozi Hamis Kagasheki (Maliasili na Utalii). Kilichowang’oa Baadhi ya tuhuma zilizokuwa zimeibuliwa na CAG kwenye Wizara ya Fedha iliyokuwa chini ya Mkulo ni kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), ili kuficha tuhuma zake ikiwemo uuzaji wa Kiwanja Na.10 kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL). Ukaguzi wa CAG ulibaini kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wizara ya Fedha, zilihusika moja kwa moja katika uuzwaji wa kiwanja hicho kilichopo kando ya Barabara ya Nyerere bila kuishirikisha bodi ya CHC. Aidha, CAG alibaini kuwapo kwa utata katika hati ya madai ya Sh2.4 bilioni kutoka katika kampuni ya DRTC zinazodaiwa kuwa ni gharama za ulinzi na tozo la matumizi ya barabara ya kuingilia kwenye Kiwanja Na.192 kando ya Barabara ya Nyerere. Upungufu pia ulionekana kwenye uuzwaji wa Jengo la Kampuni ya Tanzania Motors (TMC) lililopo Kiwanja Namba 24 kilichopo katika eneo la Viwanda la Chang’ombe kwa Kampuni ya Maungu Seed. Kwa upande wa Ngeleja, alikabiliwa na kashfa baada ya CAG kubaini kuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kwa mwaka mmoja wa fedha linafanya ununuzi wenye thamani ya Sh300 bilioni hadi Sh600bilioni. Kwa mwaka wa fedha 2009/2010, Tanesco lilitumia Sh1.8 bilioni ukilinganisha na Sh65 milioni zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya ukarabati wa gati mojawapo katika Kituo cha Bwawa la Mtera na kuingia mikataba isiyo na tija kwa taifa. Kwa Maige, ripoti ya CAG ilieleza kuwa ofisi yake ilipoteza Sh874,853,564 baada ya kufanya uamuzi wa upendeleo wa kutoa kiwango cha chini cha mrabaha kwa mauzo ya misitu. Katika kipindi cha ukaguzi wa hesabu za Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (Tanapa), ilibainika kuwa liliingia katika mkataba na kampuni ya CATS Tanzania Ltd unaohusiana na matengenezo ya kawaida, ufungaji wa vifaa vya mawasiliano na vifaa vingine katika mkataba wa jumla ya Dola za Marekani milioni moja (wastani wa Sh1.5 bilioni). Pia anatuhumiwa kuweka mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji, ambao unadaiwa kutawaliwa na dosari nyingi ikiwa ni pamoja na kutangaza majina ya waliopata vitalu bila kuonyesha jinsi walivyopewa. Pia, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilieleza kuwa kampuni 16 zilizopewa vitalu hivyo hazikuomba na kwamba vitalu hivyo vilikuwa vya daraja la kwanza na la pili. Mbali na tuhuma hizo, Maige hivi karibuni alidaiwa kununua nyumba kwa Dola za Marekani 700,000 iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam, tuhuma ambazo alizipinga na kusema kuwa nyumba hiyo ameinunua kwa Dola 410,000, sawa na zaidi ya Sh600 milioni). Dk Mponda alikabiliwa na kashfa ya Bohari ya Dawa (MSD) ambako ukaguzi maalumu ulibaini kuwapo tofauti ya Sh658.9 milioni ikiwa ni pungufu ya kiasi ambacho kilipokewa na kuripotiwa na wizara hiyo kwenda bohari, huku ushahidi wa kupokewa kwake ukiwa haujatolewa. Pia, ukaguzi huo maalumu ulibaini kuwapo kiasi cha Sh4.5 bilioni zilizotoka Hazina kwenda wizara hiyo kununulia dawa na vifaa vya hospitali, lakini kiasi cha Sh4.344 bilioni tu ndicho kilichopokewa na MSD. Nundu alikabiliwa na kashfa ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam huku akituhumiwa kuipigia kifua Kampuni ya Chinese Merchant ipewe zabuni ya upanuzi huo wa bandari. Lakini, Nundu alimtuhumu aliyekuwa naibu wake, Athumani Mfutakamba ambaye naye ameng'olewa kwamba alikuwa akishinikiza Kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC), ipewe kazi ya kujenga gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ilimgharamia safari kadhaa kwenda nje. Hata hivyo, Mfutakamba alipoulizwa kuhusu safari zake hizo za nje kugharamiwa na CCCC na baadaye kuandika ripoti akishinikiza ipewe kazi ya kujenga gati hizo, alikiri kusafirishwa lakini akasema alifuata taratibu zote za kiserikali. Dk Chami alituhumiwa kumlinda Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege kutokana na tuhuma za kuwepo ofisi hewa za ukaguzi wa TBS zilizopo nje ya nchi. Ekelege anadaiwa kusimamia ofisi hewa za ukaguzi wa magari huko Singapore na Hong Kong na kuitia Serikali hasara ya karibu Sh30bilioni. |
0 comments:
Post a Comment