Waandishi Wetu
KAULI ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Ole Millya kwamba idadi kubwa ya wanaCCM watamfuata baada ya kuhamia Chadema imeanza kujidhihirisha baada ya Diwani wa Kata ya Sombetini, Alphonce Mawazo na Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM Wilaya ya Longido, Yohana Laizer kutangaza kuondoka chama hicho tawala jana.
Kabla ya kujiunga na CCM, Mawazo ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alikuwa Chama cha TLP na alishinda udiwani wa kata hiyo kupitia TLP kabla ya kujiuzulu na baadaye kugombea tena kupitia CCM na kushinda.
Katika kampeni za ubunge mwaka 2010, licha ya Mawazo kugombea kupitia CCM, swahiba wake Lema wa Chadema aliongoza kampeni zake kwa kupanda majukwaani na kumwombea kura.
Kama ilivyokuwa kwa Ole Millya, viongozi hao pia walisisitiza kujiunga na Chadema kutoka CCM wakidai kwamba imepoteza mwelekeo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare alithibitisha jana kupokea taarifa za viongozi hao kung’oka CCM na kujiunga na Chadema.
“Ni kweli nimepewa taarifa za Laizer na huyo Mawazo kujiondoa CCM. Nadhani huo ni uamuzi wao sisi hatuwezi kuwaingilia,” alisema Sanare.
Kuhusu madai kwamba baadhi ya vijana wana mpango wa kumfuata Ole Millya iwapo CCM Arusha hakitatimiza madai yao, Sanare alisema hana taarifa za shinikizo hilo la ambalo pia linataka Katibu wa CCM wa Mkoani, Mary Chatanda aondolewe madarakani.
“Haya mambo ya kushinikiza katibu wa mkoa kuondoka, sisi tunayasikia tu mitaani hayajaletwa kwetu. Lakini kila jambo lina taratibu zake kama watu wana hoja walete kwenye vikao,” alisema Sanare.
Kuna madai kwamba wimbi la kuondoka wanaCCM zaidi, wakiwamo baadhi ya wenyeviti wa UVCCM wilaya na wajumbe wa Baraza Kuu la umoja huo Mkoa wa Arusha, linatajwa kuwa litaendelea wiki hii na ijayo.
Atinga Dodoma
Diwani Mawazo jana alikuwa mjini Dodoma ambako alizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kusema uamuzi wake umezingatia kwamba chama hicho kikuu cha upinzani ndiyo tumaini pekee la kuleta mabadiliko nchini.
“Sababu za kujitoa CCM na kujiunga Chadema ziko wazi. Chadema ni sauti ya wanyonge, ingawa baadhi ya watu hawatafurahishwa na kuondoka kwangu, lakini ukweli ni kwamba CCM kimekufa, tunachokiona ni kivuli chake tu,” alisema.
Alisema moyo wake umemwelekeza kupambana kutetea maslahi ya wengi na hakuna anayeweza kuona hilo kama ataendelea kuwa ndani ya CCM.
Mfumo mbovu
Akizungumza hali ya kisiasa katika Mkoa wa Arusha hivi sasa, aliyekuwa Mbunge wa Vunjo (CCM), Aloyce Kimaro alisema kinachotokea UVCCM ni matokeo ya mfumo mbovu wa utawala ndani ya CCM ambao unachangiwa na wanachama wenyewe huku akisema: “Mambo ndiyo kwanza yameanza. Maji tayari yanachemka na ugali lazima usongwe na walaji wapo wanausubiri.”
Alisema kinachotokea sasa ndani ya chama hicho mkoani Arusha ni matunda ya viongozi wake ambao alidai kwamba wameamua kwa makusudi kukiua.
Alisema huo ni mwanzo na kishindo zaidi kinakuja akisema, hakuna dawa ya kukinusuru dhidi ya tufani hiyo inayokuja. Alipoulizwa nini kifanyike kukinusuru, alijibu: “Labda kipelekwe India.”
Alisema makada wakongwe wa chama hicho akiwamo Mzee Ibrahimu Kaduma, walishaonya juu ya kutokea kwa hali hiyo siku nyingi, lakini hawakusikilizwa na badala yake kujengewa chuki hadi kuenguliwa kuwania nafasi yake ya ubunge.
Hivi karibuni, Kaduma akiwa na makada wenzake wakongwe, Dk Hassy Kitine na Joseph Butiku wakihojiwa katika kipindi cha 'Je, Tutafika' kinachorushwa na Channel Ten, walikitabiria kifo chama hicho kwa kile walichosema ni kupoteza maadili yaliyoasisiwa na kiongozi wake wa kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Wakizungumza na gazeti hili kuhusu maoni yao baada ya Ole Millya kuhama CCM, baadhi ya wenyeviti wa mikoa ambao waliomba majina yao yahifadhiwe walisema wengi wao na makatibu wa UVCCM wa wilaya, watakihama chama hicho kuanzia Juni hadi Septemba, mwaka huu wakidai hiyo ni kutokana na mwenendo usioridhisha na kupuuzwa kwa mawazo yao ya kutaka kukijenga.
Mwenyekiti wa UVCCM kutoka mkoa mmojawapo wa Nyanda za Juu Kusini, alisema makada wengi kutoka UVCCM watakihama chama hicho ifikapo Juni… “Watu wanamalizia vipindi vyao vya uongozi ambavyo vinakoma kati ya Juni na Septemba.”
Alisema ukweli wa jambo hilo utathibitika wakati wa uchaguzi wa wenyeviti wa UVCCM wa mikoa ambao unatarajiwa kufanyika katika kipindi hicho.
Mwenyekiti huyo alisema, kati ya hao yupo pia kiongozi wa juu wa jumuiya hiyo ambaye naye anasubiri muda tu akisema ni mapema mno kwake kufanya hivyo sasa.
0 comments:
Post a Comment