KADUMA ASEMA UTABIRI WA WAZEE CCM KUTIMIA, MUKAMA ASEMA WAKITOKA CHAMA KITAJUA CHA KUFANYA
Waandishi Wetu
HATUA ya aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Ole Millya kujiondoa CCM na kuhamia Chadema imeanza kukitikisa chama hicho ikidaiwa kwamba wenyeviti watano wa mikoa wa umoja huo na kundi kubwa la vijana wako mbioni kumfuata.Wakati Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama akisema kwamba chama chake kitajipanga endapo hilo litatokea, kada mkongwe wa chama hicho, Ibrahim Kaduma ameelezea uamuzi wa Ole Millya wa kukihama kwamba ni kutimia kwa utabiri wa wazee wa chama hicho.
Hivi karibuni, Kaduma akiwa na makada wenzake wakongwe, Dk Hassy Kitine na Joseph Butiku wakihojiwa katika kipindi cha 'Je, Tutafika' kinachorushwa na Channel Ten, walikitabiria kifo chama hicho kwa kile walichosema ni kupoteza maadili yaliyoasisiwa na kiongozi wake wa kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Mbali ya wanasiasa hao, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kuhama kwa Ole Millya CCM si jambo geni katika siasa za Tanzania, lakini akaeleza kushangazwa kwake na hatua hiyo ya kuhama kuanza kuwahusisha vijana.
Wakizungumza na gazeti hili kuhusu maoni yao baada ya Ole Millya kuhama CCM, baadhi ya wenyeviti wa mikoa ambao waliomba majina yao yahifadhiwe walisema wengi wao na makatibu wa UVCCM wa wilaya, watakihama chama hicho kuanzia Juni hadi Septemba, mwaka huu wakidai hiyo ni kutokana na mwenendo usioridhisha na kupuuzwa kwa mawazo yao ya kutaka kukijenga chama.
Mwenyekiti wa UVCCM kutoka mkoa mmojawapo wa nyanda za juu kusini, alisema makada wengi kutoka UVCCM watakihama chama hicho ifikapo Juni… “Watu wanamalizia vipindi vyao vya uongozi ambavyo vinakoma kati ya Juni na Septemba.”
Alisema ukweli wa jambo hilo utathibitika wakati wa uchaguzi wa wenyeviti wa UVCCM wa mikoa ambao unatarajiwa kufanyika katika kipindi hicho.
Mwenyekiti huyo alisema kati ya hao, yupo pia kiongozi wa juu wa jumuiya hiyo ambaye naye anasubiri muda tu akisema ni mapema mno kwake kufanya hivyo sasa.
“Tumeshauri mambo mengi ndani ya chama na hata jumuiya, lakini hakuna hata moja ambalo limetekelezwa na zaidi kuna watu wamefanya hivyo wameonekana wabaya na kutengenezewa mizengwe,” alisema na kuongeza:
“Kuna wenzetu ni wafanyabiashara na wengine wana nafasi nyingine za kisiasa katika mabaraza hivyo, ni mapema mno kuweza kujitoa kwa sasa, lakini kila mmoja anakerwa na mwenendo wa chama,” alisema huku akibainisha kwamba huenda wengine wakajitoa kabla ya wakati huo hasa wale ambao wana ajira zao.
Akizungumzia madai hayo ya kuondoka na kundi la wana CCM hasa vijana, Ole Millya alisema wengi na wote waliokuwa wakimuunga mkono na kuchukia utendaji wa CCM, watamfuata.
“Siwezi kusema ni lini, lakini subirini. Wengi wanakuja Chadema kutoka CCM na UVCCM kwani hawaridhishwi na uongozi na mambo yaliyopo sasa ndani ya CCM” alisema Millya.
Mbali ya viongozi hao wa UVCCM wa mikoa, baadhi ya wenyeviti wa umoja huo katika baadhi ya kata na wilaya za Mkoa wa Arusha walisema wako njiani kujiunga na Chadema kama mapendekezo kadhaa waliyotoa ndani ya chama hicho hayatapewa uzito.
“Tunasema kama wanataka tubaki, kwanza wamuondoe Katibu wa CCM Mkoa Arusha, Mary Chatanda kwani ndiye chanzo cha vurugu zote za Arusha na pia chama kitusikilize katika madai mbalimbali kuhusiana na makundi,” alisema mwenyekiti wa wilaya moja.
Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma, Feruz Bano ambaye amekuwa kiongozi wa UVCCM Arusha na maeneo mengine zaidi ya miaka 20 sasa, alisema kujiondoa kwa Millya ndani ya CCM kuna sura mbili.
Alizitaja sura hizo kwamba ni kuonyesha jinsi vijana wanavyokosa uvumilivu na pia kutaka hatua zichukuliwe mapema ili kumaliza mpasuko wa viongozi Mkoa wa Arusha.
Alisema wanachama wa CCM Mkoa wa Arusha, wanapaswa kuulizwa ni kwa nini migogoro inazidi ndani ya CCM katika mkoa wao ili kuhakikisha amani na utulivu vinarejea Arusha.
“Mimi nimekuwa kiongozi wa UVCCM Arusha nakumbuka Arusha ilikuwa ni ngome ya CCM, tulikuwa na umoja na mshikamano, lakini inapaswa kujiuliza sasa tumekosea wapi hadi Arusha kuwa ngome ya Chadema?” alihoji.
Mukama: Tutajua cha kufanya
Akizungumzia suala hilo jana, Mukama alisema hakuwa amepata taarifa hizo, lakini akasisitiza kwamba endapo itatokea, chama kitajua cha kufanya.
“Hatujapata taarifa za wenyeviti wengine kujiondoa lakini, tukizipata tutajua tutafanya. Sasa hivi nipo katika kikao cha sekretarieti,” alisema na kukata simu.
Utabiri wa wazee
Kaduma ambaye aliwahi pia kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, alisema ameshazungumza mambo mengi katika kitabu chake alichokiandika kiitwacho, 'Maadili ya Taifa na Hatima ya Tanzania.'
“Ndiyo nilisema hivyo kwenye kipindi, sasa kama yametokea wewe mwenyewe utaona. Nenda kasome kitabu changu, nimeeleza kwa kina. Kama chama kimepoteza maadili unategemea nini?” alisema.
Kwa mujibu wa kitabu hicho cha Kaduma, chanzo cha CCM kuporomoka kimaadili ni kuiacha misingi ya maadili iliyoasisiwa na TANU.
Mtazamo wa wasomi
Baadhi ya wasomi nao walisema kwamba kitendo hicho cha Ole Millya kukihama chama hicho tawala kuwa, ni mwanzo wa kusambaratika.
“Hili ni zao la mizozo na makundi yaliyomo ndani ya CCM,” alisema Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaveri Lwaitama.
Dk Lwaitama aliitaja baadhi ya mizozo hiyo kuwa ni ule uliozuka siku za hivi karibuni baina ya Ole Millya na Chatanda na msigano wa makundi.
“Mizozo hiyo ndiyo iliyochangia CCM kupoteza kiti cha ubunge cha Arumeru Mashariki ambacho kimechukuliwa na Chadema,” alisema.
Dk Lwaitama alisema hakushangaa aliposikia Ole Millya ametangaza kung’oka CCM, kwa sababu kwa jinsi mikwaruzano ndani ya chama hicho tawala inavyozidi kukua, asingekuwa na namna nyingine.
Bashiru Ally kwa upande wake, mbali ya kushangazwa hatua ya kijana kuhama chama tawala alisema: “Kigeni kingine hapa ni kwamba Ole Millya amehama CCM wakati chama hicho na Chadema vikiwa kwenye uhasama na ushindani mkubwa.”
Mshauri wa Chadema, Profesa Mwesigwa Baregu alisema CCM kimekuwa kikitabiriwa kufa na kusema hizo ni dalili kwamba kinameguka vipande kabla ya kusambaratika kabisa.
“Picha ni moja tu, CCM inabomoka. Haijaanza leo. CCM ilitabiriwa kifo kwa sababu hiyo inaweza kufa au kupungua nguvu tofauti na watu wanavyofikiri,” alisema Profesa Baregu.
Alisema jambo hilo ni zuri katika kukuza demokrasia ya nchi na hata utawala bora.
Habari hii imeandaliwa na Mussa Juma, Arusha, Frederick Katulanda, Mwanza, Leon Bahati, Elias Msuya.
0 comments:
Post a Comment