Thursday, April 26, 2012

HALI ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa  (UVCCM), Mkoa wa Arusha imeanza kugubikwa na sintofahamu baada ya jana watu wasiojulikana kuvamia na kuzifunga kwa kufuli ofisi zake za mkoa kuzuia viongozi kuingia.
Pamoja na kufunga ofisi hizo, watu hao wanaodaiwa kuvamia eneo hilo kati ya Saa 4:30 na 5:00 usiku wa kuamkia jana pia walibandika mabango ya kumkataa Katibu wa UVCCM  Mkoa wa Arusha, Abdallah Mpokwa wakimtuhumu kutozingatia maslahi ya jumuiya katika uongozi wake.
Miongoni mwa mabango yaliyobandikwa kwenye mlango na madirisha ya ofisi hizo zilizoko eneo la Kaloleni jijini Arusha yalisomeka “Umoja wa vijana wa CCM Mkoa wa Arusha, hatumtaki Abdallah Mpokwa kwa kuwa mnatumika na Lowasa na si kwa Kanuni za UVCCM”

Bango lingine lililobandikwa mlangoni lilisisitiza tuhuma na madai ya kuondoka na Sh2 milioni zilizochangwa na waliokuwa wabunge wa Jimbo la Arusha mjini, Felix Mrema na mwenzake wa Arumeru Magharibi, Elisa Mollel zinazoelekezwa dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, James Ole Millya aliyehamia Chadema.

“Abdallah Mpokwa na James Millya rudisheni pesa zetu za Saccos ya vijana wa CCM Arusha” ilisomeka moja ya bango.
Waliobandika mabango hayo zaidi ya manne walimtaka katibu huyo wa UVCCM kuhamia Chadema kumfuata Ole Millya badala ya kuendelea kubaki ndani ya CCM huku akimtetea mtu aliyehamia chama hicho kikuu cha upinzani.
Hadi jana hakuna kundi lolote kati ya makundi mawili ya vijana yanayosigana lililodai kuhusika na ufungaji wa makufuli hayo.
Lakini baadhi ya vijana walioonekana dhahiri kumpinga Ole Millya walijitokeza kuzungumza na waandishi wa habari kulaani kauli ya Mpokwa waliyodai ililenga kumsafisha aliyekuwa mwenyekiti wao.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi za CCM mkoa zilizo hatua chache kutoka zile za UVCCM, Ally Shabani maarufu kwa jina la ‘Majeshi’ aliyejitambulisha kuwa ni katibu wa Jumuiya hiyo, Kata ya Moivo, wilayani Arumeru alidai kuna ushahidi unaothibitisha fedha hizo kutolewa na kukabidhiwa chini ya uongozi wa Ole Millya mwaka 2008, lakini hadi leo hakuna taarifa zozote za kuanzishwa kwa Saccos hiyo.

“Kauli ya Mpokwa kuwa  UVCCM haijawahi kuwa na mradi wa Saccos wala kuwapo kumbukumbu za Sh2 milioni zilizotolewa na waheshimiwa Felix na Elisa ni upotoshaji mkubwa kwa sababu fedha hizo zilitolewa hadharani kwenye mkutano wa Baraza lililofanyika Karatu,” alisema Shabani.

Kada huyo wa CCM ambaye ni miongoni mwa viongozi wa UVCCM waliopewa onyo kwa kwenda kinyume na taratibu za chama hicho mwishoni mwa mwaka jana alihoji kwanini katibu huyo anajitokeza kumtetea Ole Millya ambaye ndiye alipaswa kujibu tuhuma dhidi yake.

“Uamuzi wa vijana kufunga ofisi hiyo yao kama tunavyoshuhudia hapa ni sahihi kwa sababu tamko la kumtetea Ole Millya lililotolewa na katibu halina mashiko na kamwe sisi vijana wa Arusha hatuko tayari kuendelea kuongozwa na katibu anayetumikia watu binafsi badala ya chama, aende huko Chadema kwani ni mamluki” aliongeza Shabani huku akikana kuhusika na ufungaji ofisi.

Kijana mwingine Masoud Rajabu ambaye kama Shabani alimrushia madongo Mpokwa huku pia akikana kuhusika na zoezi la kufunga ofisi na kubandika mabango alimwomba mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Steven Wassira kufika haraka mkoani hapa kuokoa jahazi kama alivyofanya mwaka jana wakati kulipotokea minyukano kati ya makundi hayo mawili.

Hata hivyo Rajabu alimwonya Mlezi huyo kuacha tabia ya kufika na kukutana na viongozi pekee aliodai humpotosha na badala yake safari hii akubali kukutana na vijana kwenye kikao cha wazi ili wamweleze jinsi viongozi wengi wa chama hicho mkoani Arusha wanavyoshiriki kukiangamiza na kukipa umaarufu Chadema.

Wakati vijana hao wakikana kuhusika na waliofunga ofisi hizo, muda wote walionekana kuwapanga wenzao kuzilinda kuhakikisha hakuna mtu anayezifungua hali iliyotishia uwezekano wa kutokea machafuko iwapo kundi linalomuunga mkono Mpokwa lingejitokeza kuvunja makufuli na kuondoa mabango.

Hivi karibuni, akizungumza na waandishi wahabari ofisini kwake juzi, Mpokwa akiwa na baadhi ya wajumbe wa Baraza la vijana Mkoa wa Arusha alikanusha aliyekuwa mwenyekiti wake, Ole Millya kuhamia Chadema na Sh 2milioni za mradi wa Saccos la vijana.

Pamoja na kukana tuhuma hizo zilizotolewa na mjumbe wa Baraza la UVCCM Taifa, Mrisho Gambo na Kenenedy Mpumilwa ambaye ni mjumbe wa baraza la mkoa, Mpokwa pia alisema Ole Millya hakupaswa kukabidhi ofisi kwani hakuwa mtendaji wa kila siku bali mwongoza vikao, kauli ambazo zimewakera vijana hadi kumfungia ofisi na kumtaka aondoke

0 comments:

Post a Comment