Sunday, May 5, 2013

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ‘imemlipua’ Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, ikidai kuwa alihusika katika njama za kuhakikisha wanaCCM pekee wanachaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara.

Pia Kambi hiyo imesema hatua ya Wizara ya Katiba na Sheria kuliomba Bunge liidhinishe Sh. bilioni 33.944 kwa ajili ya matumizi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, mbali ya kuwa ni ulaji zaidi, malipo hayo pia yana uvundo na harufu mbaya ya rushwa kwa wajumbe wa Tume.

Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo kuhusu mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2013/2014, bungeni jana.
Makadirio ya bajeti hiyo, yaliwasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo, Mathias Chikawe, ambaye ameliomba Bunge liidhinishe Sh. bilioni 230.7 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo.

Lissu alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina ushahidi unaoonyesha njama hizo za Dk. Migiro.

Alisema Machi 3, mwaka huu, siku mbili tu baada ya Mwongozo wa Tume kuanza kutumika, Dk. Migiro alituma barua pepe kwa wajumbe na watendaji wa Sekretarieti ya NEC ya CCM yenye kichwa cha habari: “MUHIMU!!” kuhimiza kazi ya kuwatia hamasa makatibu wa mikoa wasimamie kikamilifu mchakato wa kuundwa kwa mabaraza hayo.

Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema katika barua pepe hiyo, mbali ya kuhimiza jambo hilo, Dk. Migiro pia aliwataka wajumbe na watendaji hao wa Sekretarieti ya NEC-CCM kuongeza juhudi za ushiriki na kutayarisha makundi husika katika mchakato huo, kama walivyoongea awali.

Kwa mujibu wa Lissu, barua pepe hiyo ya Dk. Migiro inasema: “Naandika kuhimiza kazi ya kuwatia hamasa makatibu wa mikoa wasimamie kikamilifu mchakato wa kuundwa kwa mabaraza ya katiba ya wilaya. Kama mnavyofahamu Tume ya Katiba imeshatoa taarifa rasmi kwenye vyombo vya habari…kuhusu zoezi hili muhimu. Sambamba na hatua hizo za awali tulizochukua baada ya kupata rasimu ya mwanzo ya Mwongozo wa Tume, hivi sasa tunatakiwa tuongeze juhudi za ushiriki wetu na kutayarisha makundi husika kama tulivyokwishaongea.”

Lissu alisema baada ya kuagiza ‘mawasiliano kati ya SUKI na makatibu wa mikoa’ kuhusu mambo ya kufanya, Dk. Migiro alimalizia barua pepe yake kwa maneno: “Tafadhali wanakaliwa msisite kutoa maoni, ushauri na mbinu bora zaidi za kutimiza azma yetu katika suala hili muhimu.”

Lissu alisema ‘wanakiliwa’ wa barua pepe ya Dk. Migiro, ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba; Katibu wa NEC-CCM, Uchumi na Fedha, Zakhia Meghji; Katibu wa NEC-CCM, Oganaizesheni, Mohammed Seif Khatib; na Katibu wa NEC-CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Alisema siku moja baadaye, Nape aliwaandikia ‘wanakiliwa’ wenzake akiwahimiza kuhakikisha taarifa zinapatikana kila siku au walau siku tatu ya hali halisi inavyoendelea katika kila mkoa kutokana na unyeti wa suala hilo.

Kwa mujibu wa Lissu, barua ya Nape kwa ‘wanakiliwa’ wenzake ilieleza kama ifuatavyo: “Nashauri ikiwezekana kwa sababu ya unyeti wa suala hili tupate taarifa kila siku/au walau siku tatu ya hali halisi inavyoendelea katika kila mkoa, ni vizuri idara ikaandaa checklist ya mambo muhimu ya kupima kama mchakato unakwenda vizuri au la! Mfano…idadi ya walioandaliwa kugombea katika kila eneo, idadi ya waliohamasishwa kuhudhuria na kupiga kura, nk.”

Lissu alisema njama za CCM kuteka nyara mchakato wa Katiba Mpya zinahusu pia mchakato wa uhalalishaji wa Katiba Mpya kwenye kura ya maoni.
Alisema Desemba 18, mwaka jana, Katibu wa Sekretarieti ya NEC-CCM, Francis Mwonga, aliwaandikia barua makatibu wote wa CCM wa mikoa kuwapa ‘maelekezo ya kikao cha Sekretarieti ya NEC-CCM ya Taifa na makatibu wa chama hicho wa mikoa, kilichofanyika Dar es Salaam, Desemba 10, mwaka jana’.

Kwa mujibu wa Lissu, sehemu ya maelekezo hayo inasema: “Wakati wa kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mawasiliano yafanywe na wahusika ili vituo vya kupigia kura visiwe mbali sana na wananchi.”

Lissu alisema maneno hayo yameandikwa hata kabla Tume haijamaliza zoezi la kukusanya maoni ya wananchi na tayari Sekretarieti ya NEC-CCM inawaelekeza makada wake mikoani kufanya mawasiliano na ‘wahusika’ juu ya namna ya kupanga vituo vya kupigia kura.

Aidha, alisema Sh. bilioni 33.944, ambazo wizara imeliomba Bunge liidhinishe kwa ajili ya matumizi ya Tume, ni kiasi kile kile kilichoidhinishwa na Bunge mwaka jana
Lissu alisema kiasi hicho ni pamoja na Sh. bilioni 12.193 kwa ajili ya kulipia posho za vikao kwa wajumbe wa Tume 34 na Sekretarieti 160; Sh. bilioni 1.728, ambazo zitalipia posho ya kujikimu kwa ajili ya wajumbe na Sekretarieti wanaposafiri ndani ya nchi kikazi; na Sh. bilioni 1.650 kwa ajili ya kulipa gharama za nyumba za wajumbe na Sekretarieti wanaotoka nje ya Dar es Salaam.

Alisema pia kuna Sh. milioni 18 zinazoombwa kwa ajili ya kughariamia chakula kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti watakaokuwa wamepata maambukizi ya ukimwi; Sh. milioni 60 kwa ajili ya usafiri wa ndani; Sh. milioni 50 kwa ajili ya gharama za malazi kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti ‘wanaposafiri kikazi’; Sh. milioni 423 kwa ajili ya ‘chai na vitafunwa’; na Sh. milioni 50 kwa ajili ya wahudumu wanaosaidia kazi za Tume wakiwa mikoani wakati wa kushiriki kwenye Mabaraza ya Katiba na zoezi la upigaji kura ya maoni.

Pia alisema wizara inaliomba Bunge liidhinishe Sh. milioni 60 kulipia maji kwa matumizi ya ofisi za Tume; Sh. milioni 30 kwa ajili ya kulipia gharama za usafiri wa basi na teksi kwa wajumbe na Sekretarieti watakaposafiri ndani ya nchi kikazi; na Sh. milioni 103 kwa ajili ya kulipia gharama za simu za mikononi.

Alisema wizara pia imeliomba Bunge kuidhinisha posho na ulaji zaidi ya huo kwa ajili ya wajumbe na Sekretarieti ya Tume.

“Ulaji huu mwingine unajumuisha Sh. milioni 604 kwa ajili ya posho kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa Bunge Maalum la Katiba,” alisema Lissu.
Alisema maelezo ya Tume yamejaribu kuhalalisha matumizi ya fedha hizo za ziada kwa kuzibatiza jina la ‘posho ya mazingira magumu’, wakati vikao vya Bunge Maalum la Katiba vitafanyika Dar es Salaam au Dodoma.

“Vile vile, katika ulaji huu mpya zipo Sh. milioni 266 zinazoombwa kwa ajili ya chakula na viburudisho wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba; Sh. milioni 12 nyingine kwa ajili ya huduma za chakula na viburudisho kwa shughuli zinazohusiana na Tume; na Sh. milioni 185 kwa ajili ya kulipia usafiri wa basi na teksi.

Alisema pia kuna Sh. milioni 30 za utengenezaji wa fulana na kofia kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa kushiriki kwenye zoezi za uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya maoni; Sh. milioni 40 nyingine kwa ajili ya utengenezaji wa sare wakati wa maadhimisho mbali mbali ya kitaifa; na Sh. milioni 12 kwa ajili ya posho za kujikimu kwa watumishi wa Tume watakaohudhuria kwenye maadhimisho mbalimbali ya kitaifa.

Lissu alisema zaidi ya hayo, kuna Sh. bilioni 1.307 zinazoombwa kwa ajili ya posho za kujikimu kwa ajili ya wajumbe na Sekretarieti ya Tume wanaposafiri ndani ya nchi wakati wa kushiriki kwenye zoezi la upigaji wa kura ya maoni; na Sh. milioni 218 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya magari ya Tume wakati wa kushiriki zoezi la uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya maoni.

“Kwa ujumla, Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha jumla ya Sh. bilioni 19.039 kwa ajili ya posho za aina mbalimbali na malipo mengine yanayowahusu wajumbe na Sekretarieti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2013/14. Hii ni zaidi ya asilimia 56 ya bajeti yote inayoombwa kwa ajili ya Tume,” alisema Lissu.

Alisema kwa ulinganisho, posho na malipo mengine yanayowahusu wajumbe na Sekretarieti ya Tume, yalikuwa Sh. bilioni 14.633 au asilimia 43 ya bajeti yote ya mwaka wa fedha uliopita.

Lissu alisema hiyo ina maana kwamba, gharama za moja kwa moja za wajumbe na Sekretarieti ya Tume zitaongezeka kwa zaidi ya Sh. bilioni 4.406 au zaidi ya asilimia 30 ya gharama za mwaka jana kama Bunge litaidhinisha maombi hayo.
“Maombi hayo ya mabilioni ya fedha za wananchi yanatoa uvundo na harufu mbaya ya ufisadi, na hayaelezeki na wala kukubalika kwa misingi ya kisheria, na kwa rekodi ya utendaji kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Lissu.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Mabadailiko ya Katiba, Tume ina wajumbe wasiozidi 30 pamoja na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wake.

Kwa maana hiyo, alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua uhalali wa maombi ya Sh. bilioni 12.193 kwa ajili ya posho za vikao kwa wajumbe 34 wa Tume.
Pia inataka kujua wajumbe hao wanne wa ziada ni akina nani na wameteuliwa lini kuwa wajumbe wa Tume, inakuwaje Tume iwe na wajumbe 34 wakati sheria iliyoiunda inataka Tume yenye wajumbe wasiozidi 30?
Alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia inataka kujua uhalali wa Sh. bilioni 1.055, ambazo Bunge linaombwa kuziidhinisha kwa ajili ya posho, chakula na viburudisho na usafiri wa basi na teksi kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba.

Lissu alisema kwa kazi ya mwezi mmoja tu, wajumbe na Sekretarieti ya Tume wanaombewa Sh. bilioni 1.307 kwa ajili ya posho za kujikimu.

Alisema kwa mahesabu hayo, kila mjumbe wa Tume, Katibu na Naibu Katibu pamoja na wakuu wa vitengo saba vya Tume na madereva wa kila mmoja wao, watalipwa wastani wa Sh. milioni 16.756 kwa mwezi mmoja, au Sh. 558,547 kama posho ya kujikimu kwa kila siku moja.

“Mheshimiwa Spika, katika nchi, ambayo wauguzi katika hospitali za umma wanalipwa mshahara wa kuanzia wa takriban Sh. 360,000 kwa mwezi; na walimu wa shule za msingi wanaanzia Sh. 250,000 na wale wa sekondari Sh. 325,000 kwa mwezi. Malipo hayo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yana uvundo na harufu mbaya ya rushwa kwa Wajumbe wa Tume.”

Kutokana na hali hiyo, alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuliambia Bunge ni sheria na kanuni zipi za nchi, ambazo zimetumika kuhalalisha malipo hayo makubwa kwa wajumbe na Sekretarieti ya Tume. 

habari NA MUHIBU SAID
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment