Tuesday, November 13, 2012

Habari hii imeandikwa na Peti Siyame, HabariLeo --

Idara ya Elimu Sekondari wilayani Mpanda mkoani Katavi, imeshitaki wakuu wa sekondari 10 waliokutwa na  wanafunzi 44, waliofeli mtihani wa Taifa wa darasa la saba unaoruhusu kujiunga na   sekondari za Serikali.

Mbali na kuchukua hatua hiyo, tayari imewafukuza na kusitisha masomo  ya wanafunzi hao 44 huku wakuu wa shule wakifikishwa katika Tume ya Utumishi ya Walimu kujibu tuhuma zinazohusishwa na viashiria vya rushwa.

Ofisa Elimu ya Sekondari wa Wilaya ya Mpanda, Venance Nyamwale  akizungumza jana kwa simu, alikiri kuwa pamoja wa wakuu hao kufikishwa kwenye Tume hiyo,  bado  wanaendelea  na kazi  katika nafasi zao wakisuburi uamuzi wa Tume.
Walimu hao wakuu ni wa sekondari za Usevya, Mamba, Kasokolo, Mpanda ndogo, Ikola, Kabungu, Inyonga, Sitalike, Machimboni na Kambi  ya Wakimbizi ya Mishamo.

Nyamwale alisema Kamati Maalumu  iliyohusisha viongozi waandamizi  kutoka wilayani kwa maagizo ya Wizara ya  Elimu  na Mafunzo  ya Ufundi  Stadi, ilitembelea sekondari 23  wilayani  humo  kuanzia Julai 13, hadi Agosti 2 na kubaini upungufu katika shule hizo 10.

Akifafanua, Nyamwale alisema wanafunzi hao waliokuwa wakisoma kidato cha kwanza ni watano, wanne wa kidato cha pili ambao pia walisajiliwa na kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha pili; 13 wa kidato cha tatu na 14 wa kidato cha nne.

Akifafanua, alisema wanafunzi  hao wote ilibainika hawakufaulu  mitihani  yao ya elimu ya msingi na majina yao hayakuwa kwenye kitabu cha Serikali mkoani Katavi  chenye orodha  ya wanafunzi waliofaulu mtihani wa Taifa  wa kumaliza  elimu  ya msingi.  

“Pia tulifuatilia kama Kamati  Maalumu  ili kuona  kama  walikuwa  na uhamisho rasmi  kutoka  mikoa mingine,  lakini  hata nyaraka  hizo  hazipo  kabisa.

“Naweza  kukiri kuwa pamoja na kukosa ushahidi  wa moja kwa moja, vipo  viashiria  vya rushwa katika udahili wa wanafunzi  hao  wasiokuwa na sifa.

“Inawezekana  wapo  watoto  wa walimu,  marafiki  zao na watumishi serikali lakini Tume  tuiachie wajibu wake  ifanye kazi  kwa uhuru ,“ alisisitiza.

Pia  alibainisha kuwa  tayari Mamati  Maalumu  iliwasilisha taarifa hiyo  rasmi  kwa  Mkaguzi wa Elimu  Kanda  Mjini  Mbeya  tangu Agosti. 


0 comments:

Post a Comment