Monday, November 19, 2012

na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Rufani nchini imepanga kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyomwachilia huru aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP), Abdallah Zombe, na wenzake, ambayo itaanza kusikilizwa Desemba 11.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao iliyotolewa na mahakama hiyo, rufaa hiyo inayosubiriwa kwa shauku kubwa na umma, itaanza kusikilizwa kuanzia saa 3 asubuhi mahakamani hapo jijini Dar es Salaam.
Aidha ratiba hiyo inaonyesha jopo la majaji watatu ambao ni Jaji William Mandia, Nathalia Kimaro na Jaji Catherine Oriyo ndiyo wamepangwa kuikisiliza rufaa hiyo yenye namba 254/2009 iliyokatwa Oktoba 6, 2009.
Katika rufaa hiyo, DPP ametoa sababu 11 ambazo ni kuwa Jaji Massati alikosea kisheria kuwaachilia huru washtakiwa na kwamba anaiomba Mahakama ya Rufaa itengue hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Agosti 17, 2009, kwa sababu ina mapungufu mengi ya kisheria ikiwamo jaji huyo kujielekeza vibaya katika kutoa hukumu ile iliyowaachilia huru washtakiwa.
Zombe na wenzake, walikuwa wakidaiwa kuwa Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande, ulioko Mbezi Luis, jijini Dar es Salaam waliwaua wafanyabiashara: Sabinus Chigumbi au Jongo na ndugu yake Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe, pamoja na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva teksi.
Mbali na Zombe aliyekuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa, washtakiwa wengine walikuwa ni ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Noel Leonard, Konstebo Jane Andrew, Koplo Nyangerela Moris, Konstebo Emanuel Mabula na Koplo Felix Sedrick.
Wengine walikuwa ni Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo, Koplo Rashid Lema (aliyefariki kabla ya kujitetea), Koplo Rajabu Bakari na Koplo FestusGwabisabi.

0 comments:

Post a Comment