Wednesday, November 7, 2012

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) amemtaka Rais Jakaya Kikwete kufuta haraka uteuzi wa baadhi wa majaji, akisema hawana sifa na kwamba kinyume cha hapo, atawasilisha bungeni hoja maalumu ya kumshitaki Rais.

Aidha, amemtaka Spika, Anne Makinda kutangaza bungeni uchunguzi uliofanywa dhidi yake na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi baada ya kutoa tuhuma bungeni dhidi ya majaji.

Alisisitiza kuwa umma unapaswa kujua ukweli, kwani baada ya baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali kukanusha bungeni na hatimaye kuundwa kamati, sasa ni wakati ukweli ujulikane, huku akitamba kuwa ana uhakika na alichokisema.

Alisema hayo katika ofisi ya Kambi ya Upinzani bungeni mjini hapa jana akisisitiza kuwa majaji anaowalalamikia wamo vihiyo, wasio na maadili na wengine uteuzi wao umekiuka Katiba ya nchi.

Alisema mmoja wa majaji anaotaka aondolewe hana sifa za kielimu kuwa Jaji, akisema hana Shahada ya Kwanza katika Sheria, huku akiongeza kuwa Jaji huyo wa Mahakama ya Rufani nchini kwa sasa ameingia darasani kusomea Shahada ya Sheria.

“Kama hana hata Shahada ya Sheria, anakaaje mahakamani, anatoaje haki kwa mujibu wa sheria ambayo hajasomea?”

Alihoji na kuongeza kuwa wengine wawili si waadilifu, akisema waliwahi kukamatwa wakihonga mahakimu wakati huo wakiwa mawakili.

“Majaji wa aina hiyo watamtendea nani haki. Nani ambao watakuwa na imani mashauri yao yatakapofika mbele yao? Mfumo wetu wa utoaji haki uko salama kiasi gani na majaji wa aina hii?”Aliendelea kuhoji.

Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alidai pia wamo majaji wasiojua kuunda hata sentensi moja kwa lugha ya Kiingereza, huku akimtaja mmoja kuwa alipata ujaji miaka mitatu baada ya kuhitimu Shahada yake Chuo Kikuu Huria na kuanza kazi, ilhali utaratibu unataka awe amefanya kazi angalau miaka 15.

Wengine aliodai hawastahili kufanya kazi za ujaji ni majaji wastaafu wanaofanya kazi kwa mikataba, lakini bila kuapa. Alidai kuwa karibu majaji wote walioongezwa mkataba na kuanza kazi bila kuapa tena, wanafanya kazi kinyume cha sheria.

Aliongeza kudai kwamba kutokana na uzito wa kashfa hizo, Rais Kikwete afute uteuzi wao haraka iwezekanavyo, vinginevyo ataanzisha mchakato wa kuwasilisha hoja maalumu ya kumjadili Rais na uteuzi wa majaji.

Alisema ili kutimiza azma yake, anapaswa kukusanya asilimia 20 ya saini za wabunge, sawa na wabunge kati ya 70 na 72, ili kuwasilisha hoja kwa kuwa sasa kanuni haziruhusu kumjadili Rais ndani ya Bunge bila hivyo.

Aliongeza kuwa, njia pekee ya kumaliza tatizo hilo ni kwa Rais kutengua uteuzi wao, “Hatuwezi kuwa na Mahakama chafu yenye majaji vihiyo, wasio na maadili na ambao wananchi wanakosa imani nao.”

Aidha, Lissu alidai kuwa, mmoja wa majaji mwenye jina kubwa nchini, ana kashfa ya kughushi umri wa kuzaliwa ili aendelee kubaki madarakani kwa muda mrefu, akimtuhumu kuwa amediriki hata kunyofoa nyaraka muhimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikosoma ili kuficha taarifa muhimu zinazomhusu, “Tunamfahamu, hatuna shaka ya chanzo chetu…tunamtaka azirudishe, vinginevyo tutamtaja hadharani. Na tukimtaja, hapatakalika,” alionya na kudokeza kuwa ameghushi miaka mitano.

0 comments:

Post a Comment