Wednesday, October 10, 2012

Habari imeandikwa na Khatib Suleiman, HabariLeo, Zanzibar --- SHIRIKA la Umeme la Zanzibar (ZECO), limesema linadaiwa Sh bilioni 25 ikiwa ni malimbikizo ya madeni ya kununua nishati ya umeme kutoka kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Akizungumza na waandishi wa habari Gulioni jana, Meneja Mkuu wa ZECO, Ali Hassan Mbarouk alisema deni hilo linatokana na malimbikizo mbalimbali ya matumizi ya umeme wanaonunua kutoka kwa Tanesco kwa muda mrefu sasa ikiwamo kupanda kwa bei ya nishati hiyo mara kwa mara.

Mbarouk alisema kazi kubwa inayofanywa na Menejimenti ya Shirika la Umeme la Zanzibar kwa sasa ni kuhakikisha wanalipa deni hilo awamu kwa awamu kadri ya uwezo wa shirika utakavyoruhusu, “Tumeanza mikakati ya kulipa deni letu kutoka kwa Tanesco awamu kwa awamu ili kuhakikisha tunapata huduma nzuri na sahihi za kununua umeme bila ya usumbufu,” alisema Mbarouk.

Alisema yalikuwapo malalamiko kutoka kwa upande wa ZECO katika deni la awali lililofanyiwa marekebisho na deni walilokuwa nalo kwa sasa ndiyo sahihi na wapo katika juhudi za kulilipa.

Hivi karibuni, ZECO ilipandisha bei ya umeme kutoka kwa wateja wa aina mbalimbali wakiwamo wa kawaida pamoja na wanaofanya biashara, hatua ambayo ilizusha malalamiko makubwa. Uongozi wa shirika hilo ulisema umepandisha bei ya kununua umeme kwa wananchi baada ya bei hiyo kupanda kutoka kwa wazalishaji wa umeme huo.

Hata hivyo, Mbarouk alisema shirika linatazamiwa kuwa katika hali nzuri ikiwamo kulipa madeni yake mara baada ya kuanza kazi kwa mradi wa umeme wa Shirika la Milenia (MCC).

Akifafanua zaidi, Mbarouk alisema mradi huo utakuwa mkombozi kwa kukiwezesha kisiwa cha Zanzibar kuwa na umeme wa kutosha wa megawati 100 ambazo zinatosha kwa mahitaji ya wateja majumbani pamoja na wawekezaji wa sekta ya utalii na viwanda.

Alisema wanapata malalamiko mengi ya kukatika kwa nishati hiyo kutoka kwa wateja wake ikiwamo kutoka kwa wamiliki wa sekta ya hoteli za kitalii na viwandani.


0 comments:

Post a Comment