Thursday, October 11, 2012

BAADHI ya wananchi, wakiwemo wasomi, wanasiasa na wanaharakati mbalimbali, wamekosoa ripoti ya Serikali kuhusu mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten mkoani Iringa, Daud Mwangosi.

Ripoti hiyo imepingwa sambamba na ile ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), wakisema kuwa ripoti hizo hazijatoa majibu kuhusiana na kifo hicho na kwamba hayo ni matumizi mabaya ya fedha.

Maoni hayo yamekuja siku moja baada ya ripoti mbili za uchunguzi wa kifo cha mwandishi huyo kutangazwa hadharani jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza na gazeti la MTANZANIA kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kuwa ripoti ya Serikali imeonyesha udhaifu mkubwa na kwamba imedhihirika wazi namna inavyoficha ukweli.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azaveli Lwaitama, alisema ripoti zote mbili zimewahadaa wananchi na kwamba huko ni sawa na kuwadharau Watanzania.

“Ni dhahiri kuwa ripoti ile haikuwa na jambo lolote la maana, kwa sababu kitendo cha kudai kuwa polisi hawakushiriki katika mauaji wa Mwangosi, ni uongo ambao hauwezi kuaminiwa na Watanzania. Ni ripoti ambayo imeficha ukweli kwa Watanzania wakati picha za tukio hilo zipo na zinaeleza wazi namna polisi walivyohusika,” alisema.

Dk. Lwaitama alisema ni bora Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, angeitisha mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake kuliko kutoa kitu alichokiita ripoti.

Kuhusu ripoti ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), Dk. Lwaitama alisema ripoti hiyo haikuwa na tofauti kwa sababu mambo mengi yaliyobainishwa katika ripoti hiyo tayari yanajulikana kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba, alisema kituo hicho kimeshangazwa na ripoti hizo, hususan ile ya Serikali, “Ingawa hatujaipitia vizuri, bado tunaendelea na uchunguzi, lakini kikubwa tumeshangazwa sana na baadhi ya nukuu za ripoti ya Nchimbi kuwa polisi hawakuhusika na tukio hilo.

“Kwa sababu hili ni tukio la wazi, kuna ushahidi wa picha ambao unadhihirisha wazi namna polisi walivyohusika. Ripoti ya MCT ni nzuri, tunaiunga mkono kwa sababu imeeleza ukweli, hakuna kitu kilichopindishwa ingawa hakuna kitu kipya vilevile katika ripoti hiyo. Lakini kwa kuwa tunaendelea na uchunguzi wa ripoti hizo, Ijumaa wiki hii tunatarajia kutoa tamko letu kuhusu ripoti hizo mbili,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema matukio ya umwagaji damu kama yaliyotokea kwa Mwangosi yanatokana na chuki za kisiasa ambazo chanzo chake kikuu ni mapungufu katika sheria namba tano ya vyama vya siasa.

Alisema licha ya upungufu huo, Tume ya Uchaguzi (NEC) nayo inabidi kupewa uhuru wa kujitegemea katika kutekeleza majukumu yake, “Kwa kweli ripoti zote sijazipitia, lakini kuna umuhimu wa kufanyia jambo hili utafiti ili kupata njia sahihi itakayosaidia kuondokana na tatizo la umwagaji damu. Kuendelea kwa utamaduni huo kutaliingiza taifa katika hali mbaya zaidi na hivyo, tumeamua kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutafuta njia sahihi yenye kuliweka taifa katika mfumo mzuri. Tumekubaliana kukutana kila baada ya miezi mitatu... kikubwa ni kuhakikisha amani ya taifa inaendelea kudumishwa,” alisema.

Katika hatua nyingine, MTANZANIA ilizungumza na mwananchi wa kawaida aliyejitambulisha kwa jina la Juma Khalfan, ambaye aliiponda ripoti iliyotolewa na Serikali, “Hiyo haikuwa ripoti ila ni taarifa tu...ambayo imejaa uhuni na dharau kwa wananchi, wasijitetee kuwa jambo hilo lipo mahakamani. Kama walikuwa wanajua lipo mahakamani kulikuwa na umuhimu gani wa kuendelea na uchunguzi?” alihoji.

CHADEMA

Kwa upande wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kinaendelea kuchambua ripoti zote mbili na kwamba muda wowote kitatoa taarifa yake.

Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, alisema baada ya ripoti hizo kutolewa chama chake kinafanya uchambuzi wake, “Tangu awali chama tulisema hatuna imani na tume ya Dk. Nchimbi, tulijua haiwezi kuleta ukweli, tulijua tangu awali tume itakuja na ujanja wao wa kila siku, subirini tutawaita siku yoyote,” alisema kwa ufupi.

Mtuhumiwa akwama kupelekwa mahakamani

Mtuhumiwa wa mauaji ya Mwangosi, aliyetakiwa kufikishwa mahakamani jana, hakuweza kufikishwa kutokana na sababu zilizoelezwa kuwa anaumwa.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Michael Luwena, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Iringa.

Katika maelezo yake aliyoyasoma mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Dyness Lyimo, alisema mtuhumiwa huyo hakuweza kufikishwa mahakamani hapo kutokana na taarifa za ugonjwa.

Mtuhumiwa huyo, Pasificus Cleophace Simon (23) alitakiwa kufikishwa kwa mara ya tatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kutokana na tuhuma inayomkabili. Pasificus anadaiwa kwamba alimuua kwa makusudi mwandishi huo katika ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa Septemba 2, mwaka huu.

Tofauti na wakati uliopita mahakamani hapo kuwepo na ulinzi mkali na udhibiti kwa waandishi kupiga picha, huku baadhi yao wakitishiwa kupigwa, hali ya jana ilikuwa tofauti, huku idadi ya askari waliokuwa wakifika katika uwanja huo wa mahakamani nao wakipungua.

---
Habari hii imeandikwa na:
Gabriel Mushi, Evans Magege na Benjamin Masese (Dar) na Oliver Richard (Iringa) via gazeti la MTANZANIA


0 comments:

Post a Comment