Sunday, October 21, 2012

Sasa tutaingilia maandamano yoyote ya kuhatarisha amani(gazeti la Habari Leo)

Picture
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe (picha ya maktaba kutoka kwenye blog ya Mdimuz)
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limewataka wananchi kulinda amani iliyopo na kuepuka vurugu zinazohatarisha usalama wa nchi.

Kauli hiyo, imekuja siku moja baada ya waumini wa dini ya Kiislamu jijini Dar es Salaam kuandamana kwenda Ikulu, ili  kuishinikiza Serikali kumwachia  Sheikh Issa Ponda na wafuasi wake 49 waliokamatwa wiki iliyopita kwa tuhuma mbalimbali .

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema hatua ya wanajeshi kujitokeza katika kuzima  vurugu zilizotokea jijini juzi, ililenga katika  kuwaonyesha wananchi kwamba JWTZ ipo kikazi zaidi, na kwamba anayetaka vurugu atashughulikiwa kisheria, “Juzi tulionyesha‘talent show force’ ili watujue kama tupo kazini, hata kama wametuona tupo kimya, hatuna mzaha katika kulinda na kusimamia ulinzi na usalama wa taifa hili, kwa hiyo tulikuwa kwenye sehemu ya utekelezaji wa majukumu yetu, na kwamba atakayekwenda kinyume tutamshughulikia,” alisema Mgawe.

Alisema zoezi hilo ni endelevu kwa maandamano yoyote yatakayoonyesha dalili za kuhatarisha usalama wa nchi.

Msemaji wa huyo wa JWTZ alisema wanajeshi watashiriki kikamilifu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanafuata sheria na taratibu zilizopangwa, bila ya kuathiri usalama wa nchi.

Alisema kwa sasa wanasubiri kibali cha polisi cha kuhusu kuhitaji msaada ili waweze kuungana nao katika kushughulikia maandamano yenye lengo la kuhatarisha amani na utulivu, “Tunawataka wananchi kufuata sheria na taratibu zilizopo na kuepuka kuhatarisha amani ya nchi, kama wanataka tuingie kazini tutafanya hivyo, ila tunachowaasa ni kufuata taratibu zilizopo,” alisisitiza.

Katika vurugu za juzi, watu 53 walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki kwenye maandamano. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, watu hao watafikishwa mahakamani Oktoba 22 mwaka huu.
---
Imeandikwa na Patricia Kimelemeta na Pamela Chilongola via Mwananchi

CHADEMA yaleza chanzo cha vurugu za Waislamu Dar
(gazeti la Tanzania Daima)

Picture
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Prof. Abdallah Safari akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam. (picha: Habari Mseto blog)
IMEELEZWA kuwa vurugu za kikundi cha Waislamu zilizotokea Mbagala hivi karibuni ni matokeo ya muda mrefu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kupuuzia kushughulikia matatizo yao.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari, wakati wakizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama hicho dhidi ya vurugu za kidini zilizotikisa Jiji la Dar es Salaam wiki hii.

Marando alisema kuwakamata viongozi wa Kiislamu pasipo kushughulikia matatizo yao si njia sahihi kwani kuna hatari ya kuzalisha Waislamu wengi wenye msimamo mkali dhidi ya serikali na kuifanya nchi kutotawalika.

“Kabla ya uhuru Waislamu walikuwa na taasisi zao serikali ya TANU, kwa ajili ya kulinda masilahi yake ikavifutilia mbali na kuamua kuwawekea Waislamu Bakwata na kutunga sheria za kuongoza, nataka mtambue matatizo ya Waislamu wote hayasimamiwi na BAKWATA, waitwe Waislamu na waulizwe shida zao,” alisema Marando.

Aliongeza kuwa kabla ya uhuru Waislamu walipambana kwa kuamini walikuwa wakinyanyaswa na kwamba baada ya uhuru hawakuona mabadiliko yoyote, hivyo wanalazimika kujitafutia uhuru mwingine mbali na ule wa kutoka katika mikono ya wakoloni.

Alisema serikali isisubiri vifo vitokee ndiyo ione umuhimu wa kushughulikia matatizo hayo na badala yake ijipe muda wa kukaa na makundi yote kutafuta muafaka.

“Siamini kama kuna tatizo baina ya Waislamu na Wakristo bali mfumo wa serikali unawalazimisha Waislamu kuamini hivyo kwa kuwa wametengwa, hawasikilizwi hawathaminiwi na sasa wako kama yatima kwanini?” alihoji Marando.

Akizungumzia utekwaji wa watu unaoendelea nchini, Marando alisema serikali haiwezi kukwepa lawama hizo na kwamba matamshi ya viongozi wa Ikulu kuwa hawamfahamu Ramadhani Ighondu ni hadaa kwa Watanzania.

“Sheikh Farid alipotea katika mazingira ya ajabu na hili ni jukumu la serikali kujua hatima ya raia wake lakini leo tunaona vyombo vya ulinzi vikisema havihusiki wala havina habari na kupotea kwake, haya ni majibu kama yale yale yaliyotolewa kwa Dk. Ulimboka,” aliongeza Marando.

Kwa upande wake Profesa Safari alizungumzia kitendo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuingilia kati kutuliza ghasia inaonesha kuwa serikali imeshindwa kuongoza nchi kwa kufuata sheria.

“Jeshi la Wananchi limefuata nini mtaani? Kuna tishio gani la amani inayowalazimisha wao kuingia mtaani? Kwa kuwa tunafahamu suala la kutangaza hali ya hatari na jeshi kuingia mtaani lazima liwe na baraka ya Bunge,” alisema Safari.

Aliongeza kuwa mara nyingi serikali imeshauriwa kutatua migogoro baina ya Waislamu na serikali, lakini ushauri huo umekuwa ukipuuzwa.

---
Imeandikwa na Abdallah Khamis via TanzaniaDaima
Picture
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabele Marando akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo juu ya matukio makubwa yaliyotokea nchini Tanzania yakiwemo yale ya kuchomwa kwa makanisa, maandamano ya wafuasi wa dini ya Kiislamu pamoja na tukio la kutoweka kwa Sheikh Farid wa Zanzibar ambaye kwa sasa amepatikana akiwa hai. (picha: Habari Mseto blog)

Vurugu za Waislamu Dar, Zanzibar: Chadema yaibomoa serikali(gazeti la Nipashe)


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeituhumu Serikali kuwa ndiyo inayochochea udini kwenye siasa zinazosababisha vurugu na chuki zilizoenea nchini.

Kadhalika kimeilaumu kuwa imeshindwa kushughulikia madai na malalamiko ya Waislamu kwa miongo mingi hatua iliyochochea vurugu za Waislam  katika miji ya  Zanzibar na Dar es Salaam wiki hii.

Wanasheria waandamizi wa CHADEMA, Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando, walitoa madai hayo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wanahabari ulioitishwa kuzungumzia vurumai na maandamano ya kidini.

Kuchochea dini kwenye siasa:

Marando alisema serikali ilizua kuwa chama cha CUF ni cha kidini na ni cha  Waislamu  pia inaeneza propaganda kuwa Chadema ni cha Wakristo hasa Wakatoliki.

Aliongeza kuwa madai hayo yanatolewa baada ya CUF kupata nguvu iliyoifanya kuwa tishio kwa CCM na serikali yake  wakati Chadema  inadaiwa kuwa ya kidini baada ya kuibuka kuwa chama tarajiwa chenye mwelekeo wa kutwaa  dola.

Wakizungumza kwa kupokezana, Safari na Marando waliitaka serikali kusikiliza malalamiko ya Waislam  iliyoyapuuza kwa miongo mingi badala ya kulikumbatia Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) na kuupuuza asasi nyingine.

Waliitaka kuwakutanisha Waislamu na asasi zote kusikiliza malalamiko yao na kupata ufumbuzi badala ya kutumia jeshi na polisi kuzima maandamano ambayo yanafanyika kutokana na mlundikano wa chuki nyingi zinazotokana na Waislamu kutosikilizwa.

Profesa Safari alisema yapo malalamiko ya Waislam ambayo hajasikilizwa tangu Uhuru na kila siku yanaongezeka mfano wanataka Mahakama ya Kadhi, kujiunga na Muungano wa Nchi za Kiislam (OIC) na pia kushinikiza kipengele cha kutaja imani ya mtu kuingizwa kwenye sensa ya watu na makazi.

Wakizungumzia kutoweka na kuibuka kwa kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar,  Sheikh Farid Hadi Ahmed, waliishangaa serikali ‘kumteka’ na kutangaza kuwa taasisi  za ulinzi na usalama hazijui aliko.

Marando alihoji: “Inakuwaje serikali ijidanganye kuwa haijui alipo Sheikh Faridi na kusababisha  vurugu, kuchoma na kuharibu mali na hata  kifo cha polisi  Said Abdularahman aliyepigwa mapanga kuhusiana na tukio hilo?”

CHADEMA iliitaka serikali kuwa na uwazi na kueleza alikokuwa Sheikh Farid ambaye aliibuka juzi na kuvieleza vyombo vya habari kuwa alikuwa anahojiwa na Usalama wa Taifa wakati polisi Zanzibar ilisema haijui aliko.

---
Linki: Nipashe

0 comments:

Post a Comment