Saturday, September 15, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MTIHANI WA KUMALIZA ELIMU YA MSINGI MWAKA 2012

 Ndugu wananchi,

Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 na 20 Septemba, 2012.  Jumla ya wanafunzi 894,881 wamesajiliwa  kufanya mtihani huo ambapo   wavulana ni  426,285 sawa na asilimia 47.64  na wasichana ni 468,596  sawa na asilimia 52.36. Aidha, kati ya  wanafunzi hao, wapo wanafunzi 874,379  watakaofanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi 20,502 watafanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo waliyoitumia kujifunzia.  Wanafunzi wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani ni 92 wakiwemo wavulana 53 na wasichana 39.  Watahiniwa wenye uono hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa ni 495, kati yao wavulana ni 238 na wasichana ni 257.

Mtihani huu utafanyika kwa mara ya kwanza kwa kutumia teknolojia mpya ya ‘Optical Mark Reader’ (OMR), ambapo watahiniwa watatumia fomu maalum za OMR kujibia mtihani na majibu yao yatasahihishwa kwa kutumia kompyuta.  Masomo yatakayotahiniwa katika mtihani huo ni Kiswahili, English Language, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.

Ndugu wananchi,

Maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani, kusambazwa kwa fomu maalum za   kujibia mtihani na nyaraka zote zinazohusu mtihani huo. Mafunzo maalum kwa ajili ya matumizi ya fomu za OMR yamefanyika kwa lengo la kuwaandaa watahiniwa, wasimamizi pamoja na viongozi wa elimu katika ngazi mbalimbali ili waweze kutumia ipasavyo teknolojia hiyo.

Ndugu wananchi,

Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwa kuwa unahitimisha ngazi ya Elimu ya Msingi na kufungua milango kwa ajili ya elimu ya sekondari.  Hivyo, matokeo ya mtihani huu hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na Elimu ya Sekondari.   Kwa kuzingatia umuhimu wa mtihani huo, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa taratibu zote za mitihani zinazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa  mazingira yanakuwa salama na tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu.

Napenda pia kutoa wito kwa wasimamizi wa mitihani kufanya kazi yao ya kusimamia kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.  Wapo baadhi ya wasimamizi ambao wamekuwa wakishiriki katika kuwasaidia watahiniwa kufanya udanganyifu kwenye mitihani.   Napenda kuwaasa tena wasimamizi kujiepusha na vitendo hivyo vya udanganyifu kwani serikali haitasita kuchukulia hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za mitihani.

Kwa upande wa wanafunzi watakaofanya mtihani mwaka huu, ninaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri katika kipindi chote cha miaka saba ya Elimu ya Msingi.  Hivyo, ni matarajio yangu kuwa mtaufanya mtihani huo kwa utulivu na kuzingatia taratibu zote za mitihani ili matokeo ya mtihani yaoneshe uwezo wenu halisi kulingana na maarifa na ujuzi mliopata katika Elimu ya Msingi.  Serikali inawaasa wanafunzi wote kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu katika mtihani kwani watakaobainika watafutiwa matokeo yao yote ya mtihani.

Ndugu wananchi,

Natoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha kwamba mtihani huo  unafanyika kwa amani na utulivu wa kutosha bila usumbufu unaoweza kusababishwa na shughuli za kijamii hasa katika maeneo ya jirani na shule.

Mwisho, napenda kuwaasa tena wanafunzi, walimu na wananchi wote kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya udanganyifu wa aina yoyote katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi. Nawaomba pia raia wema wasisite kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapoona au kuhisi mtu au kikundi cha watu kinajihusisha na udanganyifu wa aina yoyote katika mtihani huo.

Nawatakia watahiniwa wote heri na fanaka katika mtihani utakaofanyika tarehe 19 na 20 Septemba, 2012.

MHESHIMIWA PHILIPO AUGUSTINO MULUGO (MB)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI



0 comments:

Post a Comment