Tuesday, August 28, 2012

Waandishi Wetu

MCHAKATO wa kuwania uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeshika kasi baada ya mahasimu wawili wilayani Nzega mkoani Tabora, Hussein Bashe na Dk Hamisi Kigwangala kujitokeza kwa nyakati tofauti kuwania nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).


Mbali na mahasimu hao wawili, vigogo wengine waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho ni Mwenyekiti wa CCM mkoani Dodoma, William Kusila na Mbunge wa Bunge la Afrika
Mashariki, Adam Kimbisa ambao wanataka kuwania uenyekiti wa mkoa huo.


Kigwangala ni Mbunge wa Nzega ambaye upinzani kati yake na Bashe, ulianza katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, baada ya Bashe aliyeshika nafasi ya kwanza katika kura za maoni ndani ya CCM, kutopitishwa kwa madai kuwa hakuwa raia wa Tanzania.


Kigwangala ambaye alishika nafasi ya tatu katika kura za maoni, alipewa nafasi ya kugombea ubunge, badala ya Lucas Selelii ambaye alishika nafasi ya pili.


Akichukua fomu, Bashe alisema imani yake ni kuwa wanachama wa CCM watachagua kiongozi bora ambaye atakisaidia kufanikisha maendeleo na siyo wale ambao wanataka uongozi kama sehemu ya majaribio.

“Tunapochagua viongozi wa chama, hatuchagui mtu kwa majaribio. Kuna watu wanapita mitaani na kufanya kampeni ili wachaguliwe wao na ndugu zao ambao nao wanagombea. Chama siyo mali ya familia, naombeni sana msichague viongozi kwa misingi ya kifamilia,” alisema.

Dodoma
Kusila alichukua fomu huku akitamba kuibuka tena mshindi. Alijigamba kuwa chini ya uongozi wake, CCM iliimarika hivyo haoni ni sababu zipi zitakazowafanya wanachama wasimchague tena.

Hadi jana, ni Kusila na Kimbisa waliokuwa wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo. Tofauti na ilivyokuwa kwa Kimbisa ambaye aliongozwa na wazee maarufu wa mkoani Dodoma, Kusila jana alikuwa na msafara wa wabunge na madiwani akionyesha kuwa nguvu yake iko kwa upande wa viongozi walioko madarakani.

“Nimewezesha kuwapo kwa mshikamano, utulivu wa kisiasa katika mkoa na zaidi ya hapo kufanya chama kushinda kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010. Kwa mara ya kwanza mkoa wetu ulikuwa wa kwanza kitaifa kwenye uchaguzi huo. Sasa nataka kuhakikisha kuwa hatugawanyiki, bali tunabaki na mshikamano wetu,” alisema Kusila.

Dar es Salaam
Wanachama 192 wa CCM, Wilaya ya Kinondoni wamechukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kinondoni, Edwin Milinga alisema nafasi ya mwenyekiti inawaniwa na watu 10, makamu mwenyekiti imeombwa na wanachama zaidi ya watano.

Alisema nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu ya wilaya imeombwa na watu 72, mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa imeombwa na watu 70.

Bunda
Mwandishi wa habari, Cyprian Musiba (34) naye amechukua fomu ya kugombea ujumbe wa Nec ya CCM, kupitia Wilaya ya Bunda.Musiba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Gazeti la Afrika Leo, alichukua fomu hiyo katika Ofisi ya CCM ya Wilaya ya Bunda jana. Mwaka 2010, Musiba aliomba kuteuliwa na CCM kuwa mgombea ubunge Jimbo la Mwibara na kushindwa kwenye kura za maoni.Katibu wa CCM Wilaya ya Bunda, Sosteness Mitti alisema hadi sasa wanachama 14 wameshachukua fomu kuwania nafasi hiyo.


Mbeya
Rais wa Chama cha Makandarasi Wenyeji Tanzania (TLCO), Kura Mayuma amejitokeza kuwania uenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya... “Nimechukua fomu na kugombea nafasi hii, lengo kuu ni kusaidia jamii ili kutokuwapo na sheria kandamizi zitakazowakwamisha wananchi kujikita katika shughuli mbalimbali za maendeleo.”

Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Maganga Sengelema alisema chama hicho kimejipanga vyema kupata viongozi ambao watakitetea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014.

Habari hii imeandikwa na Frederick Katulanda, Nzega; Israel Mgussi, Dodoma; Hawa Mathias, Mbeya; Patricia Kimelemeta, Dar na Ahmed Makongo, Bunda.

0 comments:

Post a Comment